UCHAMBUZI WA MALOTO: Wanataka Katiba ivunjwe ili watambuliwe na Rais

Muktasari:

  • Ujerumani, kuna ofisi inaitwa BfV, ipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo. Jukumu la BfV ni kulinda Katiba ya Ujerumani. Hufuatilia kila vuguvugu na kazi ambayo inakinzana na Katiba, halafu ofisi hiyo huchukua hatua stahiki.

Ujerumani, kuna ofisi inaitwa BfV, ipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo. Jukumu la BfV ni kulinda Katiba ya Ujerumani. Hufuatilia kila vuguvugu na kazi ambayo inakinzana na Katiba, halafu ofisi hiyo huchukua hatua stahiki.

Marekani, jukumu la kulinda Katiba halijawekwa kwenye ofisi moja. Mahakama Kuu ina wajibu, vivyo hivyo Rais. Inapotokea upande mmoja au kuna mahali Katiba haifuatwi, moja kwa moja bunge kuu (Congress), ndiyo huchukua dhima ya kuweka mzani wa kikatiba sawia.

Katiba lazima ipewe ulinzi. Nchi ambayo Katiba yake haiogopwi, inasutwa na kupigwa masingi hovyo mitaani, hukaribisha taifa lenye mifumo dhaifu. Hali hiyo ndiyo inainyemelea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakuna mwiko wa kuibagaza Katiba, hivyo yeyote anaweza kusema chochote.

Hivi karibuni, Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, ilipendekeza kuongeza muda wa muhula wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kutoka miaka mitano hadi saba.

Kauli hiyo ya nyongeza ya muhula wa urais wa Mwinyi, ilitolewa na Dk Mohamed Said Dimwa, Naibu Katibu Mkuu wa chama Cha Mapinduzi Zanzibar, wakati wa kufunga mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya Dimami, Kiembesamaki, Zanzibar. Tukio hilo, lililofanyika katika Ofisi za Wilaya, lilibainisha imani ya chama kwa uongozi wa Rais Mwinyi.

Dk Dimwa alifafanua kuhusu sababu za pendekezo hilo, akisisitiza kuwa mafanikio makubwa ya Rais Mwinyi katika muhula wake. Kwa mujibu wa Dk. Dimwa, Rais Mwinyi ameweza kutimiza na hata kuzidi matarajio ya ilani ya chama ya mwaka 2020-2025, kwa kufanikisha zaidi ya asilimia 100 ya malengo ndani ya miaka mitatu na miezi michache tangu aingie madarakani.

Kwa vipimo hivyo na kwa hoja yake, hakuna ambacho Rais Mwinyi anastahili, zaidi ya kuvunja Katiba na kumtanulia muhula wa uongozi, kutoka miaka mitano hadi saba. Ukimfuatilia vema Dimwa, hasemi hayo kwa masilahi ya nchi, bali ni kusudi la kujaribu kuingia kwenye kitabu kizuri cha Rais Mwinyi.

Hata hivyo, Rais Mwinyi, kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zanzibar, Charles Hillary, alisema kuwa yeye ni muumini wa Katiba na sheria, akabainisha kuwa maoni ya Dimwa hayana tija, na kwamba aliyoyasema siyo msimamo wake wala Chama cha Mapinduzi (CCM).

Ilishapita kauli ya Mshauri wa Rais Samia Suluhu Hassan, Sophia Mjema, aliyenukuliwa akisema “urais wa Samia ni mpaka mwaka 2035.” Kabla ya Rais Samia, alikuwepo Rais John Magufuli, ambaye kulikuwa na kelele nyingi za kumtaka asiondoke madarakani ndani ya muda wake wa kikatiba.

Mayowe kuhusu Magufuli kuongezewa muda yalianza mitaani kisha yakaingia ndani ya Bunge la Tanzania. Aliyekuwa Mbunge Nkasi Kaskazini, Ally Keissy, alianzisha mada, na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, akasema “tutamwongezea muda atake asitake.”

Swali ni je, mtu akitaka kuingia kwenye kitabu kizuri cha Rais, lazima aanze kuikosea heshima Katiba? Watu hawana namna nyingine ya kuzungumza yenye kuwafurahisha viongozi, zaidi kuielekea Katiba na kuzungumza matamshi ambayo si ya kikatiba?

Situmii lugha ya kujipendekeza, sababu siyo uungwana. Wala siiti uchawa, kwa maana haileti heshima kwenye jamii. Ninachotaka ni kualika tafakuri kwa kila mmoja. Je, watu hawana mbinu tofauti za kuwafanya viongozi wafurahie maneno yao, zaidi ya hizi sifa zenye kukosa heshima kwa Katiba?

Kelele za nyongeza ya mihula ya urais zimeshazoeleka Tanzania Bara. Yalipigwa mayowe mengi wakati wa Magufuli. Kuanzia hoja ya Juma Nkamia na chagizo la muhula kuongezwa kutoka miaka mitano hadi saba, hadi urais usio na kikomo bungeni, yote ni wakati wa Magufuli.

Lugha zilezile zinajirejea kwa Rais Samia. Zinavuka maji hadi visiwani, Rais Mwinyi, naye anaombewa nyongeza ya muhula. Wanaotoa matamshi wanaweza kujidanganya kuwa ni wapya, wakati hata enzi za Rais wa Kwanza, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere walikuwepo.

Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, katika kitabu chake kinachoitwa “My Life, My Purpose” – “Maisha Yangu, Kusudi Langu”, amesimulia kuwa Mwalimu Nyerere alilazimisha kung’atuka kwa sababu aligundua waliokuwa wanang’ang’ania asiachie madaraka, walifanya hivyo kwa kutazama masilahi yao.

Mkapa pia kupitia kitabu chake, alibainisha kwamba wakati wa urais wake, alipata wakati mgumu kumdhibiti Rais wa Tano wa Zanzibar, Salmin Amour Juma, aliyekuwa anataka kubadili Katiba ya Zanzibar na kuongeza muhula mwingine. Hata Salmini hakuwa yeye peke yake, nyuma yake kulikuwa na waliotazama masilahi yao ndani ya Salmin.

Kutoka Sophia Mjema anayetaka Samia abaki madarakani mpaka mwaka 2035, hadi Dimwa, anayeombea nyongea ya miaka miwili kwenye mihula ya Rais Mwinyi, wote hao wanatazama masilahi yao. Wanachokipata sasa waendelee kukivuna. Zaidi, ni kuendelea kujichomeka kwenye kurasa za vitabu vizuri vya Rais Samia na Rais Mwinyi.

Ukikusanya kelele zinazopigwa na ukaziweka kwenye kapu moja, jawabu la haraka ambalo unaweza kulipata ni Katiba mpya, ambayo itakuwa na ulinzi wa kutosha. Katiba ambayo itatandaza ukuu wake, yaani supremacy of constitution. Atakayethubutu kuichezea, anakwenda na maji.

Inawezekana kutumia mbinu kama ya Ujerumani, kuwa na ofisi kama BfV au Katiba ilindwe na mifumo, mithili ya Marekani. Jambo la muhimu ni kuwa na Katiba ambayo ni mwiko kusutwa na kupigwa masingi barabarani. Haiwezekani mtu akijisikia, atoe tamko la kuvunja Katiba, kama sasa, matamko yote ya kuongeza mihula ya urais au kuondoa ukomo wa hatamu ya urais, moja kwa moja ni uvunjifu wa Katiba ya sasa.