Chelsea, Man City na kibarua cha kupindua meza Ulaya
Muktasari:
- Chelsea ni miongoni mwa Klabu za Ligi Kuu England ambazo zimewahi kupindua matokeo kibabe na kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati Man City ikihitaji kufanya hivyo kwa mara ya kwanza dhidi ya Real Madrid.
Klabu za Ligi Kuu England zilijikuta katika wakati mgumu wiki iliyopita baada ya timu tatu kati ya tano zinazoshiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuambulia vichapo vya aibu isipokuwa Arsenal na Newcastle ambazo ziliambulia sare.
Vipigo hivyo vya fedhea vilizikuta Chelsea ambayo ilikubali kipigo cha mabao 5-2 kutoka kwa PSG, sawa na Tottenham ambayo nayo ilichapwa kipigo kama hicho na Atletico Madrid na Manchester City ililazwa mabao 3-0 na Mabingwa wa Kihistoria wa michuano hiyo, Real Madrid.
Chelsea imewahi kupindua matokeo katika hatua ya robo fainali dhidi ya PSG mwaka 2014. Picha na Mtandao
Uwezekano wa kupindua meza
Hata hivyo, katika mpira wa miguu lolote huwa linaweza kutokea na hilo limeshathibitishwa na baadhi ya Klabu za Ulaya baada ya kugeuza matokeo na kuwaacha watu midomo wazi wakiwa wanashangaa.
Chelsea ni miongoni mwa Klabu ambazo zimewahi kufanya hivyo kipindi cha nyuma ikigeuza matokeo kibabe na kusonga mbele huku PSG ikiwahi kupinduliwa matokeo na miamba hiyo ya London.
Mwaka 2014 Chelsea ikiwa chini ya kocha Jose Mourinho ilipindua matokeo katika hatua ya robo fainali dhidi ya PSG ambao walikuwa wametangulia kwa ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza iliyokuwa imepigwa Ufaransa.
Katika mechi ya marudiano Chelsea ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge hivyo ikasonga mbele katika hatua ya nusu fainali kwa faida ya bao la ugenini.
Mwaka 2012 Chelsea ilipindua matokeo dhidi ya Napol katika hatua ya 16 bora na kusonga mbele. Picha na Mtandao
Ukiachana na rekodi hiyo, ipo ile ya mwaka 2012 ambayo ilitokea katika hatua ya 16 bora chini ya kocha Roberto Di Matteo ambapo Chelsea ‘The Blues’ walipindua matokeo dhidi ya Napoli waliokuwa wametoka kupata ushindi wa mabao 3-1 nchini Italia lakini kipigo cha mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge kilitosha kuwatupa nje ya mashindano.
Hata hivyo, kibarua cha leo dhidi ya PSG kinaonekana kuwa kigumu kwani Mabingwa hao wa Dunia wanahitaji ushindi wa tofauti ya mabao manne ili kupenya katika hatua ya nusu fainali.
Aliyekuwa shambuliaji wa Tottenham, Lucas Moura, wakati akishangilia bao la tatu katika ushindi wa 3-1 ambao Spurs iliupata ugenini dhidi ya Ajax katika mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mei 9, 2019. Picha na Mtandao
Spurs nao wamo
Tottenham Hotspur pia imewahi kuonesha maajabu mwaka 2019 ilipokuwa chini ya kocha Mauricio Pochettino katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Ajax.
Spurs ilikubali kipigo cha bao 1-0 katika mchezo wa kwanza ilipokuwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani. Hata hivyo, ilijibu mapigo katika Uwanja wa ugenini wa Johan Cruijff jijini Amsterdam, Uholanzi.
Katika mchezo huo wenyeji Ajax walikuwa na nafasi kubwa ya kutinga fainali baada ya kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0 lakini mabao matatu ya Lucas Moura katika kipindi cha pili yalitosha kuipeleka Tottenham katika mchezo wa fainali kwa faida ya mabao ya ugenini kabla ya kanuni hiyo kubadilisha msimu wa 2021/2022.
Kesho Tottenham itakuwa na kibarua kingine cha kupindua matokeo wakati safari hii wakiwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani, jambo ambalo kwa wengi wanaona linaweza kuwa ndoto kutokana na kiwango cha timu hiyo msimu huu kimekuwa cha kusuasua kupata matokeo ya uhakika.
Mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland, (kushoto) mwingine ni beki wa timu hiyo Marc Guehi. Picha na Mtandao
Man City ugumu upo hapa
Kwa upande wa Manchester City, wao hawana rekodi yoyote ya kupindua matokeo katika hatua za mtoano za Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo iwapo ikitokea timu hiyo imefanya hivyo leo dhidi ya Real Madrid, basi itakuwa ni kwa mara ya kwanza katika historia.
Man City inaongozwa na Pep Guardiola na kocha huyo Mhispaniola amewahi kupindua meza akiwa na timu za Barcelona na Bayern Munich.
Katika msimu wa 2010-2011 baada ya kupoteza mechi ya kwanza kwa mabao 2-1 dhidi ya Arsenal katika hatua ya 16 bora. Barcelona ilipindua matokeo baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 katika Uwanja wa Camp Nou.
Vilevile katika msimu wa 2014-2015 akiwa na Bayern Munich, Guardiola aliiongoza Klabu hiyo kupindua matokeo baada ya kutoka kupigwa katika mchezo wa kwanza ugenini kwa mabao 3-1 miamba hiyo ya soka la Ujerumani ilipata ushindi wa mabao 6-1 na kusonga katika hatua ya nusu fainali kwa jumla ya mabao 7-4.
Hata hivyo, akiwa na Man City mambo yanamwendea tofauti kocha huyo kwani hadi sasa ameshindwa kupindua matokeo katika michezo kadhaa ya mashindano hayo.
Guardiola alishindwa kupindua matokeo dhidi ya Liverpool katika msimu wa 2017-2018 ambapo Man City ilipoteza michezo yote miwili ikichapwa mabao 3-0 katika Uwanja wa Anfield kisha kupoteza tena 2-1 kwenye Uwanja wa nyumbani.
Msimu wa 2018-2019 pia ilitupwa nje dhidi ya Tottenham ambayo ilishinda bao 1-0 ikiwa nyumbani wakati katika mchezo wa marudiano Man City ilishinda mabao 4-3 ikitupwa nje kwa faida ya mabao ya ugenini.
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, ambaye bado ajaonesha maajabu ya kupindua matokeo na timu hiyo tangu alipojiunga nayo mwaka 2016. Picha na Mtandao
Awapiga mkwara wachezaji
Baada ya mchezo wa Ligi kuu England dhidi ya West Ham kumaliza kwa sare ya bao 1-1, Guardiola aliwapa siku ya mapumziko wachezaji wake huku akiwambia kuwa yoyote ambaye haamini kama Man City inaweza kupindua matokeo dhidi ya Real Madrid ni bora akae nyumbani.
Kauli hiyo inaashiria kwamba, lolote linaweza kutokea katika mtanange wa leo wa kupindua matokeo pale Etihad baada ya nyota wa kikosi hicho kurejea kambini hapo jana.
Michezo mingine itakayopigwa leo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Arsenal itakabiliana na Bayer Leverkusen kwenye Uwanja wa Emirates huku Sporting CP itakuwa na kibarua kigumu cha kugeuza matokeo dhidi ya Bodo/Glimt ambayo ilishinda mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza.