Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Liverpool, Man City vita ya ubingwa

Muktasari:

  • Huu utakuwa ni mchezo muhimu kwa kila timu na mashabiki wanatarajia kuona soka la kiwango cha juu kutoka kwa kila upande.

Kivumbi cha Ligi Kuu ya England katika raundi ya 13 kinatarajiwa kufikia kilele Jumapili hii, pale vinara wa msimu huu Liverpool, watakapokutana na mabingwa watetezi, Manchester City kwenye Uwanja wa Anfield.

Mchezo huu si tu ni mapambano ya pointi tatu, bali ni vita ya heshima, historia na utawala. Ni mtihani mkubwa kwa timu zote mbili, ambapo Liverpool wanajivunia kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi wakiwa na pointi 31 na matumaini ya kuendelea kufanya vizuri, huku Manchester City yenye pointi 23 wanahitaji kushinda ili kurejesha matumaini ya kutetea taji lao.

Huu utakuwa ni mchezo muhimu kwa kila timu na mashabiki wanatarajia kuona soka la kiwango cha juu kutoka kwa kila upande.

Kwa sasa, Liverpool wako kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa tofauti kubwa ya alama dhidi ya wapinzani wao wa karibu, huku nafasi ya kushinda taji ikiwa inaonekana dhahiri zaidi kwa kikosi cha kocha Arne Slot. Ushindi kwa Liverpool utapanua pengo lao dhidi ya Manchester City hadi alama 11, jambo ambalo linaweza kuzima kabisa matumaini ya City kutwaa taji kwa mara ya tano mfululizo. Hii ni hatua kubwa katika safari ya Liverpool kuelekea ubingwa wa ligi na wanajua kwamba kushinda dhidi ya City kutamaanisha kuwa wao ni wagombea wakubwa wa taji mwaka huu.


LIVERPOOL: KILELE CHA MAFANIKIO

Kikosi cha Arne Slot kimekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu. Kimeonyesha ubora wake katika mashindano yote, kikibeba ushindi mkubwa dhidi ya mabingwa wa Ulaya, Real Madrid, katikati ya wiki kwenye Ligi ya Mabingwa. Katika mchezo huo, Liverpool walipata ushindi wa 2-0, ambapo Alexis Mac Allister na Cody Gakpo walifunga mabao ya timu hiyo, huku kipa Caoimhin Kelleher akionyesha umahiri wake kwa kuokoa penati ya Kylian Mbappe. Liverpool walionyesha kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto kubwa, ushindi huo unawafanya kuwa na morali ya juu wanapokwenda kwenye mchezo huu dhidi ya Manchester City.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Liverpool walikwepa kudondosha pointi kwa kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Southampton katika pambano la kileleni na mkiani. Mohamed Salah, ambaye ameonyesha kuwa tegemeo kubwa kwa Liverpool msimu huu, alifunga mabao yote mawili katika kipindi cha pili na kuokoa jahazi la Slot. Huu ni uthibitisho mwingine wa uwezo wake mkubwa na umuhimu wake kwa Liverpool. Salah amekuwa na kiwango cha juu msimu huu, na kila mpenzi wa soka anajua kuwa ni mchezaji ambaye anaweza kubadilisha mchezo kwa kiwango cha juu.

Katika mechi sita zilizopita, Liverpool wamepata ushindi wa moja kwa moja katika mashindano yote, huku wakifunga mabao mawili au zaidi katika kila mchezo. Zaidi ya hayo, Anfield imekuwa ngome yao isiyovunjika kirahisi, hawajaruhusu nyavu zao kuguswa katika mechi tatu dhidi ya Real Madrid, Aston Villa na Bayer Leverkusen.

Hii ni dalili ya kujitolea kwa timu hii kuhakikisha kuwa wanatoa kiwango cha juu katika kila mchezo, na kwamba wanajua kuwa kushinda ni jambo la lazima ikiwa wanataka kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.


MAN CITY: MABINGWA WANAOYUMBA

Kwa upande wa Manchester City, hali ni tete. Kikosi cha Pep Guardiola kimejikuta kikihangaika kupata matokeo mazuri, huku kikipoteza nafasi muhimu katika mashindano yote. Kushindwa kwao 4-0 nyumbani dhidi ya Tottenham Hotspur wikendi iliyopita kumeongeza presha kwa Guardiola na kikosi chake. Katika mchezo huo, City walionyesha udhaifu mkubwa katika safu zao za ulinzi na ushambuliaji, jambo ambalo halikutarajiwa kutokana na ubora wao wa kawaida.

Mara ya mwisho City kushinda ilikuwa Oktoba mwishoni, na wanakutana na Liverpool ambayo imekuwa vizuri katika mechi za karibuni huku moto wao ukiwatisha vigogo wengi.

City kushindwa kwao kuibuka na ushindi katika Ligi ya Mabingwa katikati ya wiki dhidi ya Feyenoord  licha ya kuwa na uongozi wa mabao 3-0 kuliweka wazi mapungufu yao. Guardiola alishindwa kuongoza kikosi chake kurejesha umoja na nguvu, na mchezo huo ulionesha jinsi ambavyo timu hiyo ilivyokuwa na changamoto kubwa.

Hata hivyo, kuna mwanga wa matumaini kwa mashabiki wa City kutokana na rekodi yao ya ufungaji ugenini. Wamefunga mabao katika mechi 26 mfululizo za ugenini kwenye mashindano yote, na mara ya mwisho kushindwa kufunga ugenini ilikuwa Novemba mwaka jana dhidi ya Aston Villa, hili ni jambo ambalo Liverpool lazima litiliwe maanani.


HUKU SALAH KULE HAALAND

Mchezo huu utakutanisha wachezaji wawili wenye ushawishi mkubwa, Mohamed Salah kwa Liverpool na Erling Haaland wa Manchester City. Salah, akiwa na mabao muhimu msimu huu, ameendelea kuwa injini ya ushindi kwa Liverpool. Ana uwezo wa kutengeneza nafasi, kufunga mabao, na kuhamasisha wachezaji wenzake.

Kwa upande mwingine, Haaland, licha ya kuonyesha dalili za kushuka kiwango katika mechi za karibuni, bado ana uwezo wa kuibuka kuwa shujaa wa mchezo. Haaland anahitaji kurudi katika kiwango chake cha juu kama City wanataka kuendelea kubaki na matumaini ya kutetea taji lao.

Mbali na nyota hao wawili, wachezaji kama Alexis Mac Allister, Cody Gakpo na Trent Alexander-Arnold kwa Liverpool wanatarajiwa kuwa na mchango mkubwa. Kwa City, kurudi kwa Kevin De Bruyne kunaweza kuongeza ubunifu wa safu yao ya ushambuliaji, huku Ruben Dias akihakikisha uimara wa safu ya ulinzi. Mchezo huu pia utatoa nafasi kwa wachezaji wengine kama Gundogan, Nunes na Silva kuonyesha uwezo wao wa kufanya kazi pamoja na kutengeneza nafasi za mabao.


UPANGAJI WA VIKOSI

Liverpool wanatarajiwa kuanza na mfumo wa 4-3-3, wakimtumia Kelleher langoni, Alexander-Arnold na Robertson kama mabeki wa pembeni, Mac Allister, Gravenberch na Szoboszlai wakitawala kiungo. Salah, Diaz na Darwin Nunez wanatarajiwa kusimamia safu ya ushambuliaji. Huu ni mfumo ambao unawapa Liverpool nafasi ya kudhibiti mchezo na kuanzisha mashambulizi kwa kasi.

City, mfumo wa Guardiola 4-3-3 unaweza kuhusisha Ederson golini, Walker na Ake kama mabeki wa pembeni, Dias akiongoza safu ya ulinzi, De Bruyne, Gundogan na Nunes wakishika nafasi za kiungo. Ushambuliaji utategemea ubunifu wa Silva, Savinho na Haaland. Guardiola atakuwa na jukumu la kuhakikisha wachezaji wake wanarejea kwenye kiwango chao cha juu, hasa baada ya matokeo mabaya yaliyopita