Ligi Kuu Bara sasa ruksa kutumia viwanja Zanzibar

Muktasari:
- Kasongo ameyasema hayo mbele ya wanahabari kwenye semina iliyoandaliwa na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Almas Kasongo amesema kuanzia msimu ujao wa Ligi 2024/25 ni ruksa kwa timu ya Ligi Kuu Bara kutumia viwanja vya Zanzibar.
Kasongo ameyasema hayo mbele ya wanahabari kwenye semina iliyoandaliwa na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).
Kasongo alisema katika kanuni iliyofanyiwa maboresho kuelekea msimu mpya ruhusa ya viwanja vya Zanzibar kutumika na timu za Ligi Kuu Bara ni kanuni moja wapo iliyofanyiwa marekebisho.
"Katikati ya msimu ofisi yangu illipokea ombi la timu ya Simba kwenda kutumia uwanja wa New Amaan Complex kwa ajili ya Ligi Kuu, lakini haikuwezekana kwa sababu ya kanuni japo hoja zao zilikuwa na mashiko.
“Tulikaa na Kamati ya Utendaji ya TFF na tukaona hakuna sababu ya kuzuia hilo na tukaona ni vyema kanuni hiyo ianze kutumika msimu ujao 2024/25," alisema Kasongo.
Wakati huohuo, Kasongo amesema ndani ya siku mbili umma utafahamu ratiba na maboresho ya Ligi Kuu Bara 2024/25.
“Ratiba ya ligi pamoja na maboresho ya kanuni zipo tayari na ndani ya siku hizi mbili ofisa habari wa ligi ataweka hadharani."
"Ni kweli tulikuwa kimya kwa muda mrefu, lakini kimya kirefu kina mshindo, hivyo tunaamini ratiba ya msimu huu itakuwa bora,” alisema Kasongo.
Wakati huohuo alisema viwanja visivyo na uwezo wa kubeba watu 3,000 havitatumika msimu wa 2024/25, uamuzi huo unalenga kuimarisha mazingira ya michezo kwa kuzingatia usalama na faraja ya mashabiki.
“Kiwanja ambacho hakitakuwa na jukwaa lenye uwezo kubeba wadau wa soka elfu tatu hakitatumika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara 2024/25 ili kulinda hadhi ya soka letu, tunaamini kuwa kuweka kiwango hiki cha chini kutaboresha usalama na kuongeza mapato ya vilabu kwa kuvutia mashabiki wengi, Bodi ya Ligi itashirikiana na vilabu na wadau kuhakikisha miundombinu inaboreshwa ili kufikia viwango vinavyohitajika." alisema.
Katibu Mkuu wa Coastal Union, Omar Ayoub alisema kama ni kweli taarifa hiyo ipo litakuwa jambo bora kuwahi kutokea kwa miaka ya hivi karibuni.
"Ni suala zuri na sisi kama Coastal Union tunalipokea kwa uzuri kwani tulikuwa Kisiwani Pemba kwa kambi ya muda tumekutana na viwanja bora na mazingira mazuri huko huenda na sisi tukachagua kuchezea huko kutokana na mazingira," alisema na kuongeza;
"Kutoka Tanga hadi Pemba tunatumia saa moja na nusu na kutoka Pemba hadi Unguja saa moja na nusu, hivyo tunaweza kutumia saa mbili kwenda na kurudi lakini safari ya Tanga kwenda Arusha ni zaidi ya masaa matatu hadi manne."