Kocha kasema...Yanga hii ni kiboko

Muktasari:
- Yanga ilianza msimu kwa kuifumua Kagera Sugar mabao 2-0, kabla ya kuizima KenGold na KMC kila moja kwa bao 1-0, lakini baadhi ya watu waliichukulia kama imeotea tu, kwa namna ushindi wa mechi hizo ulikuwa kwa mbinde, ndipo ikaizima Pamba ya Jiji kwa mabao 4-0.
Haijawahi kutokea, lakini ndivyo hali ilivyo. Yanga imezidi kuboresha rekodi zake katika Ligi Kuu Bara baada ya juzi usiku kushinda mchezo mwingine mgumu kwa kuichapa Singida Black Stars kwa bao 1-0 na kukwea kileleni mwa msimamo, huku kocha wa kikosi hicho akitoa tahadhari mapema kwa timu nyingine.
Yanga ilishinda mchezo wa nane mfululizo katika ligi hiyo tena bila kuruhusu nyavu zao kuguswa, ikiwa haijawahi kutokea nchini kwa miaka ya karibuni na sasa inajiandaa kukabiliana na Azam FC katika mechi nyingine ngumu itakayopigwa kesho Jumamosi, huku kocha Miguel Gamondi akifungukia ubora wa kikosi hicho na kusema wapinzani ni lazima waje kwa heshima.
Yanga ilianza msimu kwa kuifumua Kagera Sugar mabao 2-0, kabla ya kuizima KenGold na KMC kila moja kwa bao 1-0, lakini baadhi ya watu waliichukulia kama imeotea tu, kwa namna ushindi wa mechi hizo ulikuwa kwa mbinde, ndipo ikaizima Pamba ya Jiji kwa mabao 4-0.
Ikafuata zamu ya Simba, mapema watu walisema safari hii wangekutana na Ubaya Ubwela, kwani watani wao walikuwa wakigawa dozi nene kabla ya sare ya 2-2 na Coastal Union, lakini vijana wa Gamondi wakafanya kweli kwa kushinda bao 1-0 na kelele zinaanza kusikika kwa chinichini.
Kisha zikafuata JKT Tanzania ikapigwa 2-0 na baadaye Wagosi wa Kaya wakaipeleka mechi jijini Arusha na hiyo haikuizuia Yanga kushinda kwani iliipata ushindi wa bao moja ndipo ukafuata mchezo wa juzi usiku uliopigwa New Amaan Complex, mjini Unguja Zanzibar dhidi ya Singida, wale walioichukulia Yanga kama iliyopopteza makali kwa kushindwa kutoa zile dozi za 5-0 kama ilivyokuwa msimu uliopita ikausikilizia.
Kama utani, Singida ambayo ilikuwa haijaonja machungu ya kupoteza mchezo ikazimwa na bao tamu la Pacome Zouzoua na sasa itakuwa ni zamu ya Azam FC, timu pekee msimu huu katika mechi za mashindano iliyofanikiwa kuifunga Yanga bao katika mchezo wa Fainali ya Ngao ya Jamii, ilipocharazwa mabao 4-1.
Kuna wanaoamini, huenda Azam ikaitibulia Yanga kwa kurejea mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu msimu uliopita ilipowacharaza mabao 2-1, japo ilipoteza katika fainali ya Kombe la Shirikisho kwa penalti na ile ya Ngao ya Jamii, lakini Gamondi ameweka bayana kwamba kwake muhimu ni pointi tatu na sio mabao.
Gamondi alisema kwa ubora wa kikosi hicho wala hashangazwi na hatua hiyo ushindi wa mechi nane mfululizo na kwamba wameshamalizana na Singida na sasa wanaiweka akili kwa mchezo ujao wa Azam FC.
Akizungumza na Mwananchi Gamondi alisema mchezo huo wa juzi dhidi ya Singida ulitosha kutoa majibu kwamba zilikutana timu mbili bora zilizoanza vizuri ligi kuliko zingine na kutoa mshindi baina yao.
Gamondi alisema ni bahati mbaya tu timu nyingi pinzani zimekuwa hazitaki kuiheshimu timu yake na kwamba kushinda kwao mechi nane mfululizo kunatokana na ubora wa kikosi chake.
Kocha huyo Muargentina alisema kuwa Yanga kila mchezo ambao inakwenda kuucheza inaziheshimu timu zote nane ilizokutana nazo kisha kujipanga sawasawa ikitumia ubora wao na wala hawajawahi kuidharau timu yoyote.
"Siku zote nimekuwa nikisema hakuna mechi rahisi ni kama kila mchezo tunacheza fainali, hakuna mechi ambayo utasema Yanga itashinda kirahisi, sisi sio mashabiki ni makocha lazima tutangulize weledi katika kujipanga na hata namna ya kutafuta ushindi," alisema Gamondi.
"Tulijua mechi ya jana (juzi) dhidi ya Singida Black Stars itakuwa ngumu sana, kutokana na ubora wao hii ndio timu iliyocheza vizuri mechi zake nane za kwanza, ukienda kukutana na timu ya namna hiyo lazima utumie akili kubwa namna ya kutafuta ushindi.
"Bahati mbaya tu kuna timu au baadhi ya watu hawataki kuiheshimu Yanga kwamba tuna ubora mkubwa kulingana na kikosi chetu na hata namna tunavyocheza.
Aidha Gamondi alisema Baada ya kumalizana na Singida akili yao inabadilika haraka na kaunza kuupigia hesabu mchezo mwingine mgumu wakitarajiwa kukutana na Azam .
"Angalia baada ya mechi hii tuna saa 24 tu tunatakiwa kubadilika haraka na kuwa tayari kucheza mechi nyingine ngumu dhidi ya timu ngumu ya Azam FC, sio rahisi kukabiliana na ratiba ya namna hii na ukashinda sawasawa na bado ukaonekana una timu ya kawaida."
REKODI ZA KIBABE
Ushindi huo wa nane mfululizo ukaipa rekodi mpya Yanga ya Gamondi ikishinda mechi nane bila kuruhusu bao lolote ikiwa ni hatua ya kipekee.
Hata hivyo, rekodi hiyo itakwenda kukutana na timu ngumu ya Azam ambayo katika mechi 15 za ligi walizokutana baina yao matajiri hao wa Chamazi wamekuwa kipimo kizito mbele ya mabingwa hao wa Tanzania.
Yanga ilipokutana na Azam kwenye mechi tano za ligi zilizopita kila timu imepata bao lakini Yanga ikashinda tatu, ikipoteza moja na kutoa sare moja ambapo mara ya mwisho Yanga kuifunga Azam bila matajiri hao kuruhusu bao ilikuwa Oktoba 30,2021.

MENEJA WA PACOME
Katika hatua nyingine, mabosi wa Yanga kuonyesha hawataki kuchelewa baada ya kusikia watani wao Simba wanamvizia kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Pacome Zouzoua na sasa fasta wamemrudisha meneja wa nyota huyo yakiwa ni maandalizi ya kumpa mkataba mpya.
Meneja wa Pacome, aitwaye Zambro Traore tayari yupo nchini na juzi alikuwa Zanzibar akiushuhudia mchezo dhidi ya Singida, huku kiungo huyo akiamua ushindi kwa bao pekee alililolifunga kwa ufundi na akili kubwa akifumua shuti kali mbele ya msitu wa mabeki wa Singida na kipa Metacha Mnata.
Taarifa kutoka ndani ya mabosi wa juu wa Yanga ni kwamba Zambro amekuja kwa mualiko maalum akiitwa na uongozi wa klabu hiyo ikiwa ni hatua za mwisho za Pacome kusaini mkataba mpya.
Mbali na Pacome Yanga pia inataka kumalizana na beki wake wa kulia Yao Akouassi ambaye pia anasimamiwa na Zambro.
"Tunataka kumaliza haya mambo haraka ili hawa wachezaji Pacome na Yao wasaini mikataba mpya haraka, tunajua kila hesabu za wapinzani wetu,"alisema bosi huyo wa juu wa Yanga.
"Tulikuwa kwenye mazungumzo marefu ambayo yalishakamilika nadhani wiki hii tutamalizana nao ili waendelee kuwatumia Wanayanga, tulishasema kwamba haitakuwa rahisi kwa mchezaji tunayemtaka akaondoka hapa."
Pacome ambaye amefunga bao lake la pili msimu huu juzi mkataba wake ulikuwa unakwisha mwisho wa msimu huu sambamba na Yao hatua ambayo iliziamsha klabu zingine kuvizia saini zao.