Mechi za maamuzi kuitikisa Ligi ya Mabingwa Ulaya

Muktasari:
- Aston Villa itakuwa nyumbani kuikabili PSG wakati Borussia Dortmund itakuwa na kibarua kigumu nyumbani dhidi ya Barcelona.
Ligi ya Mabingwa Ulaya itaendelea tena leo ambapo viwanja viwili vitakua katika mechi za maamuzi ya kutafuta washindi watakaoenda katika hatua ya nusu fainali.
Kule Ujerumani kwenye uwanja wa Signal Iduna Park, Nyuki wa kaskazini Magharibi, Borusia Dortmund watakuwa na kibarua kigumu cha kuikabili Barcelona katika mchezo wa marudiano kwani wana kazi ya kufanya kupindua meza baada ya kupoteza kwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza.

Barcelona imekuwa na mwendelezo bora katika michuano hiyo mikubwa Ulaya kwani hadi sasa imeshinda mechi tisa, imepata sare mechi moja na kupoteza mechi moja katika michezo 11 iliyocheza huku ikifunga mabao 36 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14.
Kutokana na mwendelezo bora wanaouonyesha Barcelona msimu huu ni dhahiri kabisa huwenda ikawa mwisho wa safari kwa Dortmund ambao walishindwa kutamba katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye uwanja wa Nou Camp, Hispania.
Kwa upande wa Dortmund wameshinda mechi saba, wamepata sare mechi mbili na kupoteza mechi nne katika michezo 13 waliyocheza huku wakifunga mabao 28 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 18.
Mshindi wa jumla kati ya Borussia Dortmund na Barcelona atakutana na mshindi baina ya Inter Milan dhdi ya Bayern Munich katika hatua ya nusu fainali.
Mchezo mwingine wa robo fainali utachezwa England kwenye uwanja wa Villa Park ambapo Aston Villa itakuwa nyumbani kuikaribisha PSG katika mchezo wa marudiano huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mabao 3-1 ilipokuwa ugenini kwenye uwanja wa Parc des Princes, Ufaransa.

Aston Villa imeshinda mechi saba, imepata sare mechi moja na kupoteza mechi tatu katika michezo 11 iliyocheza ambapo imefunga mabao 20 huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10.
Kwa upande wa PSG imeshinda mechi nane, imepata sare mechi moja na kupoteza mechi nne katika michezo 13 iliyocheza ambapo imefunga mabao 28 na kufungwa 11.
Mshindi wa jumla kati ya Aston Villa na PSG atakutana na mshindi kati ya Real Madrid dhidi ya Arsenal katika hatua ya nusu fainali.