Moto wa Europa, Conference League kuwaka leo

Muktasari:
- Manchester United itakuwa ugenini kwenye michuano ya Europa League wakati Chelsea nayo itakuwa ugenini katika michuano ya Europa Conference League.
Usiku wa leo macho na masikio ya mashabiki wa kandanda yatakuwa kwenye viwanja mbalimbali barani Ulaya, ambako hatua ya robo fainali ya mashindano ya UEFA Europa League na UEFA Conference League yataendelea.

Miongoni mwa mechi itakayofuatiliwa na wengi ni ile kati ya Lyon dhidi ya Manchester United, pambano la kukata na shoka litakalochezwa kwenye Uwanja wa Groupama huko Ufaransa. Manchester United, chini ya kocha Ruben Amorim, watahitaji kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele dhidi ya Lyon ambayo imekuwa ikipata matokeo mazuri inapokuwa nyumbani.

Katika mchezo mwingine wa kuvutia, Tottenham Hotspur watawakaribisha Eintracht Frankfurt jijini London. Frankfurt wana historia ya kufanya maajabu, wakikumbukwa kwa kutwaa taji hili mwaka 2022.

Michezo mingine itakayochezwa ni pamoja na ule wa Bodø/Glimt dhidi ya Lazio kwenye Uwanja wa Aspmyra, Norway wakati Rangers itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Ibrox kukabiliana na Athletic Club.
Kwa upande wa UEFA Conference League, macho ya wengi yatakuwa kwenye mchezo kati ya Legia Warszawa dhidi ya Chelsea. The Blues, licha ya kuwa katika mashindano haya kwa mara ya kwanza, wanatazamiwa kutumia kikosi chao kipana chenye vipaji ili kuondoka Poland na matokeo chanya. Hii ni nafasi kwa Chelsea kuonyesha dhamira yao ya kutwaa taji lingine la Ulaya, licha ya msimu wa Premier League kuwa mbaya kwao.

Real Betis itakuwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Villamarin dhidi ya Jagiellonia ya Poland wakati Fiorentina ya Italia itapambana na Celje, huku ikitafuta kurudia mafanikio yao ya kufika fainali ya mwaka jana.
Pia kutakuwa na mechi kati ya Djurgården dhidi ya Rapid Vienna, ambayo itachezwa 3Arena ambao ni uwanja wa nyumbani wa Djurgården.