Morocco yatinga 32 bora Kombe la Dunia
Muktasari:
- Matokeo hayo yanaifanya Morocco kumaliza kundi C na pointi saba sawa na Brazil inayoongoza kwa tofautiana ya mabao, huku Scotland ikimaliza ya tatu na pointi tatu wakati Haiti ikiburuza mkia bila pointi.
Atlanta, Marekani. Ushindi wa mabao 4-2 ilioupata timu ya taifa ya Morocco dhidi ya Haiti leo, umekifanya kikosi hicho kufuzu hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia.
Katika mechi hiyo ya kundi C iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mercedes-Benz, Atlanta, Marekani, ilianza kwa Morocco kushtukizwa bao la mapema dakika ya 10, baada ya kipa wa kikosi hicho, Yassine Bounou 'Bono' kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa mpira na kuipa Haiti uongozi.
Bao hilo liliiamsha Morocco na dakika ya 39, Achraf Hakimi akakisawazishia kikosi hicho, kisha kushtukizwa tena kwa kufungwa bao la pili na Wilson Isidor dakika ya 43, akimalizia pasi ya beki wa kati, Jean-Kevin Duverne.
Bao hilo la Isidor likamfanya awe mchezaji wa kwanza wa taifa la Haiti kufunga katika Kombe la Dunia baada ya miaka 52, tangu mara ya mwisho aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Emmanuel Sanon kufunga katika fainali zilizofanyika Ujerumani Magharibi mwaka 1974.
Wakati Haiti ikitegemea ingemaliza kipindi cha kwanza ikiongoza, Ismael Saibari akaifungia Morocco bao la pili na la kusawazisha dakika ya 45, baada ya kumalizia vyema kazi nzuri ya Hakimi na timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya mabao 2-2.
Baadhi ya wachezaji wa Morocco wakishangilia moja ya bao katika ushindi wa 4-2 ilioupata dhidi ya Haiti katika Fainali za Kombe la Dunia 2026. Picha na Mtandao
Kipindi cha pili kilianza kwa Morocco kuendelea kulishambulia lango la Haiti, ambapo dakika ya 78, Soufiane Rahimi akaifungia bao la tatu akimalizia pasi ya Chadi Riad kisha Gessime Yassine akafunga la nne dakika ya 89, akimalizia pasi ya Soufiane Rahimi.
Matokeo hayo yanaifanya Morocco kumaliza kundi C na pointi saba sawa na Brazil inayoongoza pia lakini zikitofautiana kwa mabao, huku Scotland ikimaliza ya tatu na pointi tatu wakati Haiti ikiburuza mkia bila pointi ambapo safari yao ya Kombe la Dunia 2026 imefikia tamati.
Morocco inashiriki Kombe la Dunia la FIFA mara saba hadi sasa, kuanzia mwaka 1970, 1986, 1994, 1998, 2018, 2022 na 2026, huku mafanikio makubwa ni ya 2022, ilipoweka rekodi nchini Qatar ya kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufika hatua ya nusu fainali.
Katika Kombe la Dunia mwaka 2022 lililofanyika Qatar, Morocco ilifika nusu fainali ikiwa ni timu ya kwanza Afrika na nchi ya kwanza pia ya Kiarabu kufika hatua hiyo, ambapo kwa mwaka huo ilimaliza nafasi ya nne na kuandika historia hiyo mpya.
Mafaniko mengine ya Morocco katika Kombe la Dunia ni mwaka 1986 nchini Mexico kama ilivyo sasa, ambapo kikosi hicho kiliweka rekodi ya timu ya kwanza kutoka Afrika kumaliza kileleni mwa kundi lake na kufika hadi hatua ya 16 bora.
Katika fainali hizo, Morocco ilimaliza kileleni mwa kundi F na pointi nne sawa na England iliyomaliza ya pili, wakati Poland ikishika nafasi ya tatu na pointi tatu, huku Ureno ikiburuza mkiani baada ya kumaliza na pointi mbili.
Morocco ilimaliza ikiwa kileleni mwa kundi ikiwa ni timu ya kwanza kutoka Afrika kuongoza kundi katika Kombe la Dunia, japo ilitolewa hatua ya 16, bora kwa kuchapwa bao 1-0, dhidi ya Ujerumani Magharibi lililofungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Lothar Matthaus dakika ya 88, Juni 17, 1986.
Kwa upande wa Haiti maarufu 'Les Grenadiers' imefuzu Kombe la Dunia 2026, kwa mara ya kwanza katika historia yake baada ya miaka 52 kupita, tangu iliposhiriki mara ya mwisho mwaka 1974 kwenye fainali zilizofanyika Ujerumani Magharibi.
Haiti ilijihakikishia nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia baada ya kuifunga Nicaragua mabao 2-0, katika mechi ya mwisho ya kufuzu kutoka ukanda wa CONCACAF na kuongoza kundi C ikikusanya pointi 11, ikishinda mechi tatu, sare mbili na kupoteza moja.
Katika kundi hilo la C, Haiti ilifuzu fainali za Kombe la Dunia mbele ya Honduras, Costa Rica na Nicaragua, ikiwa ni hatua muhimu ya kihistoria, japo ugeni wake na ugumu wa kundi lake umechangia kwa kiasi kikubwa kikosi hicho kutolewa mapema.