Prime
Kanali Kipingu: Kutoka kambini hadi viwanjani kuibua vipaji
Dar es Salaam. Kwa zaidi ya miongo mitatu, Kanali Mstaafu Idd Kipingu ameshuhudia maelfu ya wanafunzi wakipitia mikononi mwake, wakati wengi wakimfahamu kama mwalimu na mwanajeshi, wachache wanajua mchango wake mkubwa katika kuibua vipaji vya michezo vilivyozalisha wachezaji, makocha na viongozi wanaotumikia michezo hadi leo.
Katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni, Kipingu ameeleza namna michezo ilikuwa sehemu muhimu ya malezi kwa wanafunzi wa shule za jeshi, hususani Shule ya Sekondari Jitegemee na Makongo, ambako alihusika katika kukuza vipaji mbalimbali vilivyokuja kuliwakilisha Taifa.
Kwa miaka mingi, shule za jeshi zimekuwa zikijulikana si tu kwa kufundisha taaluma, bali pia kwa kusisitiza nidhamu, uzalendo na michezo kama sehemu ya malezi ya mwanafunzi, mumo ambao umechangia kuzalisha wataalamu katika sekta mbalimbali, wakiwamo wanamichezo.
Akiwa mkuu msaidizi wa Sekondari ya Jitegemee na kisha mkuu wa sekondari ya Makongo, Kipingu anasema kote huko aliona umuhimu wa kuunganisha masomo na michezo kwa sababu aliamini mwanafunzi mwenye kipaji akipewa mazingira sahihi anaweza kuwa mchezaji mkubwa baadaye.
Baada ya kupewa jukumu la kuanzisha Sekondari ya Makongo, Kipingu anasema alipata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa Serikali wakati wa usajili wa shule hiyo mwaka 1994 kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika michezo shuleni, akisisitiza shule hizo zinaweza kuwa chanzo cha kupata timu za Taifa.
“Nilisema mbele ya Waziri wa Elimu wakati huo Profesa Philemon Sarungi na mbele ya mkuu wa jeshi aliyewakilishwa na Mkuu wa Utawala kwamba tukipewa usajili wa shule hii, itakuwa kiwanda cha kutengeneza timu za Taifa,” anasema Kanali Kipingu.
Kwa mtazamo wake, shule si sehemu ya kusoma pekee, bali pia ni eneo la kugundua vipaji ambavyo vinaweza kutumika kujenga tasnia ya michezo nchini.
Anasema michezo ina nafasi kubwa katika maisha ya mwanafunzi kwa sababu mbali na burudani, hujenga afya, nidhamu, ushirikiano na uwezo wa kushindana.
“Mchezo unatoa burudani, unamjenga mtoto, unampa afya na unamfundisha kushirikiana na wengine, Huwezi kuangalia masomo pekee ukamsahau mtoto mwenye kipaji cha michezo,” anasema.
Walimu waliokuwa na macho ya vipaji
Kanali Kipingu anasema moja ya mambo yaliyomsaidia kufanikisha kazi hiyo ilikuwa ushirikiano kutoka kwa walimu waliokuwa na uwezo wa kuona vipaji vya wanafunzi.
Anasema baadhi ya walimu walikuwa na mapenzi na michezo lakini walikosa nafasi ya kuviendeleza vipaji hivyo, hivyo yeye alitumia uzoefu wake kuwasaidia.
“Nilikuwa nawapigiwa simu walimu naambiwa kuna mtoto hapa ana uwezo fulani, namtuma mtu wangu wa kuangalia vipaji alikuwa anajulikana kwa jina la Banda akimuona na kujiridhisha tunamleta Makongo ili apate mazingira bora ya kuendelea,” anasema.
Kutoa fursa kwa Hasheem
Kipingu anakumbuka namna alivyogundua kipaji cha Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Hasheem Thabeet ambaye baadaye alikuja kuwa mmoja wa wachezaji wa kimataifa katika mchezo wa kikapu.
“Niliona kuna mtu mmoja mrefu sana, watu walikuwa wanamshangilia. Nikajiuliza huyu ni nani, anasoma wapi?” anasimulia.
Baada ya kumuuliza aligundua kuwa kijana huyo alikuwa mwanafunzi na alikuwa na uwezo mkubwa katika mchezo wa kikapu hivyo alimshawishi kujiunga na Makongo kwa kuongea na mzazi wake ili kuendelea kukuza kipaji chake.
“Nilimwambia aje hapa Makongo na bahati nzuri niliongea na mzazi wake na kipindi hicho sikujua kama Mungu alikuwa ameshapanga njia yake, lakini baada ya kuja alianza kuonekana zaidi,” anasema.
Kipingu anakumbuka pia kipindi ambacho shule za Tanzania zilianza kushiriki mashindano ya michezo ya Afrika Mashariki, yaliyoshirikisha Tanzania, Kenya na Uganda.
Anasema wakati huo Burundi na Rwanda bado hazikuwa zimejiunga, lakini baadaye nchi hizo ziliongeza ushindani katika mashindano hayo na aliomba ruhusa ya kupeleka timu za shule katika mashindano hayo kwa kupata nafasi ya kushiriki katika michezo mbalimbali.
“Nilipewa mwaliko na nikapeleka timu ya kikapu, soka na volleyball, tulikwenda kushindana na shule nyingine za Afrika Mashariki,” anasema.
Anasema katika kikosi cha kikapu Hasheem Thabeet ambaye aliwekwa nje lakini alimshawishi mwalimu wake kumuingiza dakika 10 zilizobaki ili kuongeza nguvunandipo alipoonekana.
“Nilimwambia mwalimu huyu mtoto mweke kwenye timu sikuwa namweka kwa sababu ni mwanafunzi wangu, niliona uwezo wake Mungu alikuwa ameshaandika njia yake,” anasema.
Hasheem Thabeet baadaye aliendelea kung’ara katika mchezo wa mpira wa kikapu, akicheza katika ligi mbalimbali za kimataifa na kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika Ligi ya NBA nchini Marekani, jambo ambalo lilithibitisha umuhimu wa kutambua vipaji mapema.
Vipaji vya mpira wa miguu
Mbali na kikapu, Kanali Kipingu anasema shule hizo zilikuwa na mchango mkubwa katika kuzalisha wachezaji wa mpira wa miguu walikuwa wakifanya kazi ya kuwatafuta na kuwalea vijana wenye uwezo ambao baadaye walipata nafasi za kucheza katika timu mbalimbali.
“Tulikuwa tunascout watoto wengi baadhi ya wachezaji waliopita katika mfumo huo na baadaye kuonekana katika soka la juu, akisema shule hizo zilikuwa sehemu ya kwanza ya kuwapa msingi wa taaluma,”anasema.
Baadhi ya wachezaji waliopita hapo ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wilfred Kidao, kocha wa soka la ufukweni Boniface Pawasa,kocha wa magolikipa Juma Kaseja,Nicodemas Nyagawa, kocha msaidizi wa Mtibwa Awadhi Juma, aliyekuwa kocha msaidizi wa Namungo Ngawina Ngawina ambaye alikuwa mchezaji wa kwanza kuchezea TP Mazembe.
Wengine ni Haruna Moshi maarufu Boban,Jerson Tegete huku upande wa muziki Kalala Junior, Jose Mara, Daz Nundaz
Mbali na hao waliosoma Makongo wapo waliokuwa watumishi ambao wamepata vyeo vikubwa kwenye michezo akiwepo Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Oscar Mirambo ambaye alipelekwa shuleni hapo na aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule ya sekondari ya Lwiko ya mkoani Ruvuma.
Amesema Mirambo alipelekwa Makongo kuwa mwalimu wa hesabu, fizikia na michezo ambapo kwa sasa amekuwa sehemu ya waibua vipaji na mkufunzi wa makocha ndani nan je ya nchi.
Kuanzisha Lord Baden
Wakati wengi wanapostaafu kazi zao hufikiria kupumzika na kufurahia matunda ya miaka mingi ya utumishi, kwake ilikuwa tofauti, baada ya kuvua sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mwaka 2007.
Aliamini bado alikuwa na jukumu kubwa la kulitimiza kwa taifa hakutaka maisha yake yawe hadithi ya mafanikio ya kijeshi pekee alitaka kuacha alama katika maisha ya maelfu ya vijana wa Tanzania.
“Kutokana na uzoefu huo, niliamua kujenga shule ambayo ingekuwa tofauti na niliamini mtoto akipata malezi bora, elimu nzuri na nafasi ya kushiriki michezo, anaweza kufikia mafanikio makubwa bila kujali ametoka katika mazingira gani,”anasema.
Ndani ya moyo wake kulikuwa na imani kwamba taifa imara halijengwi kwa silaha pekee, bali kwa vijana wenye elimu, maadili na nidhamu ndiyo maana mwaka mmoja baada ya kustaafu, mwaka 2008, akaanzisha Lord Baden Secondary School iliyopo Mapinga, Bagamoyo, shule ambayo kwa sasa haitoi huduma kwa sababu maalum.
Anasema miongoni mwa wanafunzi waliowahi kupitia katika shule hiyo ni msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Zuhura Othman Soud maarufu Zuchu, ambaye leo ni miongoni mwa wasanii wanaofanya vizuri zaidi nchini na Afrika Mashariki.
Michezo ni sehemu ya elimu
Kwa Kipingu, mafanikio hayo yalitokana na mtazamo kwamba michezo haipaswi kutenganishwa na elimu mwanafunzi anayeshiriki michezo anajifunza nidhamu, uwajibikaji na namna ya kushirikiana na wenzake.
“Mtoto anayefanya vizuri darasani na kwenye michezo anakuwa na uwezo mpana zaidi wa kukabiliana na maisha,” anasema.
Anaamini shule nyingi nchini zinapaswa kupewa mazingira ya kutambua vipaji mapema ili Tanzania iweze kupata wanamichezo wengi watakaoiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.
Kanali Kipingu anasema uzoefu wake katika shule za jeshi umemfundisha kuwa vipaji vipo kila mahali, kinachohitajika ni macho ya kuviona na mazingira ya kuvikuza.
“Mtoto anaweza kuwa mahiri sana, lakini kama hakuna mtu wa kumuona na kumuendeleza, kipaji kinaweza kupotea,” anasema.
Leo, anapotazama nyuma, Kanali Kipingu anasema furaha yake kubwa si cheo alichowahi kushika jeshini bali kuona vijana aliowahi kuwapa nafasi wakiiwakilisha Tanzania katika michezo, uongozi na taaluma mbalimbali. Kwake, huo ndio urithi mkubwa aliouacha kwa Taifa.
Mgogoro wa Yanga wampa shavu
Kanali Mstaafu Idd Kipingu anasema mgogoro mkubwa uliotikisa Yanga ni wa mwaka 1974 ambao uliomfungulia mlango wa kujiunga na klabu hiyo baada ya viongozi kufukuza sehemu kubwa ya wachezaji wa kikosi cha kwanza na kuanza kusaka vipaji vipya.
Anasema wakati huo alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako timu ya chuo ilikuwa ikifanya vizuri na kucheza mechi dhidi ya timu mbalimbali, zikiwemo Simba, Yanga na hata timu za Taifa. Kiwango chake kilivutia maskauti wa Yanga, huku aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Tambwe Leya akiwatuma watu kumfuatilia kabla ya kumshawishi kujiunga na kikosi hicho.
“Baada ya Yanga kuvunja kikosi, walikuwa wanatafuta wachezaji wapya, ndipo wakaanza kunifuatilia kupitia mechi nilizokuwa nacheza chuoni na baadaye nikajiunga na timu,” anasema.
Kipingu anasema timu inakwenda Mombasa, nchini Kenya hakwenda nayo hivyo mpasuko ulivyotokea wakavunja kikosi cha timu hiyo na kubaki wachezaji sita ambao hawakwenda nao.
Anasema alicheza na baadhi ya nyota waliokuwa wamebaki na wengine waliokuwa wamejiunga katika kikosi kipya ambao ni Mwinga Ramadhani, marehemu Seleman Said,Twaha Ufungo.
Hata hivyo, anasema maisha yake ndani ya Yanga hayakudumu kwa muda mrefu baada ya klabu kuingia tena katika migogoro ya kiuongozi na kisiasa iliyoathiri benchi la ufundi na kocha Tambwelea aliondolewa kufuatia matokeo mabaya, yakiwemo ya mchezo dhidi ya Simba. ambapo walifungwa goli 1-0
Wakati hayo yakitokea, Kipingu alikuwa akihitimisha masomo yake ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mara baada ya kuhitimu, alichukuliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa mafunzo ya kijeshi, hatua iliyomlazimu kuachana na soka la ushindani.
“Nilipoingia Jeshini nikalazimika kuyaweka pembeni maisha ya kucheza Yanga na kuanza safari mpya ya utumishi wa taifa, ingawa mapenzi yangu kwa mpira hayakuisha,” anasema.