Arteta atoa tahadhari Arsenal kumaliza msimu bila taji
Meneja Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Hata hivyo, timu hiyo inakabiliwa na changamoto ya majeruhi, huku Declan Rice, Bukayo Saka, Martin Ødegaard na Jurrien Timber wakikosa mazoezi.
London, England. Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta amewataka wachezaji wake kucheza bila hofu katika mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Sporting Lisbon.
Kauli hiyo inakuja wakati presha ikiongezeka kwa miamba hiyo ya London Kaskazini kufuatia matokeo mabaya, ikiwemo kupoteza fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Manchester City, kutolewa katika Kombe la FA na Southampton na kichapo cha nyumbani dhidi ya Bournemouth.
Matokeo hayo yameifanya Arsenal kukaribia kumaliza msimu wa sita mfululizo bila taji. Hata hivyo, Arteta amesema bado wana nafasi kubwa ya kubadili hali hiyo.
“Hakuna hofu, ni motisha tu. Hiyo ndiyo ninayotaka kuona kwa wachezaji na mashabiki,” amesema Arteta.
Arsenal inaingia kwenye mchezo wa robo fainali ya pili ikiwa na faida ya ushindi wa 1-0 walioupata ugenini.
Hata hivyo, timu hiyo inakabiliwa na changamoto ya majeruhi, huku Declan Rice, Bukayo Saka, Martin Ødegaard na Jurrien Timber wakikosa mazoezi.
Arteta amesema huenda baadhi yao wakarejea uwanjani, huku akibainisha kuwa Saka bado ana tatizo la kisigino cha nyuma.
Naye mchezaji Eberechi Eze amesema hawajali wanaobeza uwezo wao, akisisitiza kuwa timu hiyo ina uwezo wa kushinda na itathibitisha hilo msimu huu.
“Sijali watu wanavyofikiria au wanavyosema kuhusu sisi kushinda. Ninajua tuna timu yenye uwezo mkubwa na tumethibitisha tuko katika kiwango cha juu. Tutakaposhinda, kila mtu atalazimika kukubali hilo.”
Mshindi wa jumla kati ya Arsenal au Sporting CP atakutana na Atletico Madrid ambayo jana iliitupa nje Barcelona na kutinga hatua ya nusu fainali.