Kisa Man United vs Spurs bei ya bia yapaa Bilbao

Muktasari:
- Mbali na bia na vinywaji vingine kupanda bei, pia gharama za usafiri, chakula pamoja na malazi nazo zimepanda kwa kiwango kikubwa huku ulinzi ukiimarisha kila kona.
Bilbao, Hispania. Mashabiki wa Manchester United na Tottenham wameshaelezwa kuwa wajiandae kunywa bia kwa bei ghali zaidi wakati watakapokwenda kwenye mchezo wa fainali wa Europa nchini Hispania.

Wiki ijayo Manchester United inatarajia kuvaana na Spurs kwenye mchezo wa fainali wa kombe hilo, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Bilbao nchini Hispania.

Ujumbe uliopatikana kwenye hoteli kadhaa ambazo zinatarajiwa kupokea mashabiki zimesema kuwa bia zimepanda kwa asilimia 900, baada tu ya kufahamika kuwa timu hizo za England ambazo mashabiki wake ni wanywaji wazuri ndiyo zimeingia fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Ulaya.
Mji wa Bilbao, unatarajiwa kupokea mashabiki 80,000, huku ikielezwa kuwa ni tukio kubwa zaidi kufanyika kwenye eneo hilo kwa miaka ya hivi karibuni ambalo litahusisha mashabiki wengi.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa kati ya mashabiki hao, 30,000 pekee ndiyo tayari wana tiketi hadi sasa na wanaobaki hawana uhakika wa kuingia uwanjani siku hiyo, jambo ambalo linaonyesha kuwa biashara ya vinywaji itakuwa juu nje ya uwanja.

Tukio hili linafananishwa na lile la mwaka 2018 ambapo yalifanyika mashindano ya Fainali ya Kombe la Euro ya mchezo wa Rugby mjini hapo ambapo mashabiki waliuziwa bia moja kwa 10 euro, kiwango ambacho kilikuwa cha juu sana kwa kipindi hicho.
Timu hizo mbili za Ligi Kuu England zimekata tiketi hiyo baada ya kufanya vizuri kwenye michezo ya nusu fainali dhidi ya Athletic Bilbao kwa Man United na Bodo/Glimt kwa Spurs.

Timu zote mbili Spurs chini ya Ange Postecoglou kwa sasa ipo nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England huku Man United ikiwa chini ya kocha Ruben Amorim ipo nafasi ya 16, ikiwa imefanya vibaya zaidi kwa msimu huu kuliko mingine kadhaa iliyopita.

Mbali na bia na vinywaji vingine kupanda bei, pia gharama za usafiri, chakula pamoja na malazi nazo zimepanda kwa kiwango kikubwa huku ulinzi ukiimarisha kila kona.