Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msuva apania kuweka heshima Saudi Arabia

Muktasari:

  • Kabla ya kujiunga na Al Najmah, Msuva amewahi kuzichezea pia Azam, Yanga, Difaa El Jadida, Wydad Casablanca, Al Quadsiah na JS Kabylie

Dar es Salaam. Mshambuliaji Saimon Msuva amesema kuwa hatoruhusu historia ya kucheza kwa muda mfupi soka la kulipwa Saudi Arabia ijirudie akitambia kubebwa na uzoefu wa soka na mazingira ya nchini humo ambako ataelekea siku chache zijazo.

Nyota huyo wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' hivi karibuni alikamilisha uhamisho wa kujiunga na Al Najmah inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na JS Kabylie ya Algeria.

Hii ni mara ya pili kwa Msuva kucheza soka la kulipwa nchini humo ambapo mara ya kwanza aliitumikia Al-Qadsiah inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kama ilivyo kwa Al Najmah.

Hata hivyo Msuva hakudumu sana katika timu ya Al-Qadsiah ambapo aliichezea kwa msimu mmoja tu kabla ya kuachana nayo na kujiunga na Kabylie ambayo hivi karibuni alivunja mkataba wa kuendelea kuichezea.

Msuva alisema kuwa anaamini kilichotokea nyuma hakitojirudia safari hii kwani tayari ana uzoefu mkubwa wa soka la Saudi Arabia na maisha yake kijumla.

"Malengo yangu ni kucheza kwa muda mrefu kule Saudi Arabia. Sina wasiwasi na hilo kwa sababu naifahamu vyema ile ligi daraja la kwanza na nilishacheza. Nilicheza pale kwa msimu mmoja na bahati mbaya uongozi wa timu ulibadilika hivyo sikuweza kuendelea ingawa nilitamani kucheza kwa muda mrefu zaidi.

"Lakini kwa sasa nina uzoefu wa kule na nimejiandaa kuhakikisha malengo yangu yanatimia. Kikubwa sio ligi nyepesi hivyo jambo la msingi ni kupambana ili kuweza kuisadia timu yangu," alisema Msuva.

Mshambuliaji huyo alisema kuwa anatamani kuona wachezaji wengi wa Kitanzania wanatoka kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa ili waimarike na kuwa bora zaidi ili kuwa msaada kwa Taifa Stars katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.

Katika hatua nyingine, Msuva alisema anatamani kuifikia na kuvuka rekodi ya mfungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars ambayo kwa sasa inashikiliwa na Mrisho Ngassa aliyepachika mabao 25.

Kwa sasa, Msuva amefumania nyavu mara 22 sawa na Mbwana Samatta na mwenyewe anaamini kwamba anayo nafasi ya kutosha ya kumfikia Ngassa na kuandika rekodi mpya.

"Ninapofunga, kipaumbele cha kwanza ni timu kwamba inatakiwa ifanye vizuri na baada ya hapo mengine ndio yanafuata. Ninamheshimu sana Mrisho Ngassa kwani yeye ni kaka yangu ni 'Role Model' (mfano wa kuigwa) kwangu na nampongeza kwa rekodi aliyoiweka kwani sio rahisi.

"Kiukweli nami natamani kuifikia, kuivunja na ikiwezekana niweke rekodi yangu na naamini hilo linawezekana kwani nafasi ya kuitumikia Taifa Stars ninayo ya kutosha na naamini bado uwezo wa kufunga mabao upo hivyo natamani kuweka hiyo rekodi," alisema Msuva.