Isak awasili Liverpool kufanyiwa vipimo vya afya
Muktasari:
- Baada ya kumnasa Isak, Majogoo wa Anfield bado wanamuwinda beki wa Crystal Palace, Marc Guéhi ambaye wamepanga kumnasa kabla ya dilisha hili la majira ya kiangazi kufungwa.
Liverpool, England. Mshambuliaji wa kimataifa wa Sweden, Alexander Isak, amefika Liverpool kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya ikiwa ni hatua ya mwisho kabla ya kukamilisha rasmi uhamisho wake kutoka Newcastle United wenye thamani ya Paundi milioni 125 (Sh423 bilioni) kujiunga na Liverpool FC.
Mazungumzo baina ya Newcastle United na Liverpool yalikamilika Jumapili usiku na makubaliano rasmi kati ya klabu hizo sasa yamekamilika.
Isak amekubali mkataba wa miaka sita na Liverpool, huku vyanzo kutoka Newcastle United vikibainisha kuwa jumla ya thamani ya uhamisho huo ni takriban Paundi milioni 130 (Sh440 bilioni) na mauzo hayo yamethibitishwa na wamiliki wa klabu hiyo.
Newcastle ilikuwa tayari kuangalia uwezekano wa Isak kuondoka baada ya mshambuliaji huyo kutoa ishara mwishoni mwa msimu uliopita kwamba angependa kuondoka Klabuni hapo.
Hata hivyo, taarifa rasmi ya klabu wiki mbili zilizopita ilibainisha kwamba masharti ya uhamisho bado hayakukamilika kwani masharti hayo yalihusisha ofa inayokubalika kutoka Liverpool pamoja na mchezaji mbadala wa Isak kuthibitishwa.
Newcastle ilijaribu kumshawishi Isak kubaki St James’ Park, lakini baada ya ujumbe rasmi kutoka kwa wamiliki wake, mchezaji huyo aliendelea kushikilia msimamo wake wa kuhamia Liverpool.
Isak ambaye msimu uliopita alifunga mabao 23 kwenye Ligi Kuu England, aliwaambia wamiliki wake kwamba angeendelea kushikilia msimamo wa kutocheza hadi angepewa ruhusa ya kuondoka.
Mazungumzo ya siri yamekuwa yakifanyika kwa wiki nzima kuelekea kuondoka kwake, huku wakala wake Vlado Lemic akishiriki kikamilifu kuhakikisha dili hilo linakamilika kwani mpaka kufikia Jumapili usiku, makubaliano kati ya vilabu hivyo viwili yalifikia pazuri na Isak sasa yuko tayari kujiunga na Liverpool.
Katika hatua nyingine, Newcastle tayari imemsajili mshambuliaji wa Ujerumani Nick Woltemade kwa rekodi ya klabu ya Paundi milioni 69 (Sh233 bilioni) huku ikitarajia kumwongeza Yoane Wissa kutokea Brentford.
Baada ya kumnasa Isak, Majogoo wa Anfield bado wanamuwinda beki wa Crystal Palace, Marc Guéhi ambaye wamepanga kumnasa kabla ya dilisha hili la kiangazi kufungwa.