Man United inavyomchelewesha Garnacho kwenda Chelsea
Muktasari:
- Chelsea bado ipo mbali na kiwango cha pesa inachotaka Man United kwenye mauzo ya mchezaji huyo, ambapo inataka Pauni 40 milioni pamoja na bonasi nyingine.
London, England. Winga wa Manchester United, Alejandro Garnacho anaamini kwamba atakwenda kuwa mchezaji mpya wa Chelsea wakati dirisha la usajili litakapofungwa.
Chelsea bado ipo mbali na kiwango cha pesa inachotaka Man United kwenye mauzo ya mchezaji huyo, ambapo inataka Pauni 40 milioni pamoja na bonasi nyingine.
Chelsea ilijaribu kuishawishi Man United juu ya dili la kubadilishana wachezaji wakiwataja mastaa Christopher Nkunku na Tyrique George, lakini hakuna chochote kinachoendelea.
Timu hiyo inamthaminisha Garnacho kuwa na thamani ya Pauni 30 milioni, lakini Man United inadai thamani yake inazidi Pauni 50 milioni, lakini inataka kumuuza kwa bei ya chini kidogo baada ya kutokuwapo kwenye mipango ya kocha Ruben Amorim.
Licha ya kuwapo kwa hiyo sintofahamu, Garnacho anaamini Chelsea ina dhamira ya dhati katika kunasa saini yake na ndiyo maana amegomea ofa za timu nyingine, ikiwamo kwenda kwa mkopo Bayern Munich. Chelsea yenyewe inataka kuwaachana na Nkunku na Nicolas Jackson huku ikimweka sokoni Raheem Sterling aondoke kwa mkopo ili wao wawe na nafasi ya kunasa huduma ya Garnancho.
Garnacho hayupo kwenye mipango ya kocha Amorim na aliambiwa atafute timu. Wachezaji wengine wa Man United ambao Amorim anataka waondoke ni Jadon Sancho, Antony na Tyrell Malacia.
Marcus Rashford alikuwa kwenye orodha, lakini alishaondoka kwenda Barcelona kwa mkopo huku kukiwa na makubaliano ya kulipa Pauni 30 milioni kumchukua jumla mwakani.