Prime
Dili la Mzize lawafunika Chama, Luis
Muktasari:
- Kiujumla, Yanga katika mwaka huo ilitumia Sh22 bilioni, ambazo pesa ya Mzize Sh3 bilioni inakuwa ni sawa na asilimia 13.64 ya bajeti nzima ya Yanga ya 2023-24
Akiwa ndio kwanza ameitumikia Yanga kwa misimu miwili na nusu tu, mabilioni ya pesa yanamuita Clement Mzize, akiwindwa na klabu kadhaa ikiwamo ofa mpya nono kutoka Al Ettihad ya Libya.
Straika huyo zao la timu ya vijana ya Yanga, anatakiwa na klabu hiyo kwa ada ya uhamisho ya Sh3 bilioni, huku ada yake binafsi ya kusaini mkataba (sign-on fee) ni zaidi ya Sh 1.1 bilioni kwa miaka miwili, hiyo ni mbali na mshahara wa Sh50 milioni (ambao kwa miaka miwili ni sawa na Sh1.2 bilioni).
Kwa maana hiyo, pamoja na bonsai nyingine, kuna zaidi ya Sh2.5 bilioni zitakazoingia kwenye akaunti binafsi ya Mzize, kama dili hilo na Ettihad litatimia.
Mshambuliaji huyo mrefu, mwenye nguvu, kasi, mashuti makali na anayetumia miguu yote miwili anaelezwa kuvutiwa na ofa hiyo ambayo kiujumla itamfanya kuwa mchezaji ghali zaidi aliyepata kununuliwa nchini, akifunika wote wa kigeni na wazawa.
MBWANA SAMATTA
Kufikia sasa, mchezaji mzawa aliyenunuliwa kwa pesa nyingi moja kwa moja kutoka klabu ya Tanzania kwenda nje ni Mbwana Samatta, ambaye TP Mazembe ya DR Congo ililipa dola 100,000 (sawa na Sh250 milioni) ilipomnasa kutoka Simba 2011. Baadaye Samatta aliuzwa kwa Euro 800,000 (sawa na Sh2.1 bilioni) mwaka 2016 kwenda KRC Genk ya Ubelgiji, ambako pia akaja kuuzwa Januari 2020 kwenda Aston Villa ya Ligi Kuu England kwa Euro 10 milioni (sawa Sh26 bilioni).
CLATOUS CHAMA
Kwa wachezaji wa kigeni, Clatous Chama aliuzwa na Simba kwa Dola 300,000 kwenda RS Berkane ya Morocco mwaka 2022 kabla ya baadaye kurejea Msimbazi na kisha kutua Yanga alipo sasa.
LUIS MIQUISSONE
Luis Miquissone aliuzwa na Simba kwenda kwa mabingwa mara 12 wa Afrika, Al Ahly ya Misri mwaka 2021 kwa ada ya uhamisho ya dola 600,000 (sawa na Sh1.5 bilioni) kabla ya kurejea Simba 2023 ambako kisha alitemwa.
FISTON MAYELE
Straika wa mabao, Fiston Mayele alihama kutoka Yanga SC ya Tanzania kwenda Pyramids FC ya Misri kwa ada ya uhamisho ambayo haikutajwa hadharani lakini ikisemekana kuwa ni dola 900,000 (sawa na Sh2.3 bilioni).
DILI LA MZIZE
Mzize, ambaye msimu wake wa kwanza alikuwa akicheza nyuma ya Mayele baada ya kupandishwa kutoka timu ya vijana ya Yanga, ikiwa uhamisho wake utakamilika, utawafunika wachezaji wote waliowahi kuuzwa nje moja kwa moja kutoka katika klabu za Tanzania na itaigharimu Al Ettihad zaidi ya Sh5.5 bilioni – ukijumlisha ada ya uhamisho na malipo binafsi ya mchezaji.
Pesa hiyo inaweza kufanya jambo moja kati ya haya:
MISHAHARA YA TIMU NZIMA
Kuwa na Mzize kisosini, ni faida kubwa kimichezo kwa Yanga kwa sababu ya mchango wake katika timu hiyo ambayo mwaka huu inatimiza umri wa miaka 90 tangu ilipoasisiwa mwaka 1935, lakini haijawahi kutwaa taji lolote la Afrika ukiacha kuwa ndiyo klabu yenye mafanikio zaidi kwa ndani ikitwaa mataji 30 ya Ligi Kuu.
Na baada ya kutolewa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ikiwa ni misimu miwili tu tangu ilipocheza fainali yake ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kwa kanuni ya mabao nyumbani na ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria, mashabiki wangetarajia kuona mastaa wanabakishwa kikosini na kuongezwa wengine wa ubora zaidi wa kupigania mataji ya Afrika.
Lakini kama inalazimika kuuza kutokana na ofa nono na pengine kutimiza ndoto za mchezaji, kuna mengi Yanga inaweza kufanya kutokana na mkwanja ambao itavuna katika uhamisho huu wa Mzize.
Kwa mujibu wa taarifa ya mapato na matumizi ya mwaka wa mwaka fedha 2023-24, mishahara ya watumishi wa Yanga kuanzia wachezaji, viongozi hadi wafagizi ilikuwa ni Sh7.3 bilioni, jambo ambalo linaonyesha ada ya uhamisho ya Mzize Sh3 bilioni inaweza kulipa mishahara ya wachezaji wote, benchi la ufundi, watumishi na viongozi Yanga kwa karibu nusu ya msimu. Kumbuka hapa tunazungumzia Yanga yenye mastaa wakubwa kama Stephane Aziz Ki, Clatous Chama, Pacome Zouzua, Djigui Diarra. Khalid Aucho na wengineo wote kwa pamoja kikosini.
INANUNUA UWANJA KMC
Yanga bado haina uwanja wake, lakini maajabu ya pesa ya uhamisho ya Mzize (Sh3 bilioni) inaweza kujenga uwanja kama wa KMC, ambao ulijengwa kwa Sh2.7 bilioni na umekuwa ukiinufaisha klabu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni kwani kwa mechi moja unaiingizia Sh6 milioni wakiukodisha.
MAPATO VIINGILIO MIAKA MIWILI
Ada ya uhamisho ya Sh3 bilioni, ambayo Al Ettihad inataka kuipa Yanga ili kumpata Mzize ni zaidi ya mapato ya viingilio vya uwanjani vya mashabiki kwa miaka miwili kwani kwa mujibu wa ripoti ya Yanga ya 2023-24, klabu hiyo ilipata Sh1.49 bilioni kwa mwaka mzima. Hivyo pesa hiyo ni sawa na kusema uwaache mashabiki wa Yanga waingie bure uwanjani katika mechi zao zote za Dar es Salaam na mikoani kwa miaka miwili.
USAJILI YANGA NZIMA
Ada ya uhamisho ya Mzize ya Sh3 bilioni inakaribiana sana na fedha ambazo Yanga ilitumia katika bajeti yake ya 2023-24 ya usajili na uhamisho wa wachezaji ambapo kwa mwaka huo ilitumia Sh3.5 bilioni. Pesa hizo pia ni nyingi zaidi ya gharama ambazo Yanga ilitumia katika usafiri na malazi katika mechi zake za ndani na kimataifa katika kipindi cha 2023-24, ambapo ilitumia Sh2.8 bilioni kwa mujibu wa ripoti hiyo ya timu ya wananchi.
Kiujumla, Yanga katika mwaka huo ilitumia Sh22 bilioni, ambazo pesa ya Mzize Sh3 bilioni inakuwa ni sawa na asilimia 13.64 ya bajeti nzima ya Yanga ya 2023-24.
LIGI YA FURSA
Kuuzwa kwa nyota mbalimbali nje ya nchi kunachangiwa na ubora wa Ligi Kuu Bara ambayo kwa sasa imepanda chati IFFHS kutoka nafasi ya sita Afrika hadi ya nne.
1. Nile Premier League — Misri
2. Botola Pro League — Morocco
3. Ligue 1 — Algeria
4. NBC Premier League — Tanzania
5. Ligue 1 Pro — Tunisia
Ligi Kuu Bara ndiyo ligi pekee barani Afrika ambayo inaonyeshwa mechi zake zote kwa asilimia 100. Hii ni tofauti na nchi kama Afrika Kusini ambayo inaonyesha kwa chini ya asilimia 65 na mataifa mengine yakionyesha chini ya hapo.
Mambo hayo na ushindani, vinachangia kuvutia wachezaji wa mataifa mbalimbali kumiminika kucheza Tanzania kwa kutambua kuwa wataonekana na kupata soko.
ALICHOSEMA ARAFAT
Mwanaspoti ilipowasiliana na Makamu wa Rais wa Yanga, Haji Arafat alisema hakuwa na taarifa za kuletwa kwa ofa hiyo kutoka Libya na kama itakuwepo watatoa taarifa kwa umma.
"Kwa kweli kama ofa hiyo imekuja, bado sijaisikia labda kama ilikuja usiku wa jana (juzi) au asubuhi hii (jana), ila ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho kwa sasa, lakini ngoja nifuatilie," alisema Arafat aliyekiri kuwapo kwa ofa za awali.
Awali, mmoja wa vigogo wa Yanga, alikiri kwamba wameamua kutaka kumuuza Mzize, kutokana na kupokea ofa nyingine na baadhi zikiwa zimevuka kiwango walichokiweka cha Sh2 bilioni walizokuwa wakitaka wapewe ili wamuachie.
Ofa za awali zinadaiwa zilikuwa zimetoka klabu za Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Wydad Casablanca ya Morocco waliorejea mara mbili wakiongeza dau walilolitanguliza mapema la Sh1. 5 bilioni hadi bilioni 2 huku lile la klabu kutoka Ubelgiji ambayo hata hivyo haitajwi ni Sh2.5 bilioni.
TAKWIMU ZA MZIZE
Clement Mzize amechangia mabao tisa ya kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kufunga sita na kutoa asisti za mabao mengine matatu kati ya 32 yaliyofungwa na timu hiyo inayoshika nafasi ya pili na pointi 39, nyuma ya Simba yenye 40.
Katika Ligi ya Mabingwa 2024-25, Mzize amefunga mabao matano kuanzia hatua ya mchujo hadi makundi ambako Yanga ilikwamia.