Mayele anukia Saudi Arabia, Pyramids waingia mchecheto

Muktasari:
- Katika msimu wa 2024/2025, Al Fateh ilimaliza katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Saudi Arabia baada ya kukusanya pointi 39 katika mechi 34.
Kuna uwezekano mkubwa kwa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele akajiunga na timu mojawapo inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia na kuachana na Pyramids FC anayoitumikia hivi sasa.
Kiwango bora kilichoonyeshwa na Mayele katika msimu uliomalizika wa 2024/2025 kimezivutia timu mbalimbali hasa za Saudi Arabia ingawa pia zipo za Qatar na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Hata hivyo mtandao wa Win Win wa Saudi Arabia umeripoti kwamba kipaumbele cha mshambuliaji huyo raia wa DR Congo ni kucheza Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
Katika kundi la timu zinazotajwa kuwania saini yake, Al Fateh inaripotiwa kuwa ndio ipo mstari wa mbele kuhakikisha inamsajili mchezaji huyo katika kipindi cha sasa cha dirisha kubwa la usajili.
Al Fateh inaamini kwamba Mayele ataongeza makali katika safu yao ya ushambuliaji ambayo katika msimu uliopita ilifunga mabao 47 tu katika mechi 34 za Ligi Kuu ya Saudi Arabia, sawa na wastani wa bao 1.4 kwa mechi.
Na hamu ya timu za Saudi Arabia kumsajili Mayele inachangiwa na kauli ambayo mshambuliaji huyo aliitoa hivi karibuni ambayo ilionekana kama ya kuaga mashabiki wa Pyramids FC ambayo amebakiza mwaka mmoja wa kuitumikia.
“Misimu miwili ya Pyramids, mabao 41 katika mashindano yote. Asante kwa timu nzima na kila mmoja ambaye amenisaidia kwa kila njia. Alhmdulillah,” alisema Mayele muda mfupi baada ya mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Katika mashindano hayo ambayo Pyramids FC ilitwaa ubingwa, Mayele aliibuka mfungaji bora baada ya kupachika mabao saba.
Hata hivyo chanzo cha ndani ya Pyramids kimeuambia mtandao wa Win Win kuwa klabu hiyo haina mpango wa kumuuza Mayele.
“Hatuna mpango wowote wa kumuachia mchezaji yeyote tegemeo kwenye timu aondoke hivi sasa. Hatuna mpango wa kumuachia Mayele aondoke hasa ukizingatia mpango wa uongozi kubakisha wachezaji muhimu na kuimarisha timu na usajili mzuri kuzingatia mashindano magumu tutakayokabiliana nayo.
“Kuna hitajio la kuimarisha safu ya ushambuliaji katika dirisha la sasa la usajili wa kiangazi lakini hilo halihusiani na kuondoka kwa Mayele,” kimefichua chanzo hicho.