Julen Lopetegui achukua nafasi ya Moyes

Klabu ya West Ham ya Ligi Kuu England imemtangaza Julen Lopetegui kuwa kocha wake mkuu akichukua nafasi ya David Moyes aliyeondoka baada ya mkataba wake kumalizika.
Moyes kocha wa zamani wa Manchester United ameondoka kwenye timu hiyo baada ya kuipa mafanikio makubwa kwa misimu miwili lakini mashabiki wa kikosi hicho cha London wamekuwa wakilalamika kuwa amebadilisha staili ya timu hiyo ya kiuchezaji na sasa havutii tena.
Lopetegui ambaye amewahi kufanya kazi na timu kubwa kama Porto, Real Madrid, Sevilla na Wolves ya England ataanza kazi yake rasmi kwenye timu hiyo iliyomaliza nafasi ya tisa kwenye ligi, Julai Mosi.
“Najisikia vizuri sana, ni jambo la furaha kuona nakuwa sehemu ya klabu hii kubwa, tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuhakikisha kuwa tunatimiza malengo ya timu hii," alisema Lopetegui.
Mbali na mafanikio mengine, Moyes msimu wa 2022–23 aliiwezesha timu hiyo kwa mara ya kwanza kutwaa ubingwa wa UEFA Europa Conference League.