Haaland aibuka mfungaji Bora kufuzu Kombe la Dunia
Mshambuliaji wa Norway, Erling Haaland, akiwa ameshika tuzo baada ya kuibuka mfungaji bora wa Ulaya katika kampeni ya kufuzu Kombe la Dunia 2026. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Idadi ya mabao 16 aliyofunga Haaland imefikia rekodi iliyowekwa na Robert Lewandowski wakati wa kufuzu michuano ya mwaka 2018.
Mshambuliaji wa Norway, Erling Haaland, amemaliza hatua ya makundi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 barani Ulaya akiwa kinara wa mabao, baada ya kufunga jumla ya mabao 16 na kuisaidia nchi yake kufuzu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998.
Haaland, anayekipiga katika klabu ya Manchester City, alionesha kiwango cha juu katika mechi zote nane za kundi hilo. Miongoni mwa mafanikio yake makubwa ni kufunga mabao matano katika ushindi wa mabao 11-1 dhidi ya Moldova, pamoja na kufunga mabao matatu katika mchezo dhidi ya Israel.
Nyota huyo amemaliza mechi hizo akiwa mbele kwa tofauti ya mabao nane dhidi ya washindani wake wa karibu ambao ni nahodha wa England, Harry Kane, mshambuliaji wa Uholanzi, Memphis Depay, pamoja na Marko Arnautović wa Austria, wote wakiwa na mabao nane kila mmoja.
Idadi ya mabao 16 aliyofunga Haaland pia imefikia rekodi ya mchezaji wa Ulaya aliyewahi kufunga mabao mengi zaidi katika kampeni ya kufuzu Kombe la Dunia, rekodi iliyowekwa na Robert Lewandowski wakati wa kufuzu michuano ya mwaka 2018.
Wachezaji wengine waliofanya vizuri katika hatua hiyo ni Kevin De Bruyne, Andrej Kramarić, pamoja na nyota wa Hispania, Mikel Oyarzabal na Mikel Merino, wote wakiwa na mabao sita.
Wakati huo huo, gwiji wa soka wa Ureno, Cristiano Ronaldo, amemaliza kampeni hiyo akiwa na mabao matano, na kufikisha jumla ya mabao 41 katika historia ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia akiwa kinara.