Prime
MZEE WA FACT: C tatu zimewapa ushindi Yanga

Muktasari:
- Unaweza kudhani nini kingewakuta bodi ya ligi na TFF endapo wangekataa kuahirisha tena mechi?Yanga sio wa kawaida!
Kuna kanuni ya kimkakati inayoitwa “Rule of 3Cs” yaani sheria ya C 3 ambayo ipo duniani kwa miaka zaidi ya 1000 sasa.
Hii ni kanuni inayotumiwa na serikali, taasisi, asasi, makampuni ya biashara na hata watu binafsi katika kujenga ushawishi ili kufanikisha mambo yao.
C hizi tatu ni Convince, Confuse, Corrupt, ambazo kwa Kiswahili ni Shawishi, Changanya, Haribu. Kwa kifupi, unatengeneza ushawishi kwa watu usipofanikiwa, unawachanganya, usipofanikiwa unaharibu kila kitu ili muanze upya.
Hii C ya tatu, yaani Corrupt au haribu, ni hatari sana, ikifikia hatua hii ndio utasikia vita vimelipuka, au mtu kauawa au tukio lolote kubwa, la hatari.
Maneno haya "convince," "confuse," na "corrupt" huwakilisha namna tofauti za kushawishi au kumvuta mtu upande wako.
"Convince" (Shawishi)
Maana yake kushawishi au kumsihi mtu hadi akubaliane na wewe, aghalabu kwa hoja au ushahidi.
"Confuse" (Changanya)
Maana yake kukifanya kitu kisieleweke moja kwa moja au kigumu kueleweka, aghalabu kwa kudanganya au kutengeneza hofu.
"Corrupt" (Haribu)
Maana yake kuchafua hali ya hewa na kukifanya kitu kionekane cha hovyo au kama ni mtu kumvunjia heshima, kumfedhehesha na kumfanya aonekane asiye na maana kabisa.
Na hizi ndizo hatua ambazo Yanga walipitia katika kufanikisha mpango wao wa kutocheza mechi ya marudio na watani wao Simba, hadi watake wao wenyewe.
C ya kwanza (Convince)
Yanga walianza taratibu na kwa amani kabisa wakijaribu kuona ni namna gani mamlaka za soka zinaweza kufanya kile ambacho wanataka baada ya kushindikana kwa mchezo wa Machi 8.
Walitumia sauti ya upole wakiomba waelezwe sababu za kushindikana kwa mechi hiyo.
Wakaenda CAS ambako walikwama wakarudi na kuja kuzindua kaulimbiu ya HATUCHEZI!
Lakini hakuna aliyewasikiliza na hatimaye bodi ya ligi wakatangaza tarehe mpya ya mechi, Juni 15, 2025.
Mivutano ikaendelea na Juni 8, Bodi ya Ligi ikawaita Yanga ili kulijadili jambo hili.
Yanga wakaitikia wito na kwenda kwenye kikao.
C ya pili (Confuse)
Baada ya kuona C ya kwanza haijatoa majibu, wakahamia kwenye C ya pili kuchanganya.
Walianza kuitumia C hii baada ya walipokuwa kwenye kikao na Bodi ya Ligi, Juni 8, 2025.
Wakatoa masharti manne ndani ya kikao hicho, Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ajiuzulu, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi ajiuzulu na Katibu Mkuu wa TFF pia ajiuzulu, halafu kamati ya saa 72 ivunjwe na bodi ya ligi kiwe chombo huru.
Hakika masharti haya yaliwachanganya sana watu wa bodi ya ligi kwenye kikao. Yanga walipoondoka, kikao kikaanza kufikiria kuahirisha tena mechi, lakini wakakwama, sababu itakuwa nini?
Baada ya kuwachanganya bodi ya ligi kwenye kikao, wakatoka nje kuwachanganya raia.
Ofisa habari wao, Ali Kamwe, akaitisha mkutano na vyombo vya habari na kuanza kuishambulia TFF.
Wakaibua hoja ya zawadi za ubingwa wa mashindano mbalimbali ambazo walitakiwa kupewa na TFF lakini hawakupewa.
Kutokana na hilo wakatangaza msimamo mpya, kwamba hawatacheza fainali ya Kombe la CRDB kule Zanzibar, Juni 28.
Madai haya yaliyotolewa kwa sauti ya herufi kubwa, yaliuchanganya umma, mamlaka za soka, TFF na hata wadhamini CRDB.
Wakaja na msimamo mwingine kwamba endapo watakatwa alama 15 kwa kutocheza mechi ya Juni 15 basi hawatocheza mechi zinazokuja na msimu ujao hawachezi ligi kabisa.
TFF wakachanganyikiwa, Bodi ya Ligi wakachanganyikiwa na CRDB wakachanganyikiwa kila mtu akachanganyikiwa kwa wakati wake.
Hapo tayari Yanga walikuwa wameshafanikiwa. TFF ikawaita Yanga Juni 10 kujadili madeni yao, lakini katika muendelezo wa kuwachanganya, Yanga wakapeleka barua na kuwaachia, bila maongezi yoyote.
Barua hiyo imejaa hati ya madai ya malipo ya fedha zao ambazo Juni 8 walisema wanaidai TFF wakaondoka.
C ya tatu (Corrupt)
Licha ya kuchanganyikiwa, lakini bado msimamo wa bodi ya ligi ulikuwa mechi ichezwe kama ilivyopangwa, Juni 15.
Yanga sasa wakaja na C ya tatu, yaani kuharibu. Hapa ilikuwa kuharibu kila kitu kuiharibu bodi ya ligi na TFF kama taasisi na kuharibu heshima na kazi za watendaji wake.
Wakaachana na wote na wakamtafuta namba moja wa nchi.
Hii ilikuwa silaha kubwa zaidi ambayo Yanga waliamua kuitumia katika kufanya uharibifu.
Hatuna shabaha ambayo ingekoswa kwa silaha na ndivyo ilivyokuwa wa mamlaka za soka.
Bila kupoteza muda, bodi ya ligi wenyewe wakatangaza kuahirisha mechi hadi Juni 25, kama walivyotaka Yanga.
Wakatangaza kujiuzulu kwa mwenyekiti wa bodi ya ligi, Steven Mguto kama walivyotaka Yanga.
Wakatangaza kwamba Rais wa TFF amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo, kama walivyotaka Yanga.
Taarifa hizi zikaambatana na picha ya uongozi wa Yanga ukiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Unaweza kudhani nini kingewakuta bodi ya ligi na TFF endapo wangekataa kuahirisha tena mechi?
Yanga sio wa kawaida!