Man United kwa Mbeumo kuna kipengelee!
Muktasari:
- Man United imeliweka jina la Mbeumo kwenye kipaumbele chao cha usajili wa msimu huu ili kwenda kumalizana na tatizo la ufungaji wa mabao lililowakabili msimu uliopita.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United inakabiliwa na ishu nyingine kwenye mpango wao wa kumsajili staa wa Brentford, Bryan Mbeumo katika kipindi cha dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi.
Man United imeliweka jina la Mbeumo kwenye kipaumbele chao cha usajili wa msimu huu ili kwenda kumalizana na tatizo la ufungaji wa mabao lililowakabili msimu uliopita.
Miamba hiyo ya Old Trafford imeshuhudia ofa zao mbili kwa ajili ya Mcamerooni huyo zikikataliwa na Brentford, ambao bado wameshikilia msimamo wao wa kutaka kulipwa Pauni 63 milioni.
Man United bado ina matumaini ya kumsajili staa huyo huku ikiwa na uhakika dili litakamilika kabla ya ziara ya kwenda Marekani kwenye mechi za maandalizi ya msimu ujao.
Lakini, kuna wasiwasi. Tottenham nayo ilikuwa ikimtaka staa huyo, kabla ya Mbeumo mwenyewe kuweka kiupambele chake cha kwenda Old Trafford.
Na sasa ishu ya usajili wa Mbeumo inaweza kuwa ngumu baada ya kuibuka kwa timu nyingine inayotaka huduma ya mchezaji mwingine kwenye kikosi cha Brentford.
Nottingham Forest imepiga hodi Brentford kwenda kuulizia huduma ya Yoanne Wissa, ikihitaji saini yake ili akarithi mikoba ya Anthony Elanga, ambaye anaweza kwenda kujiunga na Newcastle muda wowote kuanzia sasa.
Uhamisho wa Wissa kwenda City Ground ukitokea, utawafanya Brentford sasa matumaini yao makubwa kubaki kwa mchezaji Mbeumo, ni silaha yao, asiondoke.
Hilo linaweza kuiweka Man United kwenye matatizo makubwa ya kumpata Mbeumo kama itachelewa kukamilisha dili hilo kabla ya Wissa kusajiliwa na Nottingham Forest.
Mbeumo, 25, alikuwa na msimu bora kabisa huko Brentford msimu uliopita alipofunga mabao 20 katika michuano yote na mkataba wake wa sasa umebakiza mwaka mmoja tu huko Gtech Community.