Klose na rekodi inayowatesa Messi, Ronaldo Kombe la Dunia
Muktasari:
- Lionel Messi wa Argentina ndiye anaonekana kuwa karibu zaidi kuvunja au kufikia rekodi tofauti katika mashindano ya mwaka huu.
Rekodi ambazo ziliwekwa hapo nyuma katika Fainali tofauti za Kombe la Dunia huenda baadhi zikavunjwa katika fainali za mwaka huu kutokana na baadhi ya mastaa kukaribia kuzifikia.
Aliyekuwa mshambuliaji wa Ujerumani, Miroslav Klose. Picha na Mtandao
Rekodi ya mfungaji bora wa muda wote
Aliyekuwa mshambuliaji wa Ujerumani, Miroslav Klose ndiye anayeshikilia rekodi ya hiyo akiwa na mabao 16 aliyofunga katika fainali nne tofauti za mashindano hayo kuanzia 2002 hadi 2014.
Katika fainali za mwaka huu, huenda nahodha wa Argentina, Lionel Messi mwenye mabao 13 akaifikia au kuivunja rekodi hiyo kwani anahitaji mabao matatu kufikia idadi ya mabao 16 au mabao manne kuvuka idadi hiyo na kuwa kinara mpya wa ufungaji katika michuano hiyo mikubwa duniani.
Mshambuliaji wa Ufaransa, Kylian Mbappé naye anaonekana kuwa karibu kufikia rekodi hiyo, akiwa na mabao 12, Mbappé anahitaji mabao manne kufikia rekodi ya Klose au bao moja kuvuka rekodi hiyo.
Mshambuliaji wa zamani wa Brazil, Edson Arantes do Nascimento, maarufu Pelé, alipokuwa amebebwa na wachezaji wenzake katika moja ya Fainali za Kombe la Dunia. Picha na Mtandao
Rekodi ya pasi za mabao
Mshambuliaji wa zamani wa Brazil, Edson Arantes do Nascimento maarufu Pelé ndiye kinara wa utoaji pasi za mwisho katika Fainali za Kombe la Dunia akifanya hivyo mara 10.
Hata hivyo, huenda rekodi hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu ikavunjwa katika fainali za mwaka huu na Messi ambaye ana idadi ya pasi nane za mwisho alizotoa.
Nahodha wa Argentina, Lionel Messi. Picha na Mtandao
Rekodi ya kushinda mechi
Mshambuliaji wa zamani wa Ujerumani, Miroslav Klose anaongoza kwa kushinda idadi ya mechi 17 akiwa na timu ya Taifa ya Ujerumani katika Fainali za Kombe la Dunia.
Lakini rekodi hiyo inaweza kufikiwa au kuvunjwa na Messi ambaye ameiongoza Argentina kushinda idadi ya mechi 16 katika Fainali za Kombe la Dunia.
Kipa wa Mexico, Guillermo Ochoa. Picha na Mtandao
Rekodi ya kushiriki
Katika fainali za mwaka huu, nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo anaungana na nyota wengine kama kipa wa Mexico, Guillermo Ochoa pamoja na Messi wakishiriki katika Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya sita mfululizo wakiivunja rekodi waliyoiweka katika fainali za 2022.
Nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo. Picha na Mtandao
Idadi ya mechi
Nahodha wa Argentina, Messi ndiye anaongoza kwa kucheza idadi nyingi ya mechi za fainali za Kombe la Dunia akicheza mechi 26 katika fainali hizo.
Hata hivyo, mpinzani wake wa karibu Ronaldo ambaye amecheza mechi 22 anaweza kuivuka rekodi hiyo iwapo Ureno itafika hatua za juu kuliko Argentina.
Moja ya Uwanja utakaotumika katikia Fainali za Kombe la Dunia. Picha na Mtandao
Idadi ya mabao katika shindano
Katika fainali za mwaka huu, idadi ya mabao yatakayofungwa huenda ikavuka ile ya fainali zilizopita ambapo yalifungwa mabao 172.
Kutokana na kuongezeka kwa timu kutoka 32 hadi 48 fainali za mwaka huu zinatarajiwa kuvunja rekodi hiyo ya mabao.