Haya ndiyo mambo anayotaka kocha mpya Yanga

Kocha mpya wa Yanga, Sead Ramovic
Muktasari:
- Ukitazama muda ambao Gamondi anaondoka timu ikiwa kwenye mashindano ikibakiza siku nane kabla ya kucheza mechi za makundi za ligi ya Mabingwa, kupata kocha anayeweza kuendeleza falsafa za mtangulizi wake lilikuwa jambo muhimu.
Dar es Salaam. Yanga itaanza maisha rasmi kesho chini ya zama za kocha Sead Ramovic aliyekuja kuchukua nafasi ya Muargentina Miguel Gamondi.
Ramovic ataanza kazi kesho Jumatatu baada ya utambulisho mbele ya kikosi cha timu hiyo kitakaporejea kambini baada ya kupewa mapumziko ya siku mbili wikiendi hii.
Inawezekana Ramovic asiwe kocha mwenye mafanikio makubwa kwenye soka la Afrika lakini kuna mambo mawili makubwa yaliyowapelekea viongozi wa Yanga kumpa nafasi hiyo.
Yanga imefanya maamuzi ambayo yamewashtua wengi kwa kumuondoa Gamondi ambaye aliwapa mafanikio makubwa msimu uliopita, akishinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la CRDB Shirikisho, akiifikisha Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na msimu huu akianza msimu kwa kuchukua Ngao ya Jamii.
Ukitazama muda ambao Gamondi anaondoka timu ikiwa kwenye mashindano ikibakiza siku nane kabla ya kucheza mechi za makundi za ligi ya Mabingwa, kupata kocha anayeweza kuendeleza falsafa za mtangulizi wake lilikuwa jambo muhimu.
Ramovic ni kocha wa soka la kushambulia kwa nguvu, kukaba kwa haraka lakini hesabu sahihi za kuzuia hiki ndicho amekifanya kwenye timu alizopita ikiwemo klabu ya mwisho ya TS Galaxy ya Afrika Kusini.
Kocha huyo raia wa Ujerumani, falsafa yake hiyo haitofautiani sana na ile ya Gamondi eneo ambalo halitawapa kazi ngumu wachezaji wake kushika anachokitaka kifanyike.
Eneo lingine ambalo Yanga itafaidi kwa Ramovic ni uimara wake kwenye kusimamia nidhamu ya wachezaji kwa kuwa huyu sio kocha anayetamani kuona mchezaji wake anafanya mambo yaliyo nje na utaratibu.
Moja ya sababu kubwa ya mabadiliko ya kumtoa Gamondi ni baada ya baadhi ya viongozi wa Yanga kuona kumeanza kuenea nidhamu mbovu kwa wachezaji wake kujikita kwenye starehe.
Viongozi wa Yanga kama wanataka kufanikiwa kwenye hili wanapaswa kumuachia Ramovic afanye yake ndani ya kikosi hicho kwani mchezaji atakayebainika kufanya jambo lolote la kukosa nidhamu hatasita kumpa adhabu kubwa na ikibidi hata kumfukuza.
Kocha huyu anapenda kufanya kazi na wachezaji wanaoweza kujitambua ili timu ipate huduma sahihi ya vipaji vyao na watakaojituma wakati wote kiushindani.
Huku kwenye timu zote alizopita akipiga marufuku matumizi ya kilevi kwa wachezaji wake lakini pia akitaka kila mmoja awe anafuata utaratibu uliowekwa.