Haaland aishika pabaya RB Leipzig
Leipzig, Ujerumani. Timu ya soka ya RB Leipzig itakuwa na kibarua cha kumdhibiti Erling Haaland asiendeleze ubabe dhidi yao itakapoikaribisha Manchester City katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, leo.
Mshambuliaji huyo ambaye amekuwa mwiba dhidi ya timu hiyo kila wakutanapo katika mashindano tofauti kulinganisha na timu nyingine za Ujerumani alizowahi kukutana nazo nyakati tofauti.
Mabao sita ambayo imeruhusu timu hiyo kutoka kwa nyota huyo yameifanya Leipzig kuwa timu ya Ujerumani iliyofungwa mara nyingi zaidi na Haaland tangu alipoanza kucheza soka la ushindani.
Na hapana shaka takwimu hizo za Haaland dhidi ya RB Leipzig na mwendelezo wa kufumania nyavu alionao msimu huu vinategemewa na kocha wa Manchester City, Pep Guardiola kuwa silaha muhimu kati ka mchezo huo utakaochezwa katika Uwanja wa RB Arena, Leipzig.
Manchester City inaingia uwanjani ikitaka kulipa kisasi cha kuchapwa mabao 2-1 katika mchezo wa mwisho baina ya timu hizo uliochezwa uwanjani hapo Desemba 7, 2021, ingawa kabla ya hapo ilichapa Leipzig mabao 6-3 katika mechi ya mzunguko wa kwanza msimu huo katika Uwanja wa Etihad, Manchester.
Timu hizo zinakabiliana zikiwa zimetoka kupata matokeo yanayofanana kwenye mechi tano zilizopita katika mashindano tofauti ambapo kila moja imeshinda mara tatu, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.
Wakati wenyeji Leipzig ikiwa imefunga angalau bao katika mechi nne zilizopita za Ligi ya Mabingwa Ulaya, Manchester City imefunga bao katika mechi mbili kati ya nne zilizopita.
Kocha wa Leipzig, Marco Rose alisema wanafahamu wanakutana na timu bora, lakini watapambana ili washinde.
“Tumewahi kuonyesha kuwa tunaweza kuwashangaza watu na tuko tayari kwa changamoto,” alisema Rose.
Naye Guardiola alisema:” Heshima kubwa kwao (Leipzig). Ni timu ndogo yenye falsafa inayoeleweka.” Mechi nyingine leo ni kati ya Inter Milan dhidi ya Porto.