Ligi yarajea, Simba na Yanga sasa Machi 8

Muktasari:
- Mchezo wa mzunguko wa kwanza wa watani wa jadi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, Oktoba 19, 2024 ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.
Dar es Salaam. Yanga na Simba zitaumana Machi 8, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Hiyo inafuatia marekebisho ya ratiba ya ligi ambayo bodi ya Ligi Kuu Tanzania imeyafanya na kuyaweka hadharani leo.
Ratiba ya awali kabla haijafanyiwa marekebisho, ilikuwa inaonyesha kuwa miamba hiyo miwili nchini ingerudiana Machi Mosi mwaka huu.
Ratiba hiyo mpya ambayo imetolewa leo, imeonyesha kuwa Ligi itamalizika Mei 25 kwa uwepo wa mechi nane zitakazochezwa katika viwanja na miji tofauti.
Marekebisho hayo ya ratiba ya ligi yamefanyika baada ya kusogezwa mbele kwa fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) 2024 ambayo yalipangwa kufanyika hapa nchini, Kenya na Uganda kuanzia Februari Mosi hadi Februari 28 mwaka huu.
Kabla ya kuahirishwa kwa fainali za Chan, bodi ya ligi ilipanga kusimamisha Ligi Kuu hadi mwezi Machi mwaka huu.
Ratiba mpya iliyotoka inaonyesha kuwa Ligi itarejea tena Februari Mosi ambapo mechi ya kwanza itakuwa kati ya Yanga na Kagera Sugar, wakati Februari 2 Simba itasafiri kwenda kuvaana na Tabora, Februari tano kutakuwa na mechi mbili pia ambapo Yanga itacheza na Ken Gold, Tabora itavaana na Namungo huku Simba ikirejea uwanjani Februari 6 kuvaana na Fountain Gate, huku Azam ikicheza na KMC.