Lionel Messi apiga bonge la bao

Muktasari:
- Sasa Miami imefikisha pointi nne kwenye kundi lake ikiwa inatakiwa kupata pointi moja kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Palmeiras ili kufanikiwa kufuzu hatua inayofuata.
Miami, Marekani. Supastaa wa Inter Miami Lionel Messi jana alifunga bao safi la mkwaju wa friikiki na kuipa timu yake ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Porto kwenye mchezo mkali wa Klabu Bingwa Dunia hatua ya makundi.
Katika mchezo wa kwanza wa timu hiyo wa michuano hiyo dhidi ya Al Ahly Messi hakuonyesha makali yake, lakini jana alikuwa staa kwenye mchezo huo huko akipiga pasi nyingi murua.
Ushindi huu umeifanya Miami kuwa timu ya kwanza wa Marekani kupata ushindi kwenye michuano hiyo inayoshirikisha timu 32 kutoka mataifa mabara mbalimbali.
Awali Porto ndiyo ilianza kupata bao kipindi cha kwanza, lakini kiungo Telasco Segovia akasawazisha mwanzoni tu mwa kipindi cha pili cha mchezo huo, huku Messi akitupia la pili kwa mkwaju wa faulo.
Kitendo cha Miami kupata ushindi huo kinamaanisha kuwa hii imekuwa timu ya kwanza kwenye michuano hiyo kutoka nyuma na kupata ushindi.
Staa huyo mwenye miaka 37, hili lilikuwa bao lake la 50 tangu alipojiunga na Miami katika michezo 61 tu ambayo ameitumikia timu hiyo.
Mara baada ya mchezo huo, staa huyo wa zamani wa Barcelona alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo huku mashabiki waliokuwa wamejazana uwanjani wakishangilia tukio hilo.
Sasa Miami imefikisha pointi nne kwenye kundi lake ikiwa inatakiwa kupata pointi moja kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Palmeiras ili kufanikiwa kufuzu hatua inayofuata.
Katika mchezo mwingine, PSG ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Botafogo, Seattle Sounders ilipoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Atletico Madrid, Palmeiras waliipiga Al Ahly mabao 2-0.