Chelsea yamhofia Di Maria mtoano Kombe la Dunia

Muktasari:
- Benfica imeongoza kundi C la Kombe la Dunia la Klabu ikiwa na pointi sana huku Chelsea ikimaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi D ikiwa na pointi sita.
Chelsea imemtaja mshambuliaji Angel Di Maria kama mchezaji inayepaswa kumchunga zaidi wakati itakapokutana na Benfica leo katika mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia la Klabu.
Mchezo baina ya timu hizo umepangwa kuchezwa katika Uwanja wa Bank of America, Charlotte, Marekani kuanzia saa 5:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki ambapo mshindi atakutana na mshindi wa mchezo baina ya Palmeiras na Botafogo katika hatua ya robo fainali.
Licha ya Di Maria kuwa na umri wa miaka 37, Chelsea imesema kuwa ndiye mchezaji hatari zaidi katika kikosi cha wapinzani wao hivyo wanajipanga kikamilifu kuhakikisha wanamdhibiti.
“Di Maria anaonyesha namna gani alivyo mchezaji mkubwa. Ni mchezaji wa daraja la juu. Nimeona mechi zake katika mashindano haya.
“Nimeangalia mechi yao dhidi ya Bayern (Munich) kwa dakika chache na nahisi alikuwa mchezaji bora wa mechi hivyo hii inaonyesha namna gani alivyo mzuri. Tunatakiwa kuwa na angalizo kwake,” amesema Meneja wa Chelsea, Maresca.
Beki wa Chelsea, Levi Colwill amesema kuwa Di Maria ni mchezaji ambaye anapokuwa uwanjani hatakiwi kupewa nafasi ya kuwa huru mara kwa mara kwa vile ni hatari.
“Hapana shaka ni mchezaji wa kipekee ambaye wakati nakua nilikuwa namtazama. Uwezo wake wa kiufundi ni wa kushangaza.
Natumaini tutaudhibiti mguu wake wa kushoto na tunatumaini hatofunga bao lolote dhidi yetu,” amesema Colwill.
Ikumbukwe katika mashindano hayo, Di Maria tayari ameshapachika mabao matatu, moja akifunga dhidi ya Boca Juniors na mengine mawili akipachika dhidi ya Auckland City.
Mchezo mwingine leo utaanza saa 1:00 usiku ambao utaIkutanisha Palmeiras na Botafogo.