Maajabu ya Masaka na njia zitakazofunguka

Muktasari:
- Nilibahatika kuzungumza na rafiki yangu mmoja Christopher Atkins, maarufu kama Chris raia wa England anayefanya kazi ya uwakala wa wachezaji wakike hususani wanaotokea Afrika, nikaamuliza kwanini hana mchezaji hata mmoja aliyemtoa Afrika kumpeleka England? akanambia ni ngumu, sio rahisi.
Kutoka kuishi maisha ya bweni kule Alliance Girls baadae kutua Yanga, Sweden kisha Brighton katika Ligi Kuu ya Wanawake ya England, stori ya Aisha Masaka ina maajabu mengi ya kustaajabisha ambayo yatafungua njia nyingi kwake, wachezaji wenzake na taifa kwa ujumla katika soka la Wanawake.
Nilibahatika kuzungumza na rafiki yangu mmoja Christopher Atkins, maarufu kama Chris raia wa England anayefanya kazi ya uwakala wa wachezaji wakike hususani wanaotokea Afrika, nikaamuliza kwanini hana mchezaji hata mmoja aliyemtoa Afrika kumpeleka England? akanambia ni ngumu, sio rahisi.
Sikutaka kuamini kama kuna ugumu sana kwa sababu Asisat Oshoala alitoka Afrika moja kwa moja na kwenda Liverpool, lakini jibu alilonipa ni mchezaji huyo alikuwa ametoka kucheza Kombe la Dunia halafu alitokea Nigeria, nchi ambayo imepiga hatua sana katika soka la wanawake.
Akanieleza kwamba inahitaji kupoteza gharama na muda mwingi kwa wakala na timu ili kufanikisha dili la mchezaji wa Kiafrika wa kike kutua kwenye ligi hiyo, labda awe na uraia wa nchi mbili kama ilivyokuwa kwa Toni Payne anayeichezea timu ya taifa ya Nigeria lakini ana uraia wa Marekani alikozaliwa, staa huyu hivi karibuni alijiunga na Everton. Ugumu huo unatokana na vibali vya kazi na utayari wa timu husika kumchukua mchezaji.
Kwa takwimu tu, aliyoyasema rafiki yangu huyu yana ukweli kwa zaidi ya asilimia mia, wachezaji wote wakike wanaocheza timu za Afrika wanaotokea Ligi Kuu England basi wana uraia pacha wa aidha hapo England ama nchi nyingine Ulaya, unaweza kuliona hilo kwa Morocco ambayo ina Rosella Ayane anayechezea Tottenham ya Wanawake lakini alizaliwa pale Reading England.
Lakini ugumu huo umewezekana kwa Masaka, ambaye hajacheza Kombe la Dunia wala AFCON, kitu pekee cha kujivunia kwa Masaka ni kucheza Ligi ya Mabingwa na kufika hatua ya robo fainali akiwa na BK Hacken.
Achana na kucheza Ligi Kuu England, hiyo ni hatua kubwa sana. Katika soka la wanawake moja kati ya nchi kubwa ni Sweden. Soka la wanawake nchini humo limeendelea sana, ni ngumu sana hata wachezaji kutoka Ulaya kucheza ligi hiyo, inahitaji uwe na uwezo na uzoefu wa kutosha kufika huko ni moja ya ligi tano bora barani Ulaya.
Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Wanawake nchi bora zaidi huwa zinaingiza timu tatu, Sweden pia imo humo.
Wachezaji wengi wanaoingia katika ligi kwa wale wanaotokea Afrika huwa wanaanzia katika ligi nyingine Ulaya kama Uturuki, Israel na Khazakhstan mfano Flavine Mawete ambaye kwa sasa anaichezea Djurgardens IF ya nchini humo lakini kabla ya kufika hapo alianzia Uturuki akitokea Simba Queens.
Maajabu ya masaka yanaturudisha mwaka 2022, wakati ambao anasajiliwa na BK Hacken akitokea Yanga Princess, Masaka alikuwa akisumbuliwa na majeraha ya goti.
Baada ya kufika na kufanyiwa vipimo akakutwa na shida hiyo, akatibiwa hadi alipokaa sawa kisha ndio akaanza kucheza, sio tu kwa soka la Wanawake bali hata wanaume ni ngumu sana mchezaji kukutwa na majeraha halafu akasajiliwa, mara nyingi dili huwa linaishia hapohapo lakini hiyo haikutokea kwa Masaka na maajabu yake.
Usishangae kuona maajabu ya Masaka akitoka England akatua katika moja ya timu kubwa pale Hispania sehemu ambayo ni ndoto ya kila mchezaji wakike kwa sababu ya ubora wa soka na mafanikio ya timu za hapo hususani Barcelona ambayo ndio imetawala zaidi michuano ya Ligi ya Mabingwa katika miaka minne iliyopita ambapo imechukua mara tatu.
Aliondoka Tanzania akiwa hajaonja hata ladha ya ubingwa wa Ligi Kuu lakini maajabu yalikuwa sehemu ya maisha yake.
MAAJABU HAYA YANA MAANA GANI?
Kitendo cha Masaka kutua England kinakwenda kufungua mianya zaidi kwa wachezaji wakike wa Tanzania katika soko la kimataifa.
Inawezekana yasifungue milango kwa wachezaji wa Tanzania kwenda Ulaya, lakini itafungua kwenda nchi nyingine duniani.
Sio wachezaji weng wa Afrika wanacheza England kitendo chakuwa na namba ndogo katika eneo hilo kinafanya mchezaji husika kuonekana zaidi.
Timu nyingi hazitokuwa na ugeni zitakaposikia jina la mchezaji anayetoka Tanzania, tayari Masaka ameshatambulisha bendera.
Ingawa inaweza kuwa hasara au faida, ikiwa ataonyesha kiwango bora kiasi cha kuimba sana, itazidi kufungua milango na ikiwa hatofanya hivyo, inaweza ikafanya England iwe na taswira mbaya kuhusu wachezaji wa Tanzania.
Sio ajabu Masaka akifanya vizuri, Brighton ikamchukua Opa Clement, Diana Msewa, Julietha Singano ama Enekia Kasonga ambao wameshatoka nje ya mipaka ya Tanzania.
Ingawa hata kama atafanya vibaya kwa umri wake wa miaka 20, timu nyingi zinamuangalia kama mchezaji anayekua ambaye anaweza akawapa faida baada ya misimu miwili au mitatu.
Vilevile,kitendo cha kucheza ligi hiyo, kimeshamtambulisha kwenye kila nchi, ni ngumu sana Masaka kutoka England akaenda nchi ambayo ipo chini katika soka la Wanawake.
Ukiondoa kufungua milango kwa wachezaji wakike kwa kutua kwake England, Masaka pia atabadilisha maono ya wachezaji wengi wakike wa Tanzania.
Katika kipindi nilichobahatika kuwa mdau wa soka hili, nimeshuhudia zaidi ya wachezaji wawili wakikataa ofa za kwenda kucheza soka Ulaya.
Mafanikio ambayo Masaka atayapata nje na ndani ya uwanja, huenda yakaabdilisha mitazamo ya wachezaji wa aina hiyo na kuona kwamba kuna haja ya kutoka kwenda kucheza soka la kulipwa ili kufanikiwa zaidi.
Hadi sasa Tanzania ina zaidi ya wachezaji watano wanaoiwa timu ya taifa ambaowanacheza soka la kulipwa nje lakini huenda wakaongezeka zaidi kabla ya mwezi huu kumalizika kutokana na tetesi zilizopo juu ya baadhi ya wachezaji kuhusishwa na kwenda nje.
Sio idadi mbaya na wala sio idadi nzuri, wachezaji wengi wazuri wameendelea kuwa hapa nchini lakini sio kama hawapati nafasi za kucheza nje, wanapata ila ni jinsi wanavyofikiri, hivyo kwenda kwa Masaka huko huenda kukawafungua masikio.
Ukiondoa hilo, pia maajabu ya Masaka yaliyomfikisha England yatasaidia kuongezeka kwa mawakala wengi kutoka Ulaya watakaokuwa wanafanya kazi na wachezaji wa hapa nchini kwa sababu ya CV ambayo kama nchi imeipata kwa ajili ya Masaka.
Mawakala ambao pengine hawakuwa wanaamini kama wanaweza kupata vipaji vikubwa katika ardhi ya Tanzania wataanza kuangalia kwa jicho lapili. Kimsingi maajabu ya Masaka yamefungua njia zaidi ya moja ambazo zitakuwa na faida kwake, kwa wachezaji wenzake na taifa kwa ujumla.
REKODI BONGO
Alikuwa mfungaji bora msimu wa 2020/21 wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara akifunga mabao 35.
Msimu huo huo akiwa na timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 17 ya Cosafa yaliyofanyika Afrika Kusini alichukua tena kiatu kwa kuweka nyavuni mabao 10.