Mayele aiweka matatani Pyramids, kuondoka msimu ujao

Muktasari:
- Mayele alikuwa nguzo muhimu kwa Pyramids msimu huu akiisaidia timu yake kubeba taji la Klabu Bingwa Afrika msimu huu pamoja na kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Misri.
Cairo, Misri. Mshambuliaji wa Pyramids FC ya Misri, Fiston Mayele amezua wasiwasi kwenye timu hiyo baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa huenda akaachana na mabingwa hao wapya wa CAF msimu ujao.
Pyramids iliandika historia kwa kuichapa Mamelodi Sundowns kwa jumla ya mabao 3-2 katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa kwa mikondo miwili. Katika mchezo wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya 1-1, kabla ya Pyramids kushinda 2-1 nyumbani.

Mayele alitoa mchango mkubwa kwenye mafanikio hayo, akifunga mabao mawili dhidi ya Orlando Pirates kwenye hatua ya nusu fainali na jingine katika fainali dhidi ya Sundowns. Jumla ya mabao sita aliyofunga kwenye mashindano hayo yalimfanya aibuke mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Hii ni mara ya pili Mayele kushinda kiatu cha dhahabu katika michuano ya Kimataifa baada ya kufanya hivyo alipokuwa Yanga msimu wa 2022-2023 alipofunga jumla ya mabao saba kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Mbali na mafanikio hayo ya Afrika, Mayele pia amekuwa mhimili ndani ya ligi ya nyumbani ya Misri, akiisaidia Pyramids kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Misri akifunga jumla ya mabao nane na kufuzu fainali ya Kombe la Misri ambalo Pyramids imepoteza jana baada ya kufungwa kwa changamoto za mikwaju ya penalti 7-8 dhidi ya Zamalek baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya 1-1.

Pyramids wamwaga mamilioni kumbakiza
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Misri, hususani kutoka kwa mwandishi maarufu, Khaled El-Ghandour ni kwamba mabosi wa Pyramids wametoa ofa ya mkataba wa mamilioni kwa Mayele ikiwa ni juhudi za kuendelea kumbakisha kikosini baada ya kuisaidia timu hiyo kubeba taji la Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza.
Pyramids wametoa ofa ya mkataba mpya kwa Mayele yenye thamani kati ya dola milioni tatu hadi nne kwa mwaka, sawa na shilingi za Kitanzania 7.8 hadi 10.4 bilioni.
“Mayele ataondoka rasmi Pyramids baada ya fainali ya Kombe la Misri dhidi ya Zamalek. Tayari amepokea ofa kubwa zinazozidi dola milioni tatu kwa msimu, lakini amekataa kuendelea kuichezea klabu hiyo licha ya kuwa anapokea dola milioni moja kwa sasa,” amesema El-Ghandour.
Aliendelea kufichua kuwa Pyramids wameamua kumpa ofa hiyo kama ishara ya kuthamini mchango wake, hasa baada ya kuwa mfungaji bora kwenye michuano ya CAF na kuchangia timu kutwaa ubingwa.

Mayele, ambaye aliwahi kuhusishwa na uhamisho kwenda Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, pia alikiri kuwa na mazungumzo na kocha wa Amakhosi, Nasreddine Nabi kuhusu uwezekano wa kujiunga nao.
Kwa sasa, macho yote yameelekezwa kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, huku wadau wakisubiri kuona iwapo atakubali kubaki Misri au atachagua changamoto mpya baada ya msimu huu.

Chiefs walizembea wenyewe
Mchezaji wa zamani wa Kaizer Chiefs, Kanga Nzenza, amedai kuwa klabu hiyo ya Soweto ingeweza kuepuka fedheha ya kumaliza katika nafasi ya tisa kwenye Ligi Kuu msimu huu kama ingesikiliza ushauri wake wa kumchukua Mayele.
Chiefs walikamilisha msimu wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (2024/25) katika nafasi ya tisa kwa alama 32 tu, baada ya kushinda mechi nane, sare nane na kupoteza mara 12. Kocha mkuu wa timu hiyo, Nabi, aliwahi kudokeza kuwa tatizo kubwa la timu yake ni kutokuweza kutumia vyema nafasi za kufunga kasoro ambayo Mayele angeweza kuitatua.
Nzenza, ambaye aliwahi kuvaa jezi ya Amakhosi miaka ya 1990 na kutamba nao, amefichua kuwa kwa muda mrefu amekuwa akitamani kumuona Mayele akiwa sehemu ya kikosi hicho.
"Nilishawahi kuishauri Chiefs wamsajili Mayele," amesema Nzenza, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
"Tazama tu anachokifanya sasa. Nilikuwa wazi kabisa kuwa Chiefs wanamhitaji, ana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri hapa. Angetengeneza muunganiko mzuri na wachezaji wa Chiefs. Hata kama sasa si kwenye kiwango chake cha juu, bado ni tishio."
Nzenza ameongeza kuwa aliwahi kumtumia ujumbe Bobby Motaung, mkurugenzi wa masuala ya soka ndani ya Kaizer Chiefs, lakini hakufanikiwa kumpata moja kwa moja.
"Nilipata ugumu wa kuwasiliana na Bobby Motaung kwa sababu muda mwingi huwa yuko bize. Lakini ujumbe wangu ulikwenda: Chiefs wamsajili Mayele. Walipokea ujumbe lakini hawakuchukua hatua yoyote."
Nzenza alisema kuwa wakati huo Mayele alikuwa akiitumikia Yanga ya Tanzania, lakini baadaye klabu ya Pyramids FC kutoka Misri ilimchukua na sasa anakimbiza barani Afrika.
"Ni mchezaji wa kipekee. Kila anapoitwa timu ya taifa, hupewa heshima kama ‘super sub’ kwa sababu kila anapoingia hubadilisha mchezo. Angalia tu namna alivyowasumbua Mamelodi Sundowns kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika," amesema Nzenza akimsifu Mayele aliyefunga katika nusu fainali dhidi ya Pirates na fainali dhidi ya Sundowns.
Katika upande wa pili wa maisha yake, Nzenza amefichua kuwa kwa sasa hana uwezo wa kuona baada ya kufanyiwa upasuaji wa macho uliokwenda mrama katika hospitali ya Tembisa, jambo ambalo limeathiri maisha yake kwa kiasi kikubwa.

"Bado nafuatilia soka nikiwa nyumbani kupitia redio na televisheni, nikiwa nimekaa na familia yangu. Wananielewesha kwa sababu wanajua mapenzi yangu makubwa katika mpira. Ni jambo la huzuni kuwa siwezi kuona tena. Ningependa sana kupata mfadhili ili niweze kuonana na madaktari bingwa wa macho," amehitimisha kwa masikitiko nyota huyo wa zamani wa Kaizer Chiefs.