Messi wa Uturuki avunja rekodi ya Ronaldo Euro

Muktasari:

  • Guler, akiwa na umri wa miaka 19 na siku 114, alifunga bao matata kabisa wakati Uturuki kushinda 3-1 dhidi ya Georgia katika mchezo wao wa kwanza wa makundi katika fainali za Euro 2024.

Dortmund. Kinda wa Uturuki Arda Guler amevunja rekodi ya Cristiano Ronaldo ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao kwenye mechi yake ya kwanza kwenye mikikimikiki ya ubingwa wa Ulaya.

Guler, akiwa na umri wa miaka 19 na siku 114, alifunga bao matata wakati Uturuki ikishinda 3-1 dhidi ya Georgia katika mchezo wao wa kwanza wa makundi katika fainali za Euro 2024.

Miongo miwili iliyopita, Ronaldo aliweka rekodi hiyo ya kufunga bao kwenye michuano ya Ulaya akiwa na umri mdogo, wakati alipoifungia Ureno bao la kujifariji kwenye mechi ya kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Ugiriki.

Ronaldo wakati anafunga bao hilo, alikuwa mkubwa kumzidi Guler kwa siku 14. Guler, anayekipiga kwenye kikosi cha Real Madrid anafahamika kama 'Messi wa Uturuki'. Alifunga bao lake kwa shuti la mita 25 kuifanya Uturuki kuongoza 2-1 baada ya Georgia kusawazisha kwenye kipindi cha kwanza katika mchezo huo uliofanyika Dortmund.


Guler hakuchezeshwa sana huko Real Madrid msimu uliopita, lakini alifunga mabao sita katika mechi 12 alizopewa nafasi tangu alipotua kwenye timu hiyo akitokea Fenerbahce kwa ada ya Pauni 25 milioni.

Ronaldo, ambaye alitimiza umri wa miaka 39, Februari mwaka huu, hakujali kwa Guler kuvunja rekodi yake hiyo baada ya yeye kuandika nyingine kwa kuwa mchezaji wa kwanza kucheza kwenye fainali sita tofauti za Euro.

Ronaldo alisema: "Wala sifahamu ni miaka mingapi nimebakiza kwenye soka. Imekuwa zawadi kubwa kwangu kucheza kila mwaka baada ya kutimiza miaka 35. Sasa nina miaka 39 na ninachofanya ni kufurahia tu mpira."