Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpenja: Dabi ya leo moto balaa

KUNA ambao wanamuita Mwamba wa Umalila. Lakini wengine wanamtambua kwa jina maarufu la Sauti ya Radi. Ila ukitaka jina lake la kiserikali ni Baraka Harrison Mpenja.

Huyu ni mtangazaji nguli wa soka wa kituo cha Azam Tv ambaye siku kama ya leo ya Dabi sauti yake hutamba sana masikioni mwa mashabiki wa soka kutokana na mbwembwe na umahiri wake wa kucheza na maneno.

Mwanaspoti limefanya nae mahojiano maalum kuhusiana na mechi hiyo ya Simba na Yanga kufafanua mambo kadhaa;

Mpenja ambaye Mwanaspoti linajua atatangaza mechi hiyo, anasema; “Mashabiki wa Yanga wanaonekana kuumia kutokana na kuambiwa wachezaji na timu yao ni wa hapahapa nyumbani si kwenda kucheza mashindano ya kimataifa na ubingwa wao mkubwa ni kuifunga Simba.”

“Wakati mashabiki wa Simba, wachezaji, benchi la ufundi na viongozi hawafurahishwi kabisa kufungwa na Yanga na huko walipo wanaumia kuliko kawaida maumivu ya kawaida,”

“Itakuwa mechi yenye mvuto na ngumu kutokana na mazingira hayo mawili ya Simba iliyokwenda makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga iliyoshindwa kutinga hatua hiyo kwa muda mrefu.

“Ugumu mwingine ninaouona Yanga itataka kupata ushindi ili kufuta majonzi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Simba yenyewe inataka kushinda ili kuendeleza moto wa matokeo mazuri.”

“Nilianza kutangaza mechi za Simba na Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2017, hakuna mchezo wowote uliyowahi kuwa wa kawaida na kuzoeleka kila inapokutana miamba hiyo.

“Binafsi kabla ya kuweka neno la kwanza kwenye matangazo ya mechi huwa ninaperuzi kwanza. Kama mimi nakuwa kwenye presha kama hiyo inakuaje wachezaji, makocha, viongozi na hata mashabiki wenyewe halijawahi kuzoeleka pambano hilo la Simba na Yanga mara zote linakuwa jipya.

“Huwa najipanga kwenye kila idara na najikumbusha vitu vingi kabla kuhakikisha kila atakayekuwa anafuatilia mechi hii kupitia runinga ya Azam na mitandao ya kijamii atakuwa anapata raha kama ambavyo anasoma kwenye Mwanaspoti.”


PHIRI NA MAYELE

“Kuna utamu mwingine ndani yake upande wa Simba kuna Moses Phiri ambaye mashabiki wa upande wake wanataka kumuona akishangilia kwa kupiga saluti wakati kule Yanga kuna Fiston Mayele na mashabiki wa upande wake wanataka kutetema nao pamoja.

“Mayele mwenye mabao matatu yupo nyuma dhidi ya Phiri mwenye manne ila upande wa Yanga itapambana kadri ambavyo itawezekana ili Mkongomani huyo kuweka kambani na kutetema pamoja kama ilivyokuwa kwenye mechi iliyopita (Ngao ya Jamii).

“Phiri kwenye mechi iliyopita dhidi ya Yanga hakuwepo uwanjani, hakupewa nafasi ya kucheza. Naona pia mabeki wa Simba, Joash Onyango, Henock Inonga watakuwa na kazi ya kuhakikisha Mayele anashindwa kuonyesha makali yake kama ilivyo kwa Dickson Job, Yannick Bangala kwa Phiri.”


HAPA SASA

“Ushindani utakuwa mkubwa katikati mwa kiwanja Simba huenda ikaanza na viungo watatu kutokana na ubora wao wa hivi karibuni, Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute na mtaalamu Clatous Chama.

“Hivi karibuni Mzamiru amekuwa na ubora wa kuzuia na kuanzisha mashambulizi,ukiunganisha na ubora wa Sadio juu yao akiwa Chama kutakuwa na ushindani mkubwa dhidi ya wale wa Yanga, Feisal Salum, Khalid Aucho na Bangala kwani nao wamekuwa nguzo imara kwenye kikosi hicho.

“Kama viungo wa Simba au Yanga wale ambao watakuwa kwenye kiwango bora kuzuia wenzao kushindwa kuonyesha makali yao naamini timu hiyo ndio inakwenda kupata matokeo mazuri dhidi ya mkubwa mwenzake.”


MAYELE NA INONGA

“Ukiachana na ushindani kwenye maeneo mengine yote utamu utakuwa ndani ya mchezo huu pale uwanjani hata kwa mashabiki wataokuwa wanafuatilia mechi ni Mayele dhidi ya Inonga.

“Tangu msimu uliopita Mayele amekutana na Inonga kwenye michezo miwili ya Ligi na yote hajamfunga ila msimu huu alifunga kwenye mechi ya Ngao ya Jamii mabao mawili.

“Mayele atataka kuweka rekodi nyingine ya kufunga bao Inonga akiwepo uwanjani kwenye mchezo wa ligi na Inonga atataka kumzuia Mayele asifunge kwa mara nyingine mbele yake,patamu sana hapa.”


UBORA WA CHAMA

“Ukiachana na mechi Simba iliyoshinda mabao 4-1, dhidi ya Yanga kiungo Clatous Chama hakuwahi kuonyesha kiwango bora kwenye mechi hiyo kubwa.

“Chama amekuwa mswahili sasa hivi anafahamu kila ambacho kinaendelea kwenye mitandao ya kijamii si kama haoni kama kuna watu wanaombeza kuwa makali yake anaonyesha kwenye michezo mingine anaona na naamini amepanga kulifuta hilo.”

“Ili Phiri na washambuliaji wengine washindwe kufunga mabao wachezaji wa Yanga wanatakiwa kuwa na mpango maalumu wa kuhakikisha Chama haonyeshi ubora wake.”

“Kama wachezaji wa Yanga watashindwa kumzuia Chama na akafanikiwa kucheza kwenye kiwango bora watakwenda kupata madhara mapema na wakapoteza mchezo huo kutokana na ubora wa Mzambia huyo. Jamaa hanaga masihara kazini, amekuwa muhimili mkubwa wa kufanya maamuzi katika mechi zote muhimu za Simba.”


SIMBA ITAINGIA KWA UOGA

“Rekodi zinainyima furaha Simba na huenda wakaingia kwa uoga kwenye mechi hii kutokana na kushindwa kupata matokeo bora dhidi ya Yanga kwa michezo ya hivi karibuni.

“Imekuwa kama kasumba kwa timu hizi mbili kwa mfano misimu minne Simba iliyokuwa kwenye ubora wake na kuchukua taji la ligi ilikuwa inapata wakati mgumu kucheza dhidi ya Yanga na hata matokeo mazuri ilikuwa shida kuyapata.

“Kwenye misimu minne Simba kwenye ubora wake ilipoteza dhidi ya Yanga wakifungwa kwenye mechi mbili tofauti na Benard Morrison, Zawadi Mauya huku michezo mingine ikiisha kwa sare na mingine Mnyama alikuwa mazingira magumu dakika za mwisho,” anasema Mpenja na kuongeza;

“Kabla ya misimu hiyo minne kufika Yanga ilikuwa kwenye ubora ila ilikuwa na wakati mgumu kushinda dhidi ya Simba wakati huo Shiza Kichuya alikuwa shujaa kutokana na mabao yake kwenye michezo mitatu mfululizo.”

“Kwahiyo Simba itaingia kwa uoga mkubwa hata kama ikitangulia kupata bao itakuwa haina uhakika wa kumaliza mechi kwa ushindi tofauti na Yanga ambavyo itaingia na hali ya kujiamini kutokana na kupata matokeo mazuri mfululizo dhidi ya Yanga hivi karibuni.”