HISPANIA ILIMKATAA DIOGO JOTA

Muktasari:
- Mkataba wa Diogo Jota na Liverpool ulikuwa umalizike miaka miwili ijayo.
Julai 3, 2025 dunia ilishtushwa na habari mbaya za kifo cha mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Ureno, Diogo Jota.
Nyota huyo wa miaka 28, alifariki kwa ajali ya gari akiwa na mdogo wake, Andre Silva nchini Hispania safarini kwenda England akitokea kwao Ureno.
Kwa mujibu wa mashahidi, gari lake aina ya Lamborghini lilishika moto baada ya kishindo cha ajali na kuteketea kiasi cha kuunguza hadi mimea iliyokuwa pembani ya barabara.
Askari wa huduma za dharura wakafika mapema sana lakini hawakuweza kufanya chochote cha kuokoa maisha yake.
Ajali ilitolea saa 12:30 asubuhi huko Zamora, kaskazini-magharibi mwa Hispania.
Sababu za ajali zinatajwa kuwa ni kupasuka kwa tairi kati akilipita garj lingine, hii ni kwa mujibu wa mamlaka za salama barabarani.
Ajali hiyo mbaya ilitokea katika eneo la Palacios de Sanabria nchini Hispania.
Ni huko Hispania ambako kifo kilimkuta, ndio kumenifanya niandike makala hii.
Mashabiki wa soka nchini kwao Ureno ambako alichezea timu mbili Paços de Ferreira na FC Porto, na hadi timu ya taifa, watamkumbuka Jota kama mmoja wa wachezaji wao bora katika kizazi chake.
Ni hivyo hivyo, hata England ambako alichezea Wolverhampton Wanderers na Liverpool, watamkumbuka Jota kama nyota wao bora.
Tena Liverpool walienda mbali na kumtungia wimbo wakimsifu kwamba alikuwa bora kuliko Luis Figo.
He is a lad from Portugal
Better than Figo don't you know
Ooh...his name is Diogo
Ni kijana kutoka Ureno
Ni bora kuliko Figo, hujui?
Oooh...jina lake ni Diogo
Oh, he wears the number twenty
He will take us to victory
And when he's running down the left wing
He'll cut inside and score for LFC
Oh, huvaa namba ishirini
Atatupeleka kwenye ushindi
Na anapokimbia wingi ya kushoto
Ataingia ndani na kuifungia LFC
Hivyo ndivyo alivyoheshimiwa na mashabiki wake.
Lakini hata hivyo, hali ilikuwa tofauti nchini Hispania.
Mwaka 2016 klabu ya Atletico Madrid ya Hispania ilimnunua kijana mdogo wa miaka 19 aliyeitwa Diogo Jota kutoka klabu ya Paços de Ferreira ya Ureno.
Atlético Madrid ambayo ilitoka kupoteza fainali ya ligi ya mabingwa kwa Real Madrid, ilitoa kiasi cha euro milioni 7 kumnunua dogo huyo aliyefunga mabao 14 na kutoa pasi 10 za mabao kwenye ligi ya Ureno.
Lakini hata hivyo, kwa mshangao wa wengi, Diogo Jota hakuwahi hata kuvaa jezi ya Atlético de Madrid kwenye mechi rasmi.
Hakuwahi kucheza kwenye ule uwanja wao wa zamani wa Vicente Calderón, wala uwanja mpya wa Metropolitano.
Yaani mwezi mmoja tu baada ya kumnunua, Atletico Madrid ikaamua kumtoa kwa mkopo kwenda FC Porto ya kwao Ureno.
Huko akacheza kwa mafanikio sana lakini aliporudi Atlético Madrid baada ya mkopo wake, hali ikawa ile ile.
Akatolewa tena kwa mkopo bila kucheza hata mechi moja, safari hii kwenda Wolverhampton ya England.
Huko akakiwasha sana hadi klabu hiyo kuamua kumnunua moja kwa moja kwa euro 14 milioni mwaka 2018.
Akacheza hapo hadi 2020 aliponunuliwa na Liverpool. Alienda Liverpool mwaka 2020, akachagua jezi namba 20 na msimu uliopita akaisaidia Liverpool kutwaa ubingwa wa 20.
Na akiwa Liverpool akawa kipenzi cha mashabiki. Wolves alikuwa kipenzi cha mashabiki na hata Ureno alikuwa kipenzi cha mashabiki, kasoro Hispania.
Hapa utaona kabisa kwamba Hispania haikumtaka kabisa Jota, ndio maana haikuwahi kumpa nafasi hata kidogo.
Licha ya kununuliwa na Atlético Madrid, lakini hakuwahi kupewa hata mechi moja...aliishia kutolewa kwa mkopo juu kwa juu.
Na imekuwa bahati mbaya sana kwamba hata maisha yake yameishia hapo.
Damu yake na Hispania hazikuendana.
ANGEWEZA KUEPUKA KIFO?
Taarifa zinasema Diogo Jota angeweza kuepuka kifo endapo angezingatia mambo makuu matatu kama ifuatavyo.
ANGEPANDA NDEGE
Diogo Jota alikuwa kwao Ureno ambako alifanyiwa upasuaji mdogo wa mapafu kutibu tatizo la ugonjwa unaifahamika kama pneumothorax.
Alitakiwa afanyiwe upasuaji huo mwezi Mei baada ya ligi kuisha lakini akaichelewesha ili acheze fainali za Ligi ya Mataifa ya Ulaya.
Kwa hiyo baada ya mashindano na nchi yake kutwaa ubingwa, ndio akafanyiwa upasuaji huo.
Na baada ya kukaa sawa akataka kurudi klabuni kwake Liverpool kwa ndege kujiandaa na msimu mpya.
Lakini daktari wake, Miguel Goncalves aliyemfanyia upasuaji kwenye hospitali ya São João jijini Porto, akamshauri asipande ndege bali aende kwa gari.
Kwa kuwa upasuaji wake ulihusu mapafu, angeweza kupata shida ya kupumua akiwa hewani.
Lakini hata hivyo, alishauriwa apande gari hadi Santander Hispania kisha apate boti hadi England.
Lakini akiwa njiani ndio akapata hiyo ajali. Labda angeweza kuepuka ajali hii kama angesafiri kwa ndege.
ASINGETUMIA LAMBORGHINI
Gari aliyotumia ni aina Lamborghini ambayo sio gari nzuri kwa safari ndefu kama ile.
Kutoka Porto Ureno alikoanzia safari yake hadi Santander Hispania ambako angepanda boti ni mwendo wa saa 8.
Lamborghini sio gari kumudu safari ndefu namna hiyo.
Daktari wake amesema Jota alitakiwa kupumzika njiani katika mji wa Burgos kabla ya kuendelea na safari kwenda Santander.
Haijulikani kama walipumzika njiani au la. Lakini yote kwa yote Lamborghini ni gari ya starehe kwa safari fupi fupi za mjini.
Lakini hata hivyo, hayo yote hayana maana tena kwa sasa.
Ni pigo kubwa sana kwa familia.
Baba na mama wamepoteza watoto wawili kwa mpigo.
Mke wake kapoteza mume ambaye amefunga naye ndoa chini ya wiki mbili nyuma.
Watoto wadogo watatu wamepoteza baba.
Katika hali ya kiungwana na kuwafariji wafiwa, klabu ya Liverpool itaendelea kuilipa familia mshahara hadi mkataba wake utakapoisha.
Mkataba wa Diogo Jota na Liverpool ulikuwa umalizike miaka miwili ijayo.
Mshahara huo ni kiasi cha shilingi bilioni saba za Tanzania.
Liverpool pia ina mpango wa kuistaafisha jezi namba 20 ya Diogo Jota.