Mpishi afichua siri ulaji wa Ronaldo
Muktasari:
- Mpishi wa zamani wa Cristiano Ronaldo, amefichua kuwa mchezaji huyo alipiga marufuku matumizi ya maziwa katika lishe yake, ikiwa ni moja ya siri zinazomuweka katika kiwango cha juu.
Nyota wa soka wa Ureno, Cristiano Ronaldo (41), anaendelea kushangaza dunia kwa uimara wake na mwili uliojengeka vyema, huku akitarajia kuiongoza timu yake ya taifa katika mashindano ya Kombe la Dunia la mwaka huu.
Siri ya mafanikio yake imewekwa wazi na aliyekuwa mpishi wake binafsi, Giorgio Barone, ambaye amesema mchezaji huyo aliacha kabisa kunywa maziwa kwa sababu anaamini si sehemu ya lishe ya asili ya binadamu.
Akizungumza na vyombo vya habari, Barone amesema:
“Binadamu ndio viumbe pekee wanaokunywa maziwa ya viumbe wengine. Hili halipo kiasili. Baada ya utoto, si jambo la kawaida kuendelea kunywa maziwa.”
Nyota wa Al Nassr na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo. Picha na Mtandao
Ratiba kali ya mazoezi na lishe
Mbali na kuacha kunywa maziwa, Ronaldo anajulikana kwa nidhamu kali ya mazoezi, akifanya hadi saa nne kwa siku na kula milo midogo sita yenye protini nyingi.
Lishe yake inajumuisha Parachichi, mayai na kahawa bila sukari kwa kifungua kinywa, Samaki, kuku na mboga kwa chakula cha mchana anakula chakula chepesi jioni kama samaki au nyama ya kuchoma, nafaka zisizokobolewa na matunda.
Kwa mujibu wa mpishi huyo, Ronaldo huepuka kabisa vyakula vya unga kama mkate na pasta, huku akipata wanga kupitia mboga mboga.
Mshambuliaji wa Al Nassr na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo akiwa katika ulaji wake wa lishe. Picha na Mtandao
Mafuta kidogo, protini nyingi
Vipimo vya hivi karibuni vinaonesha Ronaldo ana kiwango cha mafuta mwilini cha asilimia saba pekee. Mbali na lishe, hutumia pia mbinu za kurejesha mwili kama sauna na kuoga maji ya barafu.
Mshambuliaji wa Al Nassr na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo akiwa na mchumba wake Georgina Rodríguez. Picha na Mtandao
Mtazamo dhidi ya vinywaji baridi
Ronaldo pia amekuwa mkosoaji wa vinywaji baridi. Katika tukio lililofanyika kwenye michuano ya Euro 2020, aliwahi kuondoa chupa ya Coca-Cola mbele yake na kuwahimiza watu kunywa maji badala yake.
Mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland. Picha na Mtandao
Utofauti na Erling Haaland
Tofauti na Ronaldo, mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland, anaripotiwa kutumia maziwa mabichi pamoja na nyama na viungo vya ndani kama ini na moyo.
Hata hivyo, Barone amesema anakubaliana na ulaji wa viungo hivyo:
“Ini, moyo na ubongo ni vyakula vyenye virutubisho vingi. Hata Cristiano alipenda ini.”