Sababu za Ukraine kutupwa nje na ratiba nzima ya 16 Bora

Munich, Ujerumani. Moja ya vitu vya kufurahisha au kushangaza katika michuano ya Euro 2024 ni Kundi E, baada ya kila timu kumaliza na pointi nne, hata hivyo mmoja hajafuzu.

Romania imemaliza kileleni mwa kundi hilo akifuatiwa na Ubelgiji ambazo zimefuzu hatua ya 16 bora huku Slovenia ikienda kama ‘best looser’ kisha Ukraine ikiaga mashindano hayo.

Kundi hilo kila timu imemaliza na pointi nne imeshinda mechi moja, imepoteza moja na kutoka sare moja, katika michezo yote mitatu zilizocheza huku mabao yakiamua nani asonge mbele na yupi arudi nyumbani.

Romania imemaliza kileleni na kufuzu hatua ya 16 ikifuatiwa na Ubelgiji zote zikiwa na faida ya bao moja huku Slovenia ikimaliza nafasi ya tatu ikiwa haina bao ambapo kilichoirudisha nyumbani Ukraine licha ya kuwa na pointi sawa na wenzake ni kudaiwa deni la mabao mawili, lakini kanuni kuwa kila kundi mwisho wa kutoa timu ni tatu hata kama zitakuwa na pointi zaidi ya nyingine kwenye makundi mengine.

Kwa ujumla timu ambazo zimefanikiwa kufuzu 16 Bora kwenye michuano ya msimu huu ni kama ifuatavyo kulingana na makundi yao.

Vinara wa makundi: Austria, England, Ujerumani, Ureno, Romania na Hispania.

Waliofuzu washindi wa pili: Ubelgiji, Denmark, Ufaransa, Italia, Uswis na Uturuki.

Waliofuzu kama Best Loser nafasi ya tatu: Georgia, Uholanzi, Slovakia, Slovenia.

Ambazo zimeshindwa kufuzu: Albania, Croatia, Czech, Hungary, Poland, Scotland, Serbia na Ukraine.


Ratiba 16 Bora

Hatua ya 16 Bora inatarajiwa kuanza keshokutwa Jumamosi wakati ambapo Uswis itakuwa uwanjani kuvaana na Italia saa 12:00 jioni wakati mechi ya usiku itakuwa kati ya Ujerumani dhidi ya  Denmark.

Jumapili Juni 30
England vs Slovakia
Spain vs Georgia
Jumatatu Julai 1
Ufaransa vs Ubelgiji
Ureno vs Slovenia
Jumanne Julai 2
Romania vs Uholanzi
Austria vs Uturuki.