Kufukuzwa kazi kulivyochangia utajiri wa Mourinho
Muktasari:
- Hata hivyo, mbali ya kufukuzwa kwake, kitu kingine kilichozua mjadala ilikuwa ni kiasi cha pesa ambacho amekipata kama sehemu ya fidia ya kuvunjiwa mkataba wake.
London, England. Mwishoni mwa wiki iiyopita moja ya stori kubwa ilikuwa ni kufukuzwa Kocha Jose Mourinho kutoka kwenye Fenerbahce ya Uturuki baada ya kutolewa hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, mbali ya kufukuzwa kwake, kitu kingine kilichozua mjadala ilikuwa ni kiasi cha pesa ambacho amekipata kama sehemu ya fidia ya kuvunjiwa mkataba wake.
Mourinho ambaye alikuwa amebakisha msimu mmoja na Fenerbahce inadaiwa kupata Pauni 13 milioni, ambacho kwa jumla kinamfanya kupata takribani Pauni 100 milioni kama fidia za kuvunjiwa mkataba pesa ambzao zimemfanya kuwa na utajiri wa kutosha.
Hapa chini tumekuwekea utajiri wa kocha huyu na mali anazomiliki kijumla.
ANAPIGAJE PESA
Kwa sasa, utajiri wa Mourinho unaokadiriwa kufikia Dola 130 milioni. Kiasi hiki kinatokana na pesa alizopata kutokana na mishahara, udhamini, fidia alizolipwa kila alipofutwa kazi, pamoja na uwekezaji wake binafsi.
Mourinho amekuwa kocha wa timu kubwa kama Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, Manchester United, Tottenham, Roma na Fenerbahce ambazo zote zilikuwa zikimpa kati ya Euro 10 hadi 16 milioni kwa mwaka kama mshahara.
Pia, amejizolea pesa za kutosha zinazofikia Pauni 90 milioni kama malipo ya kuvunjiwa mkataba na baadhi ya timu tajwa hapo juu huku kiasi kikubwa zaidi akikipata alipovunjiwa mkataba na Man United(Pauni 10 milioni).
Mbwatukaji huyu pia amekuwa akipata pesa kutokana na mikataba ya udhamini kutoka kampuni mbalimbali anazofanya nazo kazi kama balozi wao.
Miongoni mwa kampuni hizo ni Adidas, Hublot, Jaguar, Heineken, Samsung, EA Sports, American Express na kwa jumla zinakadiriwa kumpa Pauni 20 milioni kwa mwaka.
MIJENGO
Anamiliki nyumba ya kifahari maeneo ya Belgravia, London, England yenye thamani ya takribani Pauni 25 milioni.
Pia ana mjengo kwao Ureno uliopo Villa Cascais, karibu kabisa na bahari. Nyumba hiyo ina thamani ya Dola 7 milioni.
Alipokuwa Italia alikuwa akiishi katika mjengo wenye thamani ya Dola 8 milioni. Nyuma hiyo ilikuwa na vyumba 7, bustani na bwawa.
MAGARI ALIYONAYO
Ferrari 612 Scaglietti -Dola 200,000.
Aston Martin Rapide -Dola 210,000.
Jaguar F-Type-Dola120,000
Jaguar F-Pace -Dola 80,000.
BMW X6-Dola70,000
Audi A7-Dola 70,000.
Audi A8-Dola 85,000
Honda Civic-Dola 20,000
Suzuki Vitara Dola 20,000
Renault 5-Dola 10,000
MSAADA KWA JAMII
Kwa sasa ni balozi wa World Food Programme (WFP), ambao ni mpango wa Umoja wa Mataifa wa kupiga vita dhidi ya njaa duniani.
Alishiriki kampeni za kusaidia watoto wa Israel na Palestina kutokana na michezo na aliwahi kutoa Pauni 22,000 kwa waathirika wa Tsunami.
FAMILIA NA BATA
Mourinho yupo katika ndoa na Matilde “Tami” Faria tangu mwaka 1989 na wana watoto wawili, mmoja wa kike aitwaye Matilde aliyezaliwa mwaka 1996 na wa pili wa kiume aitwaye Jose Mario Jr aliyezaliwa mwaka 2000.
Familia yake mara nyingi imekuwa ikiishi maisha ya kifahari jijini London na Setubal, Ureno, lakini mara nyingi huwa hawapendelei kujionyesha.