Man City yaichapa Arsenal, mbio za ubingwa EPL nyeupe
Kiungo wa Man City, Bernardo Silva wakati akimzuia mshambuliaji wa Arsenal, Kai Harvert katika pambano la Ligi Kuu England kwenye Uwanja wa Etihad. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Arsenal inaongoza msimamo wa Ligi Kuu EPL ikiwa na pointi 70 katika mechi 33 huku Man City ikiwa nafasi ya pili na pointi 67 katika mechi 32.
Manchester, England. Man City imezidi kuiongezea presha Arsenal katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) baada ya leo Jumapili, Aprili 19, 2026 kuichapa kwa mabao 2-1.
Ushindi huo umeifanya Man City ipunguze pengo la pointi baina yake na Arsenal inayoongoza msimamo wa ligi kubakia tatu huku timu hiyo inayonolewa na Pep Guardiola ikiwa na mechi moja mkononi.
Waliopeleka kilio Arsenal katika mechi ya leo ni Rayan Cherki na Erling Haaland waliofunga bao katika kila kipindi cha mchezo. Bao pekee la Arsenal katika mechi ya leo limefungwa na Kai Havertz.
Huo ni ushindi wa kwanza kwa Man City dhidi ya Arsenal katika EPL baada ya kucheza mechi tano mfululizo bila kupata ushindi tangu Aprili 26, 2023.
Huo ni mchezo wa 10 mfululizo kwa Man City kutopoteza katika EPL wakikaribia rekodi yao ya kutopoteza mechi 11 mfululizo waliyoiweka kuanzia Machi 15, 2025 hadi Agosti 16, 2025.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Liverpool imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Everton, Aston Villa imeichapa Sunderland mabao 4-3 na Nottingham Forest imeibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Burnley.