Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mmiliki Alliance alivyoacha alama

Muktasari:

  • Bwire ambaye alikuwa mdau mkubwa wa michezo nchini akiwa ni Mkurugenzi wa Kituo cha Kukuza na Kulea vipaji cha Alliance aliwahi pia kuwa mwanasiasa akiwa Diwani wa Kata ya Mahina Jimbo la Nyamagana na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Mmiliki  wa timu za Alliance FC na Alliance Girls za Mwanza, James Bwire amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumapili (Januari 26, 2025) wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

Bwire ni mmoja kati ya watu ambao wamefanikiwa kuweka alama ya kukumbukwa kwenye michezo Tanzania kutokana na kituo chake kuzalisha wachezaji wengi mahiri kwenye soka upande wa wanawake na wanaume hapa nchini.

Bwire ambaye alikuwa mdau mkubwa wa michezo nchini akiwa ni Mkurugenzi wa Kituo cha Kukuza na Kulea vipaji cha Alliance aliwahi pia kuwa mwanasiasa akiwa Diwani wa Kata ya Mahina Jimbo la Nyamagana na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mashindano kituo cha Alliance, Stephano Nyaitati,  ni kwamba Bwire amefikwa na umauti baada ya kushambuliwa na kiharusi saa 3 usiku jana Jumamosi akiwa nyumbani kwake na kupelekwa Hospitali ya Bugando ambapo alifariki saa 4 usiku baada ya kupokelewa kitengo cha dharura.

Amesema Bwire alikuwa na changamoto ya kuumwa kwa muda mrefu kutokana na matatizo ya presha ambapo hivi karibuni alipelekwa India kupata matibabu na afya yake kuimarika, lakini jana hali ilibadilika ghafla na kusababisha kifo chake.

"Ni kweli mkurugenzi wetu ambaye ndiyo muasisi wa Shule na Kituo cha Michezo cha Alliance amefariki dunia. Alikuwa ni mgonjwa kwa muda kidogo alipata changamoto kidogo utakumbuka kuna mwaka hapo nyuma alishakwenda India akapata matibabu alikuwa anaendelea vizuri," amesema Nyaitati na kuongeza;

"Alikuwa na changamoto ya presha lakini hali yake ilibadilika jana (jumamosi) majira ya saa tatu usiku akiwa nyumbani kwake baada ya kushikwa na Kiharusi, tukafanya utaratibu wa kumpeleka hospitalini, baada ya kufika hospitali ya Bugando ikabainika ameshafariki."

Nyaitati alisema uongozi wa kituo cha Alliance umekubaliana kufanya mazishi ya mwasisi wao huyo Jumapili Februari 2, mwaka huu, huku akiwakaribisha ndugu, jamaa na marafiki kushirikiana kuhakikisha mpendwa wao huyo anastiriwa vizuri.

"Kama unavyojua mzee Bwire ni mtu wa watu amefanya kazi Serikalini na kulitumikia Jiji la Mwanza amekitumikia pia chama (CCM) na kwenye mpira amefanya mambo makubwa, kwahiyo sisi kama familia ya Alliance tumekubaliana kwamba maziko yake tutayafanya siku ya Jumapili wiki ijayo (Februari 2)," amesema Nyaitati na kuongeza;

"Kwa sasahivi kwa watu ambao ni ndugu, jamaa na marafiki wafike nyumbani kwa ajili ya kuomboleza na kuendelea kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kwamba tunamsitiri vizuri."

Akizungumzia dakika za mwisho za Bwire, Nyaitati amesema amefariki akiwa anazungumzia michezo.

"Alipenda sana michezo hasa soka, hadi jana (Jumamosi) mauti inamkuta alikuwa akisisitiza kufanya kazi kwa bidii, alitamani kuona mafanikio makubwa kwa vijana wenye vipaji.

"Bosi (Bwire) alikuwa ni mtu asiyekubali kushindwa, njia ambazo wengine waliziona ni ngumu, yeye alitaka kupita na aliweza," alisema.

Alliance FC ilianzishwa mwaka 2012 na kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa mwaka 2018/2019 na baadaye kushuka daraja ambapo kwa sasa inashiriki First League. Timu hiyo imetoa wachezaji mbalimbali akiwemo Israel Mwenda ambaye kwa sasa anaichezea Yanga, Zabona Mayombya, Juma Nyangi, Hans Masoud na Balama Mapinduzi (Kipenseli).

Alliance Girls ilianzishwa mwaka 2016 na inashiriki Ligi Kuu ya Wanawake tangu mwaka 2017  na hadi sasa ikiwa imewaibua nyota mbalimbali wanaotamba ndani na nje ya nchi wakiwemo, Aisha Masaka (Brighton &Holves Albion) huyu ndiye mchezaji wa soka kutoka Tanzania ambaye anacheza kwenye ligi kubwa zaidi akitokea kwenye kituo hicho, Aisha Mnunka (Simba Queens), Enekia Kasonga (Uturuki), Winfrida Charles (Fountain Gate) na Aliya Fikiri (JKT Queens).

Alliance ilifanikiwa kudumu kwenye ligi kwa misimu miwili tu, lakini heshima kubwa ambayo iliibakiza kwenye ligi hiyo ni kitendo cha timu hiyo kutumia wachezaji wengi vijana ambao walifanikiwa kuonyesha kiwango cha juu sana kwenye soka.