Penalti zilivyoituliza Atletico, Arsenal usiku wa Ulaya
Mshambuliaji wa Arsenal, Noni Madueke wakati akifanyiwa madhambi na beki wa Atletico, Dávid Hancko kabla ya mwamuzi kukataa faulo hiyo baada ya kuthibitisha kwenye VAR. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Atletico hawajafungwa katika michezo sita iliyopita ya hatua ya mtoano dhidi ya timu za England.
Madrid, Hispania. Atletico Madrid na Arsenal zimetoka sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uliotawaliwa na penalti.
Wakiwa wanacheza nusu fainali ya pili mfululizo ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza katika historia yao, Arsenal walijua wanahitaji mwanzo imara wakiwa Hispania, ambako Atletico hawajafungwa katika michezo yao sita iliyopita ya hatua ya mtoano ya michuano hii dhidi ya timu za England, ikishinda tatu sawa na sare.
Wakiungwa mkono na mashabiki wao wenye hamasa kubwa, kikosi cha Diego Simeone kilipata nafasi ya kwanza ya maana, ambapo David Raya aliokoa kwa ustadi shuti la kupinda la Julian Alvarez na kulipeleka nje ya lango.
Arsenal walijibu shambulizi hilo baada ya nahodha Martin Odegaard kuzuiwa shuti lake na Johnny Cardoso, kabla ya Noni Madueke kupiga shuti lililokwenda nje akiwa umbali wa mita 25.
Baada ya kushinda mechi tano kati ya sita zilizopita za Ligi ya Mabingwa ugenini msimu huu sare ikiwa moja, Arsenal waliendelea kutawala mchezo, na juhudi zao zilizaa matunda kabla ya mapumziko wakati David Hancko alipomwangusha Viktor Gyokeres ndani ya eneo la hatari.
Gyokeres alisimama kupiga penalti na kufunga kwa kujiamini dhidi ya Jan Oblak, akifunga bao lake la 19 msimu huu na kuipa Arsenal uongozi kabla ya mapumziko.
Atletico walirejea kipindi cha pili kwa nguvu, Julian Alvarez akipiga mpira wa adhabu uliogonga wavu wa pembeni, huku Ademola Lookman akizuiwa kwa karibu na Raya.
Shinikizo lao lilizaa matunda walipopata penalti baada ya Ben White kushika mpira ndani ya boksi. Alvarez hakukosea alipofunga penalti na kusawazisha.
Atletico walikaribia kuongoza dakika ya 63 wakati Antoine Griezmann alipiga mpira uliogonga mwamba wa juu wa lango.
Licha ya kuendelea kuwa tishio, kumalizia nafasi kwa uzembe kutoka kwa Lookman na uokozi mzuri wa Raya uliifanya Arsenal kubaki salama.
Arsenal walidhani wamepata penalti ya pili baada ya Hancko kumchezea rafu Eberechi Eze, lakini uamuzi huo ulifutwa baada ya ukaguzi wa VAR.
Katika dakika za mwisho, Atletico walishindwa kurejesha makali yao ya ushambuliaji, huku Arsenal wakidhibiti mchezo na kubeba matokeo mazuri kuelekea mchezo wa marudiano Jumanne ijayo huko London Kaskazini.
Kwa upande wa Atletico, wataenda ugenini wakiwa na matumaini makubwa licha ya sare, wakikumbuka wamefanikiwa kusonga mbele katika nusu fainali sita kati ya saba zilizopita kwenye mashindano ya UEFA.