Lampard aipaisha Coventry City EPL baada ya miaka 25
Muktasari:
- Mara ya mwisho kwa Coventry City kushiriki Ligi Kuu England (EPL) ilikuwa ni msimu wa 2000/2001 ilipomaliza ikiwa nafasi ya 19 katika msimamo wa ligi na pointi zao 34.
Hatimaye kiu ya muda mrefu ya mashabiki wa Coventry City imetamatika baada ya klabu hiyo kufanikiwa kurejea katika Ligi Kuu England (EPL) kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2000/2001.
Chini ya kocha Frank Lampard, Coventry imepata tiketi ya kupanda daraja kufuatia sare ya mabao 1-1 dhidi ya Blackburn Rovers katika mchezo wa Championship uliochezwa jana Aprili 17, 2026.
Matokeo hayo yameihakikishia Coventry kumaliza nafasi ya kwanza katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 86, idadi inayotosha kuirejesha moja kwa moja EPL.
Katika mchezo huo uliokuwa na presha kubwa, Coventry ilijikuta nyuma baada ya Ryoya Morishita kuifungia Blackburn bao la kuongoza dakika ya 54. Hata hivyo, juhudi za wageni hao zilizaa matunda dakika ya 84, pale Bobby Thomas alipofunga bao la kusawazisha lililowapa tiketi ya kupanda daraja.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Lampard alisema mafanikio hayo yana maana kubwa kwake na kwa mashabiki wa klabu hiyo.
“Ni jambo la kipekee. Mashabiki wamepitia mengi – huzuni na nyakati ngumu. Kupanda daraja na klabu kama hii kunaleta hisia kubwa,” alisema Lampard.
Aliongeza kuwa wachezaji wake wameonyesha moyo wa kipekee na wanastahili kusherehekea mafanikio hayo makubwa.
Chini ya Lampard, Coventry imekuwa na msimu bora ikionesha uwiano mzuri kati ya ushambuliaji na ulinzi, jambo lililoipa uthabiti wa matokeo. Mafanikio haya yanarejesha kumbukumbu za enzi zao za ubora walipodumu EPL kwa miaka 34 mfululizo kuanzia 1967 hadi 2001, huku mafanikio yao makubwa yakibaki kuwa ubingwa wa FA Cup mwaka 1987.
Kwa upande wa Blackburn Rovers, sare hiyo imeiacha ikipepesuka katika nafasi ya 19 kwenye msimamo wa Championship ikiwa na pointi 49, hali inayoweka hatma yake pabaya kuelekea mwisho wa msimu.