Gamondi, Fadlu wanyoosha upanga juu

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi (kushoto) akizungumza jambo na Fadlu Davids wa Simba walipokutana kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa Agosti 7, 2024 kuzungumza na waandishi wa habari kuekea mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii.
Muktasari:
- Dabi ya Simba na Yanga kesho inatarajiwa kuwa na msisimko mkubwa baada ya maandalizi ya kila kitu kwenye Pre Season huku makocha wakiutaka ushindi.
Daar es Salaam. Makocha wa Yanga na Simba, Miguel Gamond na Fadlu Davids ni kama wamenyoosha upanga juu ishara ya kuwa tayari na vita ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa kwa kila mmoja kueleza alivyojipanga kukabiliana na mwenzake kwenye mchezo huo wa Dabi.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa makocha hao kukutana huku ikiwa ni mara ya pili kwa vigogo hao wa soka la Tanzania kuonyeshana ubabe katika mfumo mpya wa uchezaji wa michezo ya ufunguzi wa Ligi, mwaka jana Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti jijini Tanga.
Katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika leo Jumatano Agosti 7, 2024 kwenye Uwanja wa Mkapa, kocha wa Yanga, Gamondi alikumbushiwa matokeo ya Ngao ya Jamii msimu uliopita na kusema hayana nafasi kwake maana huu ni mchezo mpya.
"Mechi zilizopita kwangu hazina nafasi kuelekea mchezo ujao kwa sababu huu ni mchezo mpya, hatujui sana kuhusu Simba, jambo muhimu ilikuwa ni sisi kujiandaa na sio kuwafuatilia, naweza kusema tumefanya hilo kwa zaidi ya asilimia 75,"
"Tupo tayari kwa ajili ya kukabiliana nao, siku zote nimekuwa nikitoa heshima kwa wapinzani wangu, najua kuwa Simba inawachezaji wapya na benchi jipya la ufundi hivyo watakuwa hari mpya kwa hiyo itakuwa mechi ngumu sana na naweza kuiweka katika mzani wa 50/50," amesema Gamondi na kuongeza;
"Kikawaida ni ngumu kujua nini kinaweza kutokea, kesho ni mchezo wa mashindano hivyo utawakuwa mchezo mgumu, naamini utakuwa mchezo mzuri na wa ushindani lakini mpango wangu ni kupata ushindi kwenye mchezo huo, ni kweli kwamba kwenye mchezo uliopita (dhidi ya Red Arrow) tulipoteza sana nafasi hivyo tumekuwa kazi ya kufanya msahihisho."
Kwa upande wake, Fadlu anaamini wanaweza kufanya vizuri katika mchezo huo licha ya mradi wa kuijenga Simba tishio kuwa na wiki tatu lakini kwake sio kikwazo maana anauchukulia mtanange huo kama ilivyo mengine waliyocheza.
"Huu mchezo utaonyesha ni namna gani huu msimu utakuwa baada ya kuwa na wiki tatu kuanza kwa projekti. Nauchukulia huu mchezo kama ilivyo mengine, tutaingia na mpango wa kusaka matokeo ya ushindi," amesema Fadlu na kuongeza;
"Yanga ni timu nzuri na tumewaona wana namna tofauti ya uchezaji lakini tuna wachezaji wenye vipaji sana, wapo wenye uwezo wa kucheza uwezo wa katika nafasi tofauti, wapo wenye uwezo wa kukaa na mipira, ni suala la kujenga tu kikosi na kuamini katika lile ambalo tutakuwa tukilifanyaa. Kiukweli mashabiki wategemee tu mazuri."
Msimu uliopita Simba ilitwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga katika fainali kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya dakika 90 za mchezo huo kumalizika kwa suluhu.
Mshindi wa mchezo kati ya Yanga dhidi ya Simba atacheza na Azam/Coastal Union ambao wanacheza nusu fainali ya pili Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan kesho.
Fainali ya Ngao ya Jamii itachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Agosti 11.