Kambi Simba sasa Julai Mosi

Taarifa mpya kutoka ndani ya Simba SC zinabainisha kwamba, wachezaji wao wote sambamba na benchi la ufundi wanapaswa kuwa kambini jijini Dar es Salaam kuanzia Julai Mosi mwaka huu kama ilivyo kwa Yanga na Azam.

Awali iliripotiwa kwamba Simba wangeanza kukutana leo Alhamisi kwa ajili ya maandalizi ya safari yao ya kwenda Misri ambayo ilipangwa kuwa Julai Mosi, lakini sasa mambo yamebadilika.

Simba sasa imepanga kuanzia Julai Mosi wachezaji na benchi zima la ufundi kuanza kuwasili kambini jijini Dar kuweka mambo sawa kujiandaa na kambi yao ya maandalizi ya msimu ujao 'pre season' inatarajiwa kuanza rasmi Julai 8 mwaka huu huko nchini Misri.

Baada ya kuanza kukutana Julai Mosi, zoezi litakalofanyika ni wachezaji wote kufanyiwa vipimo vya afya kuanzia wale wapya waliosajiliwa kipindi hiki na waliokuwepo msimu uliopita.

"Kambi yetu rasmi ya kujiandaa na msimu ujao inaanza Julai Mosi mwaka huu ambapo wachezaji na makocha wote wanatakiwa kufika kambini kwa ajili ya maandalizi ya safari," alisema mtoa taarifa na kuendelea.

"Baada ya kufika kila mmoja, litafanyika zoezi la upimaji afya kwa wachezaji wapya na wale wa zamani."

Mtoa taarifa huyo aliendelea kubainisha kwamba baada ya vipimo vya afya kumalizika, wachezaji watagawiwa vifaa vyao vya mazoezi.

"Kila mchezaji atakabidhiwa vifaa vyake vya mazoezi baada ya kumaliza kupima afya, kisha safari yetu itakuwa Julai 8 kuelekea Misri kuweka kambi yetu," alisema.

Simba imepanga kuweka kambi Misri kwa takribani wiki tatu kabla ya kurejea nchini kujiandaa na Tamasha la Simba Day sambamba na michezo ya Ngao ya Jamii itakayoanza Agosti 8 hadi 11 mwaka huu.

Katika mipango yao hiyo pia ishu ya kocha mpya ipo ndani yake kwani mpaka sasa haijamtambulisha mrithi wa Abdelhak Benchikha aliyeondoka Aprili mwaka huu siku chache baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Yanga.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amezungumzia kambi yao ya maandalizi ya msimu ujao akisema: "Tunatarajia kwenda Misri katika Mji wa Ismailia kuweka kambi ya maandalizi ya msimu ujao.

"Tumechagua kwenda Misri kwa sababu hali ya hewa ni rafiki kwetu lakini pia timu nyingi zinakwenda huko hasa katika Mji wa Ismailia kutokana na utulivu uliopo kulinganisha na Cairo kwenye hekaheka nyingi. Tunatarajia kuondoka wiki ya kwanza ya mwezi Julai."

Wakati Simba ikienda kuweka kambi nchini Misri, Azam ambao wataanza kukutana Julai Mosi katika viunga vya Chamazi yalipo maskani yao, mikakati ya pre season ni kwenda Morocco Julai 14, huku kuanzia Julai 4 hadi 13 wakitarajiwa kujificha visiwani Zanzibar.

Yanga wana mialiko mitatu, Afrika Kusini, Kenya na Urusi, hivyo nao wakiingia kambini Julai Mosi pale Avic Town maeneo ya Kigamboni ndiyo itafahamika wanakwenda wapi kati ya sehemu hizo.