Al Nassr kumfunga upya Ronaldo

Muktasari:
- Tangu alipojiunga na timu hiyo mwaka 2023, Ronaldo ameifungia Al Nassr mabao 90 katika michezo 99 aliyoitumikia timu hiyo.
Riyadh, Saudi Arabia. Al Nassr imetamba kuwa haidhani mshambuliaji wake Cristiano Ronaldo ataondoka klabuni hapo mara baada ya mkataba wake wa sasa kumalizika, Juni mwaka huu na inaripotiwa imeanza mchakato wa kumuongeza mkataba mpya.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 40, alijiunga na Al Nassr, Januari 2023 kwa mkataba wa miaka miwili na nusu ambao baada ya msimu huu kumalizika, utafikia tamati.
Kumekuwa na tetesi kuwa wapinzani wa Al Nassr, Al Hilal wamejipanga kufanya uhamisho wa kushtukiza wa nyota huyo huku pia Inter Miami nayo ikiripotiwa kumnyemelea.
Lakini makamu wa Rais wa Al Nassr, Khaled Al Malik amesema kuwa timu zinazoamini kuwa zinaweza kumnasa Cristiano Ronaldo zifute mawazo hayo kwa vile ni jambo ambalo haliwezekani na mchezaji huyo atabakia hapo kwa muda mrefu.
Al malik amesema kuwa akili ya Ronaldo inaiwaza Al Nassr na mshambuliaji huyo ambaye ni nahodha wa kikosi chao, anafurahishwa na maisha klabuni hapo.
“Ronaldo ni shabiki wa Al Nassr na tutatangaza uamuzi wa kusaini mkataba mpya katika vyombo vya habari. Tumesahau kuhusu ushindi dhidi ya Al Hilal na sasa tunachokifikiria ni ushindi dhidi ya Al Qadsiah,” alisema Malik.
Cristiano Ronaldo amekuwa na kiwango bora msimu huu akiwa na jezi za Al Nassr kutokana na mchango wake wa kuzalisha mabao kwa kufunga au kupiga pasi za mwisho.
Mshambuliaji huyo amehusika na mabao 36 katika mechi 35 za Al Nassr msimu huu ambapo amefumania nyavu mara 32 na kupiga pasi nne za mwisho.
Tangu alipojiunga na timu hiyo mwaka 2023, Ronaldo ameifungia Al Nassr mabao 90 na kupiga pasi 19 za mwisho katika michezo 99 aliyoitumikia timu hiyo.
Jumamosi iliyopita, Ronaldo alifunga mabao mawili na kuiongoza timu yake Al Nassr kupindua uongozi wa bao moja wa Al Hilal katika mchezo huo na kuifanya iibuke na ushindi wa mabao 2-1.
Mabao hayo mawili yalikuwa ni muendelezo wa Ronaldo kufumania nyavu ambapo yalimfanya afikishe mabao sita katika mechi nne mfululizo za Ligi Kuu Saudi Arabia.
Kwa sasa, Cristiano Ronaldo ndiye kinara wa kufumania nyavu katika Ligi Kuu Saudi Arabia akiwa amefunga mabao 23 na kupiga pasi tatu za mwisho katika mechi 26.
Al Nassr inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Saudi Arabia ikiwa na pointi 57 katika mechi 27.
Kinara wa ligi hiyo ni Al Ittihad yenye pointi 65 na inayoshika nafasi ya pili ni Al Hilal ikiwa na pointi 58.