Gyokeres aingia kwenye rekodi Arsenal
Mshambuliaji wa Aresenal, Victory Gyokeres. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Jumla ya mabao yake katika mashindano yote msimu huu imefikia 21, na kumfanya kuwa mchezaji wa pili tu kufikisha zaidi ya mabao 20 katika msimu wake wa kwanza akiwa Arsenal katika karne hii.
London, England. Mabao mawili aliyofunga Viktor Gyokeres dhidi ya Fulham juzi yamemfanya mshambuliaji huyo mpya wa Arsenal kuweka rekodi mpya kwenye kikosi hicho.
Mshambuliaji huyo amekuwa akijadiliwa sana tangu alipojiunga na klabu hiyo ya kaskazini mwa London majira ya kiangazi kwa ada inayofikia paundi 63.5 milioni.
Msimu uliopita, Gyokeres alijijengea sifa kama mmoja wa washambuliaji hatari zaidi duniani, akifunga mabao 39 na kutoa pasi za mabao sita katika michezo 33 akiwa na klabu ya Sporting ya Ureno.
Ingawa mwanzoni mwa msimu huu kiwango chake kilikosolewa na baadhi ya mashabiki wa Arsenal na wengine, mchezaji huyo wa Sweden sasa ameonyesha kiwango bora katika miezi ya hivi karibuni.
Mabao yake mawili dhidi ya Fulham Jumamosi yalimfanya afikishe jumla ya mabao 14 ya ligi msimu huu, huku akiwa ameongeza mengine matano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na bao moja kwenye Kombe la EFL.
Hivyo, Jumla ya mabao yake katika mashindano yote msimu huu imefikia 21, na kumfanya kuwa mchezaji wa pili tu kufikisha zaidi ya mabao 20 katika msimu wake wa kwanza akiwa Arsenal katika karne hii.
Mchezaji wa mwisho kufanya hivyo alikuwa Alexis Sanchez, aliyefunga mabao 25 katika mashindano yote msimu wa 2014/15 baada ya kuwasili kutoka Barcelona.
Ingawa haikuwa katika msimu wake wa kwanza, Bukayo Saka ndiye aliyekuwa wa hivi karibuni zaidi kufikisha mabao 20, akifunga idadi hiyo katika msimu wa 2023/24.
Saka pia alirejea vizuri katika kikosi cha kwanza tangu Machi alipoanza dhidi ya timu ya West London, akifunga bao moja na kutoa pasi ya bao kwa Gyokeres, na hivyo kufikisha jumla ya mchango wake wa mabao msimu huu kuwa 12.