Barker akoshwa Libasse kurejea kundini Simba
Dar es Salaam. Kiungo mshambuliaji wa Simba, Libasse Gueye, ameungana na timu hiyo akitokea mapumzikoni huku Kocha Mkuu, Steve Barker akisema bado wanahitaji muda wa kumuangalia kabla ya kufanya maamuzi kuhusu utayari wake wa kucheza.
Gueye alikuwa miongoni mwa wachezaji waliochelewa kuungana na kikosi kutokana na kuwa mapumzikoni baada ya kumaliza majukumu yake ya msimu uliopita, lakini tayari ameanza mazoezi na wenzake huku benchi la ufundi likifuatilia kwa karibu maendeleo yake.
Barker alisema mshambuliaji huyo bado hajafanya mazoezi ya kutosha, hivyo wataendelea kumfanyia tathmini katika kila kipindi cha mazoezi kabla ya kuamua kama yuko tayari kupewa nafasi ya kucheza.
"Amewasili tu hivi karibuni na hajafanya mazoezi mengi. Tutafuatilia namna alivyopitia mazoezi ya jana na kuona maendeleo yake katika mazoezi ya leo, kisha tutajua kama yuko tayari au la," alisema Barker.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini alisema hana tabia ya kuwahukumu wachezaji kwa muda mfupi, akieleza kuwa kila aliyesajiliwa au aliyerudi kambini anatakiwa apewe nafasi ya kuzoea mfumo, falsafa na misingi ya uchezaji wa Simba kabla ya kutathminiwa.
"Ni muhimu kwangu kuona kila mchezaji anaingia vizuri kwenye mfumo wetu wa uchezaji na kuelewa falsafa pamoja na kanuni tunazotaka kuzifuata. Hilo ndilo jambo tunaloendelea kulifanyia kazi kila siku."
Barker alisema ameridhishwa na namna wachezaji wapya walivyoanza kuendana na kikosi, lakini akasisitiza tathmini itaendelea katika kipindi chote cha maandalizi kwa sababu hawezi kufanya maamuzi kwa kuangalia mchezo mmoja au mazoezi machache.
"Siwezi kumhukumu mchezaji kwa mechi moja au mazoezi machache. Tunahitaji muda wa kuwaona wote, kuwapa nafasi na kutambua namna wanavyoweza kuitumikia timu,” amesema Barker.
Kurejea kwa Gueye kunazidi kuongeza ushindani kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba wakati timu hiyo ikiendelea kutumia michuano ya kombe la Kagame kujenga kikosi kitakachoanza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara ambapo pazia lake watafungua kwa kucheza dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Agosti 12.
Barker amekiri kikosi chake bado hakijafikia kiwango cha juu cha utayari kutokana na wachezaji wengi kurejea hivi karibuni kutoka mapumzikoni lakini akaeleza kila mchezo wa maandalizi unawapa nafasi ya kuboresha kiwango na kuongeza uelewano.
"Ni wazi bado hatujafikia utayari tunaoutaka kwa sababu tumetoka mapumzikoni. Kila mchezo unatupa nafasi ya kukua, kuboresha kiwango na kuendelea kujenga timu,” amesema Barker.
Kocha huyo anaamini mashindano ya Kagame yatawasaidia kupata picha halisi ya uwezo wa kila mchezaji kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa mashindano.