Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dakika 15 za hatari Mashujaa, Simba

Muktasari:

  • Nyota wa Simba wakiongozwa na Jean Charles Ahoua ambaye amehusika kwenye mabao saba kati ya 16 yaliyofungwa na timu hiyo, wana jukumu kubwa la kuitawanya ngome ya Mashujaa ambayo haitakuwa na nahodha wake, Ibrahim Ame aliyepo timu ya taifa

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Fadlu Davids anafahamu kwamba hivi sasa ameachwa pointi tano na watani zao wa jadi, Yanga huku michezo wakiwa sawa kila mmoja anayo nane.

Katika kuifukuzia Yanga kileleni, Fadlu ana mtihani mzito leo ugenini mbele ya Mashujaa, mchezo ukipigwa Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma saa 10:00 jioni ukiwa ni wa tisa kwao kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini kuna uwezekano dakika 15 za mwanzo zikaamua mchezo.

Nyota wa Simba wakiongozwa na Jean Charles Ahoua ambaye amehusika kwenye mabao saba kati ya 16 yaliyofungwa na timu hiyo, wana jukumu kubwa la kuitawanya ngome ya Mashujaa ambayo haitakuwa na nahodha wake, Ibrahim Ame aliyepo timu ya taifa.

Kukosekana na Ame ambaye amekuwa akitengeneza pacha na Baraka Mtuwi, sasa hivi ukuta wa Mashujaa pale kati amesalia Baraka Mtuwi na Ibrahim Abbas.

Mashujaa katika mechi ngumu kama hizi wamekuwa wakitumia viungo wengi katika kuzima mashambulizi ya wapinzani hivyo leo tunaweza kushuhudia hilo likiendelea kufanyika chini ya Kocha Abdallah Mohammed ‘Baresi’.

Fadlu na vijana wake leo wakipata ushindi, watafikisha pointi 22 zitakazowaweka nafasi ya pili wakiwa sawa na Singida Black Stars lakini Wekundu hao wa Msimbazi wanabebwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.


Dakika hizi ni noma

Hapa kuna kitu ambacho Simba na Mashujaa wanatakiwa kuwa makini katika mchezo wa leo kwani kila mmoja ana dakika zake za hatari katika kufunga na kuruhusu mabao.

Simba katika mabao yake 16, imefunga mengi zaidi katika muda wa kipindi cha mwanzo wa mchezo hadi kufika dakika ya 15. Katika kipindi hicho, Simba imefunga mabao matano huku timu za Tabora United, Fountain Gate, Azam, Prisons na Namungo zikikumbana na balaa hilo.

Kuanzia dakika ya 31 hadi 45, Simba imefunga mabao matatu, hivyo timu hiyo imekuwa hatari zaidi dakika 15 za kwanza na 15 za mwisho wakati ambao kipindi cha kwanza kinakwenda ukingoni.

Mbali na hilo, Simba ambayo imeruhusu mabao matatu mpaka sasa, yote hayo yametokea kipindi cha pili, hivyo bado Kocha Fadlu anapaswa kuwakumbusha vijana wake kuwa makini kinapofika kipindi hicho.

Ukija kwa Mashujaa yenye mabao tisa ya kufunga na kuruhusu matano, imefunga matatu katika kipindi cha mwanzo wa mchezo hadi dakika ya 15. Muda huo ndiyo umeonekana pia kuwa vizuri kwao katika kufunga ambapo ni sawa na ilivyo kwa Simba.

Lakini pia, katika ishu ya kuruhusu mabao, mengi zaidi yametokea katika kipindi cha kati ya dakika 31 hadi 45. Kocha Baresi anapaswa kuwa makini na Simba ambayo pia ipo vizuri kipindi hicho katika kufunga mabao.


Jeuri ipo hapa

Kikosi cha Mashujaa kilichofunga mabao tisa na kuruhusu matano, kinapewa jeuri zaidi na David Ulomi na Ismail Mgunda ambao kila mmoja amefunga mabao mawili.

Mbali na hao, pia kuna Seif Karihe anayeongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji ambalo linamkosa Crispin Ngushi aliyepo timu ya taifa.

Wakati jeuri ya Mashujaa ikiwa hapo, Simba kwa asilimia kubwa inabebwa na eneo la kiungo cha ushambuliaji sambamba na safu ya ulinzi.

Timu hiyo ikiwa imeruhusu mabao matatu huku ikifunga 16, Jean Charles Ahoua ndiye kinara wao wa mabao akifunga matatu akifuatiwa na beki Che Malone Fondoh mwenye mawili sawa na washambuliaji Valentino Mashaka na Leonel Ateba.

Lakini pia, mabao ya Simba yamegawanywa kila eneo, yani mabeki, viungo na washambuliaji yeyote anakufunga kama alivyofanya Awesu Awesu, Edwin Balua, Steven Mukwala, Fabrice Ngoma, Mohamed Hussein, Shomari Kapombe na Debora Fernandes.

Msimu huu Mashujaa katika mechi nane ilizocheza, za nyumbani ni tano ambapo imeshinda mbili sawa na sare huku ikipoteza moja dhidi ya Singida Black Stars kwa bao 1-0 ambalo ndiyo pekee imeruhusu nyumbani.

Takwimu hizo zinaonyesha kwamba Mashujaa ikiwa kwao kuifunga si kitu rahisi hivyo Simba wana kazi kubwa ya kufanya leo licha ya kwamba wana rekodi nzuri ya kushinda mechi zote tatu za ugenini ilizocheza tena bila  kuruhusu bao.

Wakati wa kutengeneza mashambulizi, Mashujaa imekuwa ikitumia zaidi upande wa kulia ambapo huko imezalisha mabao matano kati ya tisa. Upande huo anacheza sana Abrahman Mussa na Omary Kindamba. Lakini pia ndipo anapocheza Mohamed Hussein 'Tshabalala' katika eneo la ulinzi la Simba.

Simba nayo inatumia mawinga na mabeki wake wa pembeni kutengeneza mabao, hivyo vita kubwa itakuwa pembeni ya uwanja, lakini pia hata pale kati kutakuwa na shughuli pevu.


Wababe wengine

Rekodi zinaonyesha huu ukiwa ni msimu wa pili kwa Mashujaa kushiriki Ligi Kuu Bara, wamekutana na Simba mara tatu msimu uliopita, mbili ligi kuu na moja Kombe la FA.

Katika mechi hizo tatu, moja wameshinda kwa penalti 6-5 baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa sare ya 1-1, hiyo ilikuwa Kombe la FA.

Lakini katika Ligi, mechi zote mbili Mashujaa imepoteza, nyumbani ilifungwa 1-0 na ugenini ikachapwa 2-0. Wachezaji wote waliofunga mabao katika mechi hizo tatu, leo hii hawapo hapo.

Katika ule mchezo wa Kombe la FA walipofungana 1-1 kabla ya penalti kuamua, Mashujaa ilianza kufunga kupitia Reliants Lusajo dakika ya 6, sasa hivi mshambuliaji huyo ametimkia Dodoma Jiji, huku mfungaji wa Simba akiwa Freddy Kouablan dakika ya 52, naye ameondoka mwisho wa msimu uliopita.

Zile za ligi, Simba iliposhinda 2-0, mfungaji alikuwa Clatous Chama dakika ya 58 na 73 ambaye amejiunga na Yanga, huku waliposhinda 1-0, mfungaji wa Simba alikuwa Saidi Ntibazonkiza dakika ya 17, naye hayupo kikosini hapo.


Kauli za makocha?

Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdallah Mohamed 'Bares', amesema: “Vijana wamekubali kujitolea kuipambania timu, muunganiko unaanza kuonekana kwa sababu katika mechi mbili za hivi karibuni tumepata mabao, hii inaonesha washambuliaji wameamka tofauti na tulivyoanza.

“Katika mchezo dhidi ya Simba malengo ni kufuta uteja dhidi yao hasa tukiwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani, tutapambana kutafuta ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi."

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, bado ana imani na kikosi chake baada ya kubainisha kwamba siku zinavyozidi kwenda kuna mabadiliko anayaona.

"Kikosi kinaendelea kuimarika siku hadi siku, tunacheza ugenini mechi inayofuata hivyo lazima tuwe imara kila idara ili kufanya vizuri.

"Kuna baadhi ya wachezaji majeruhi ambao tutawakosa, lakini waliopo wapo tayari kwa kuifanya kazi iliyo mbele yetu."