Prime
Mkude aikataa jezi ya feitoto

Muktasari:
- Mbali na Kibabage sura nyingine mpya ni beki wa kati Gift Fred ambaye tayari ameshapewa mkataba wa miaka miwili Gift licha ya kwamba hatajwi sana lakini kwa mujibu wa wachambuzi wa Uganda alitamba sana msimu uliopita akiwa na SC Villa.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga wamerudi kazini jana. Kocha wao mpya Miguel Gamondi atakutana na mastaa wake tayari kuseti mitambo tayari kwa kuliamsha dude.
Hawaendi Ulaya, watakuwa kwenye kambi yao ya kisasa pale Avic Town, Kigamboni Jijini Dar es Salaam lakini tambua kwamba kutakuwa na sura mpya kibao.
Rais wa Yanga, Hersi Said tayari juzi alitangaza kwamba sasa ni kitu baada ya kitu; "Naona watu wanaposti sajili zao na kutamba mitandaoni wanayanga wasitishike kwani wanayoyafanya wao walishayafanya na watayafanya kwasabu wamesajili na wana imani na usajili walioufanya;
"Kwa namna tulivyopata mafanikio Yanga kwenye mashindano ya ndani na kimataifa msimu huu tunahitaji jitihada zaidi ilikuvuka hatua hiyo na kufikia huko tunahitaji uwekezaji kwenye usajili,"alisema.
Kocha Gamondi rasmi ataanza kukinoa kikosi hicho Yanga ikianza maisha mapya chini yake ambapo tayari kuna mastaa watatu wapya watakuwa ndani ya mazoezi hayo na ametangaza kwamba;
"Natarajia kuwa na timu nzuri na bora na napenda kuwa na wachezaji ambao ni waumini wa kucheza mpira natamani kuona timu yangu inacheza mpira."
Tayari Yanga ilishamtambulisha beki na winga wa kushoto Nickson Kibabage ambaye walimnunua akitokea Singida Fountain Gate katika dirisha hili la usajili na jamaa atakuwa kazini huku Simon Msuva akiwahakikishia mashabiki wa Yanga kwamba mchezaji huyo mwenye kasi kama yeye atawasapraizi.
Mbali na Kibabage sura nyingine mpya ni beki wa kati Gift Fred ambaye tayari ameshapewa mkataba wa miaka miwili Gift licha ya kwamba hatajwi sana lakini kwa mujibu wa wachambuzi wa Uganda alitamba sana msimu uliopita akiwa na SC Villa.
Timu hiyo ya Uganda ambayo ilimpa cheo cha unahodha ilimpandisha thamani na alikuwa akiwaniwa na klabu kadhaa ikiwemo KCCA na Vipers kabla ya Yanga kumnyakua juu kwa juu. Villa iliwahi kuwauzia Yanga vyuma vilivyowika akiwemo Hamis Kiiza.
Klabu ya Yanga imetangaza rasmi kumsajili kiungo mkabaji mzawa Jonas Mkude kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Simba alikoishi kwa miaka 13 na wekundu hao. Simba wametangaza watamuaga kwa gwaride kwenye Uwanja wa Mkapa siku ya Simba Day lakini amewang'ong'a.
Hadi sasa wameshatambulishwa Gift na Mkude wakati wowote wanaweza kumtambulisha winga Mkongomani Maxi Nzengeli ambaye naye ameshamaliza usajili wake akitokea Union Maniema ambayo ni washikaji wa Yanga.
Taarifa kutoka kwa wasimamizi wa Mkude Mwanaspoti limepenyezewa kuwa kiungo huyo amegomea kukabidhiwa jezi namba 6 iliyoachwa na kiungo Feisal Salum 'Fei Toto'ambaye aliuzwa kwa utata Azam FC na kutambulishwa na jezi namba 20 aliyokuwa akiitumia akiwa Simba
Mwanaspoti pia linajua kwamba Yanga ina nafasi ndogo ya kumpata staa wa Asec Memosas, Mohamed Zoungrana ambaye ndiye waliyempanga kumpa jezi namba 6
Inaelezwa Mkude amegomea jezi hiyo akidai hataki kuanza na presha ndani ya klabu hiyo aliyowahi kuichezea akiwa mdogo kwa kile alichoeleza tayari Kuna mashabiki wengi wanasubiri kujua mchezaji gani mkubwa atakabidhiwa namba hiyo.
Mbali na wachezaji pia kitendawili kingine kitakachosubiriwa kwenye mazoezi hayo ni wasaidizi wa Gamondi ambapo juzi usiku walimtambulisha Mousa Ndao raia wa Senegal kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo akisaidiana na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kuhakikisha wanatengeneza timu imara msimu wa ujao, kwani Cedrick Kaze naye hatakuwa Jangwani msimu ujao
Taarifa ambazo Mwanaspoti imepenyezewa ni kwamba Gamondi amepewa nafasi ya kuwaleta watu wake katika nafasi zote zilizosalia wakiwemo kocha wa makipa, kocha wa mazoezi ya viungo.