Keane ampigia debe Diego Simeone Man United
Muktasari:
- Man United ambayo msimu huu haishiriki michuano ya Ulaya, tayari imeshacheza mechi saba za Ligi ya EPL ikishinda tatu, ikipoteza tatu na kuambulia sare moja.
Gwiji wa Manchester United, Roy Keane, ameutaka uongozi wa klabu hiyo kuachana na kocha Ruben Amorim haraka iwezekanavyo, ili kuinusuru timu hiyo ambayo imeanza vibaya msimu huu 2025-2026.
Man United ambayo msimu huu haishiriki michuano ya Ulaya, tayari imeshacheza mechi saba za Ligi ya EPL ikishinda tatu, ikipoteza tatu na kuambulia sare moja.
Keane ambaye aliwahi kuwa nahodha na kiungo wa miamba hiyo ya Old Trafford, amesema uongozi wa Man United haupaswi kuendelea kumvumilia Amorim, kwani hali huenda ikawa mbaya zaidi siku za usoni.
Amesema kuna haja ya kufanya uamuzi wa haraka na mtu anayempendekeza akabidhiwe kazi ya kurithi nafasi ya kocha huyo kutoka Ureno ni Diego Simeone, ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Atletico Madrid ya Hispania.
“Uongozi hauna budi kufanya uamuzi wa haraka wa kuachana na Amorim ili kunusuru hali hii inayoendelea kwa sasa, ukimya wao una maana mbaya sana, lakini kuna haja wakafanya jambo la kuachana naye kwani huyu kocha ameonesha kushindwa kabisa.
“Ukiniuliza sasa hivi, nani anafaa kurithi mikoba ya Amorim, kwangu ninaamini Diego Simeone ni mtu sahihi kwa sababu ana uzofu wa kutosha na anajua pa kuanzia kutokana na kuheshimu misingi ya kazi yake na ya klabu kubwa kama hii.
“Nimesema hili kwa miaka mingi. Ningependa kumuona... ningependa kuingilia... Simeone. Ningependa kumuona akija hapa. Nadhani ataleta mabadiliko makubwa, na huu ni muda sahihi wa mtu kama huyu kuja hapa."
Hata hivyo, pendekezo hilo la Roy Keane, huenda likawashtua wengi, ikizingatiwa uhusiano wa muda mrefu wa Simeone na Atletico Madrid, ambayo ameitumikia kwa zaidi ya miaka kumi sasa.
Rekodi ya uongozi wa Diego Simeone
Simeone amekuwa kocha mkuu akiwa na klabu kama Racing Club, Estudiantes, River Plate, San Lorenzo, na Catania kabla ya kutua Atletico Madrid.
Amekaa kwenye benchi la ufundi la Atletico Madrid kwa kuongoza mechi 955, akishinda mataji ya ndani na kufikia hatua kubwa katika michuano ya Ulaya.
Mechi - 955
Ushindi - 537
Sare - 216
Kipigo - 202
Mabao ya kufungwa - 1574
Mabao ya kufungwa - 862