Makocha, wachezaji walia na ratiba Ligi Kuu
Muktasari:
- Beki wa kati wa Namungo FC, Hussein Kazi amesema kuchelewa kumalizika kwa ligi kunafanya wakose muda wa kutosha wa kuwa na familia zao.
Dar es Salaam. Kuchelewa kumalizika kwa msimu wa 2025/2026, kumewaibua makocha na wachezaji wa klabu tofauti za Ligi Kuu ambao wamesema kunawapa athari mbalimbali hasi, kubwa ikiwa ni kukosa muda wa kutosha wa mapumziko.
Athari nyingine ni timu kutopata maandalizi mazuri ya msimu unaofuata lakini pia kupata gharama za ziada za kutunza wachezaji.
Kilio hicho kimekuja baada ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kutangaza kuwa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati 'Kombe la Kagame' yatachezwa kuanzia Julai 18 hadi Agosti 9 mwaka huu.
Mashindano hayo ya Kombe la Kagame, yatamalizika wiki mbili kabla ya kuanza kwa mechi za awali za mashindano ya Klabu Afrika zilizopangwa kuanza Septemba nne.
Kwa klabu za Tanzania, ratiba hiyo inaweza kuzibana zaidi kwa vile hazitopata muda mwingi wa kupumzika na kujiandaa na msimu mpya kwani Ligi Kuu msimu huu itafikia tamati Juni 30 na fainali ya Kombe la CRDB itachezwa Julai 4.
Pia yanaeza kuingiliana na mechi za shindano la Ngao ya Jamii ambalo huchezwa wiki moja kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi.
Hata hivyo, kama msimu wa ligi ungemalizika Mei mwishoni kama kalenda ya mwanzo ilivyoonyesha kabla ya kufanyiwa mabadiliko kadhaa, timu na wachezaji wangepata angalau miezi miwili ya mapumziko.
Wakizungumza na gazeti la Mwananchi, baadhi ya makocha na wachezaji wa timu za Ligi Kuu, wameiomba Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kujitahidi kuwa na ratiba rafiki na itakayomalizika mapema msimu ujao ili yaliyotokea msimu huu yasijirudie tena kwani yana athari nyingi hasi kwa timu, viongozi na hata kwa ligi yenyewe.
Kocha wa Singida BS, Muhibu Kanu amesema ingawa kuna makosa yanafanywa na klabu zenyewe kuomba kusogezwa mechi mbele zinapokuwa na jukumu la kimataifa pia Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inatakiwa isimamie kalenda ya ratiba inayopangwa kwa msimu husika.
"Ligi inapochelewa kumalizika wachezaji wanakuwa na muda mchache wa kupumzika. Wengine mechi za mwisho timu zinakuwa ugenini zianze kurejea kambini. Viongozi wafanye mchakato wa nauli zao, kisha warudi makwao. Muda wote wapo na vibegi mgongoni, hilo linawachosha ninashauri tujaribu kuiga kwa wenzetu wanaokwenda na muda," amesema.
Amani Josiah wa Dodoma Jiji amesema itategemeana na muda wa kuanza kwa msimu mpya, lakini kama ligi ikiisha Juni na kuanza Agosti basi wachezaji watakuwa na muda mchache wa kupumzika
"Pia maandalizi ya msimu wa 2026/27 hayatafanyika kwa ukubwa unaotakiwa kocha kutengeneza uwiano w timu. Ili wale ambao hawakupata nafasi ya kucheza watumie muda huo kujiweka fiti,"
"Kila mchezaji ana mipango yake, wengine wanakuwa na ratiba za kuoa, baadhi yao wanakuwa wamekata tiketi mapema za kwenda kupumzika nje. Ikitokea ligi imechelewa kuisha basi kila kitu kinakuwa kimeharibika," amesema Josiah.
Kocha msaidizi wa Namungo, Ngawina Ngawina amesema athari ya moja kwa moja kwa wachezaji kutopata mapumziko inavyotakiwa.
"Mara nyingi ligi inakuwa inaanza Agosti katikati au mwishonI. Kwa klabu zinazoshiriki michuano ya CAF, zitawapumzisha wachezaji kwa wiki moja na hizi timu zingine zitawapumzika wiki mbili. Hivyo wakirejea mapema kambini kiakili na kimwili wanakuwa hawapo sawa," amesema Ngawina.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Yusuf Chippo amesema, "sijui msimu mpya utaanza lini kama itaanza Septemba bado wachezaji watakuwa na muda wa kupumzika na kama itaanza Agosti muda wao utakuwa mchache. Sasa itakuwa juu yao kujilinda kwa muda mfupi wanaopata, ili kupumzisha miili na kuipa nguvu mpya ya kupambana."
Kiungo mshambuliaji wa KMC, Daruwesh Saliboko anayemiliki mabao matano, amesema muda wa kupumzika unakuwa mchache, inapotokea hali kama hiyo mchezaji anatakiwa ajitunze mwenyewe na kuepuka kwenda kucheza mtaani.
"Wachezaji wengi tunapokuwa mapumziko tunapenda kucheza soka la mtaani, tofauti na wenzetu nje ambako wachezaji wanakwenda maeneo mengine nje kabisa na mpira ili kuingiza vitu vipya na kuruhusu mwili kupumzika vya kutosha," alisema Saliboko.
Beki wa kati wa Namungo FC, Hussein Kazi amesema kuchelewa kumalizika kwa ligi kunafanya wakose muda wa kutosha wa kuwa na familia zao.
"Ligi inapochelewa kuisha inawahi kuanza, sisi tunaocheza mikoani tunakosa muda wa kukaa na familia kwa muda mrefu. Ni tofauti na Ulaya wenzetu wanapopewa nyumba za kuishi zinakuwa zina nafasi za kukaa na familia zao pia tunakuwa hatujapumzika vya kutosha," amesema Kazi.