Dabi ya Kariakoo yazitibulia Azam FC, Coastal Union

Mashabiki mbalimbali wa soka visiwani Zanzibar, wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya mchezo wa Azam na Coastal Union kuwekwa siku moja huku pia ikipigwa 'Dabi ya Kariakoo' kati ya watani wa jadi Yanga na Simba.
Azam FC inakutana na Coastal Union katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii itakayopigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan visiwani Zanzibar, kisha baadae saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa itapigwa nusu fainali ya pili kati ya Yanga na Simba.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashabiki wa soka visiwani hapa wamelitaka Shirikisho la Soka nchini TFF, kutenganisha mechi nyingine ikiwa Yanga na Simba zinacheza siku hiyo.
Shabiki wa soka, Salum Khamisi amesema, kitendo cha mchezo wa Azam na Coastal Union kuwekwa siku moja na mechi ya Yanga na Simba ni kuukosesha mashabiki wengi kujitokeza uwanjani.
"Yanga na Simba ni timu kubwa sasa zikiwa zinacheza ni lazima mashabiki wote akili zao zielekee huko, Azam na Coastal ni mechi nzuri ila imeharibiwa na 'Dabi ya Kariakoo' kuchezwa siku moja na mechi yao," amesema.
Kwa upande wa shabiki aliyejitambulisha kwa jina la Nurath Othman amesema, mchezo wa Azam na Coastal umepoonza na hauzungumzwi sana kama mechi ya Yanga na Simba.
"Tanzania sote tunajua mashabiki wakubwa ni wa Yanga na Simba, sasa hata ukiweka mechi ya aina gani watu watazungumzia hiyo tu, hivyo niwaombe wapangaji wa hizi mechi wajaribu kutofautisha zichezwe siku tofauti."