Vinicius atupia mawili Etihad, Man City ikiumaliza mwendo Ulaya
Muktasari:
- City ilikuwa na kazi ngumu sana Ikijaribu kufuta pengo la mabao 3-0 kutoka mechi ya kwanza katika hatua ya 16 bora, na ingawa ilianza kwa kasi kubwa ya kushambulia, kutolewa kwa Silva dakika ya 20, kulizima kabisa matumaini ya kurejea kwa kishindo.
Manchester, England. Kadi nyekundu ya kipindi cha kwanza kwa nahodha, Bernardo Silva iligeuka kuwa pigo kubwa, huku mabao mawili ya Vinícius Júnior yakiiwezesha Real Madrid, kuiongezea mateso Manchester City katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwaondoa vijana hao wa Pep Guardiola kwa msimu wa tatu mfululizo.
City ilikuwa na kazi ngumu sana Ikijaribu kufuta pengo la mabao 3-0 kutoka mechi ya kwanza katika hatua ya 16 bora, na ingawa ilianza kwa kasi kubwa ya kushambulia, kutolewa kwa Silva dakika ya 20, kulizima kabisa matumaini ya kurejea kwa kishindo.
Baadhi ya wachezaji wa Real Madrid wakati wakishangilia baada ya kufanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
Mreno huyo alikuwa amesimama kwenye mstari wa goli alipouzuia mpira wa shuti la Vinícius kwa mkono, na baada ya ukaguzi wa muda mrefu wa VAR pamoja na mwamuzi Clément Turpin kupitia tukio hilo, alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja huku penalti ikitolewa kwa wageni.
Vinícius alikuwa amekosa penalti wiki iliyopita dhidi ya Gianluigi Donnarumma, lakini safari hii hakufanya makosa, akimtuma kipa huyo wa Italia upande tofauti na kuzima shamrashamra za mashabiki wa Etihad dakika ya 22.
Real Madrid ingeweza kumaliza kabisa mchezo mapema dakika ya kwanza pale shujaa wa hat-trick wa Bernabeu, Federico Valverde alipobaki uso kwa uso na kipa, lakini alishindwa kuinua mpira na ukaishia mikononi mwa Donnarumma.
Mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Jr, wakati akifunga bao la pili. Picha na Mtandao
City ilipata nafasi za kujibu lakini ilishindwa kumpita kipa mrefu, Thibaut Courtois. Rayan Cherki alipiga mpira uliokwenda moja kwa moja kwa kipa, huku juhudi ya Rodri ikizuiwa juu ya lango na Courtois, na pia shuti la kwanza la Erling Haaland likiokolewa kwa ustadi mkubwa na kipa huyo wa Ubelgiji.
Haaland hatimaye alifunga kuelekea dakika za mwisho za kipindi cha kwanza na kuipa City matumaini madogo, lakini hawakuweza kufanya comeback ya kihistoria kipindi cha pili, huku Vinícius akiongeza bao la pili katika dakika za majeruhi 90+3.
City imeondoshwa katika michuano hiyo hatua ya 16 bora kwa jumla ya mabao 5-1 na kumfanya Guardiola kupoteza kombe la kwanza kati ya manne anayoshindania msimu huu ambayo sasa yamebaki; Kombe la FA (City ipo robo fainali itacheza dhidi ya Liverpool), Premier (ipo nafasi ya pili ikiachwa pointi tisa na vinara Arsenal) na Kombe la Carabao ambalo Jumapili hii Machi 22, 2026 itacheza fainali dhidi ya Arsenal.