Man United yaongeza straika mwingine

Muktasari:
- Na kwa kuanza, Man United itatuma skauti wake kwenye mechi ya kimataifa ambayo itawakutanisha mastraika wawili ambao wapo kwenye orodha ya wale inaowataka kwa ajili ya msimu ujao.
MANCHESTER, ENGLAND: HABARI ndo hiyo, Manchester United imeongeza straika wa tano kwenye orodha ya wakali inaowasaka kwa ajili ya kumpa kocha Ruben Amorim jeuri ya kuwa na watu wa mabao kwa ajili ya msimu ujao.
Na kwa kuanza, Man United itatuma skauti wake kwenye mechi ya kimataifa ambayo itawakutanisha mastraika wawili ambao wapo kwenye orodha ya wale inaowataka kwa ajili ya msimu ujao.
Awali, iliripotiwa Man United imeweka mezani majina ya mastraika wanne, lakini sasa imeongeza mmoja na kufanya mastraika hao kuwa wa tano, ambapo wawili itawatazama kwenye mechi hizi za kimataifa, akiwamo straika wa Ipswich Town, Liam Delap.
Man United itakuwa bize sokoni wakati dirisha lijalo litakapofunguliwa kunasa huduma ya straika mpya, ambaye atakuja kuhakikishia timu hiyo mabao.
Miamba hiyo ya Old Trafford imefunga mabao 37 tu kwenye Ligi Kuu England msimu huu, mabao 32 pungufu ya yale yaliyofungwa na vinara wa ligi hiyo, Liverpool na sasa wanataka kumaliza tatizo hilo.
Kwa sasa, mastraika wa Man United ni Rasmus Hojlund na Joshua Zirkzee, lakini kocha Amorim kwa sasa amekuwa akimtumia Zirkzee kwenye majukumu mengine kabisa ndani ya uwanja.
Straika Delap atakabiliana na Hugo Ekitike wakati timu ya taifa ya England ya U-21 itakapokabiliana na Ufaransa, Ijumaa huku Man United ikivutiwa na washambuliaji wote hao wawili. Delap amekuwa kwenye kiwango bora tangu alipoondoka Manchester City, wakati Ekitike amefunga mabao 19 kwenye kikosi cha Eintracht Frankfurt msimu huu.
Orodha ya mastraika wanne wa awali waliokuwa kwenye rada ya Man United ni Ekitike, staa wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, Victor Osimhen na mtambo wa mabao wa Sporting CP, Viktor Gyokeres. Imemwongeza Delap baada ya kuwapo kwa ugumu wa kumsajili Gyokeres.
Delap amekuwa akiwindwa pia na timu nyingine ikiwamo Chelsea na Tottenham, wakati Man City yenyewe ikiweka kipengele cha kuwaruhusu kumnunua tena mshambuliaji huyo itakapoamua kufanya hivyo.